Hikma za Nahjul Balagha (40)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 40 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Ingawa hii ni sehemu ya 40 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua ni ya 36.
مَنْ أَطَالَ الْأَمَلَ أَسَاءَ الْعَمَلَ
Mwenye tamaa nyingi, huharibu mambo.
Imam Ali AS anasema katika hikma hii ya 36 iliyojaa nuru ya kitabu cha Nahjul Balagha kwamba, tamaa zikiwa nyingi, mwisho wake ni mambo kuharibika. Anasema: Mwenye tamaa nyingi, huharibu mambo.
Hapana shaka kwamba matumaini ndiyo yanayotoa msukumo wa kila harakati anayofanya mwanadamu, iwe kubwa, iwe ndogo. Lakini kama tulivyosema kwenye hikma iliyopita ya 35, tamaa inapokuwa nyingi huwa ni sababu ya mambo kuharibika. Huwa sababu ya kwenda kombo mambo. Huwa sababu ya mabalaa na ni mfano wa maji ya mvua yanapokuwa mingi kupindukia, huvunja kingo za mito na kusababisha mafuriko yenye uharibifu. Tamaa inapovuka kikomo, humkwamisha mtu kwenye kinamasi ya kujaribia kufikia mambo yaliyo muhali kufikiwa. Mtu mwenye tamaa nyingi hudhani mali yake ni ndogo na haina maana. Kiujumla ni kwamba, mtu ambaye ndoto zake ni nyingi kupita kiasi hawezi kufurahia alicho nacho. Mtu mwenye tamaa nyingi huwa hatosheki. Siku zote huwa anatamani vitu vingine na haijalishi kwake ana vitu vingi kiasi gani na hicho anachotamani kukihodhi kina thamani ya ukubwa gani. Mtu mwenye tamaa kupindukia huwa hajali anamiliki nini, anachojali yeye ni kukusanya tu vitu vingine hata visivyo na faida kwake kwa tamaa ya kupata furaha na utulivu wa moyo na kamwe haupati. Kila anapopata kitu alichokuwa anakipigania usiku na mchana, tamaa ya kupata kitu kingine humwongezekea na hayo ndiyo yanayokuwa maisha yake hadi anaingia kaburini.
Ni jambo lililo wazi kwamba, mtu mwenye tamaa kupindukia hulazimika kuelekeza nguvu zake zote kwenye kufanikisha tamaa zake hizo. Watu wengi utaona wako tayari kutumia njia yoyote ile na huhalalisha chochote kile alimradi tu wafikie muradi wao. Hutokezea mara nyingi tu watu hao kujipendekeza na kujidhalilisha mbele ya wengine na mwishowe huishia kwenye maisha ya udhalili na ya duni kama anavyotufundisha hapa Imam Ali AS katika hikma hii ya 36 ya Nahjul Balagha.
Ni wazi kwamba, kama mtu atadhibiti matamanio yake na kukinaika na kile alichoruzukiwa na Muumba wake, hupata muda wa kutosha wa kutekeleza majukumu na wajibu wake mbele ya Mwenyezi Mungu na hujiwekea akiba bora kwa ajili ya maisha ya Akhera. Hupata fursa pia ya kujisafisha na madhambi na kujiweka mbali na mambo ya haramu.
Kuna hadithi maarufu ambayo imepokewa kutoka kwa Mtume Muhammad SAW na Amirul-Muuminin Ali bin Abi Talib (AS), ambayo inasema: Jambo la hatari zaidi tunalolihofia kwenu ni kufuata matamanio ya nafsi na kuwa na tamaa kupindukia, kwani kufuata matamanio ya nafsi humzuia mtu kuifikia haki; na tamaa kupindukia humfanya mtu asahau Akhera.
Mawalii wa Mwenyezi Mungu walikuwa na matumaini madogo sana na muda wote walikuwa wanajiandaa kwa ajili ya safari ya Akhera. Kila sekunde wakiihesabu kuwa ni lahdha ya kuihama dunia na kuelekea Akhera. Hadithi moja yenye maana kubwa iliyonukuliwa kutoka kwa Mtume Muhammad SAW inasema: Naapa kwa Ambaye nafsi ya Muhammad imo mkononi Mwake, kamwe sijawahi kupwesa bila ya kufikiri kwamba huenda nisifikie kupwesua kabla ya kuchukuliwa roho yangu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.