Jan 29, 2024 23:14 UTC
  • Jumanne, tarehe 30 Januari, 2024

Lo ni Jumanne tarehe 18 Rajab 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe 30 Januari 2024.

Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita alifariki dunia mtoto mdogo wa Mtume wetu Muhammad (saw), Ibrahim akiwa na umri wa miezi 18 tu.

Ibrahim ambaye alifariki dunia kutokana na maradhi alikuwa mtoto pekee wa kiume wa Mtume ambaye hakuzaliwa na Bibi Khadija (as). Mama yake alikuwa Maria al Qibtiyya ambaye alitumwa na mfalme wa Misri ya wakati huo kuwa hadimu na mtumishi wa Mtume na aliolewa na mtukufu huyo baada ya kusilimu.

Kifo cha Ibrahim kilimhuzunisha sana Mtume (saw) kwa sababu mtukufu huyo alikuwa akimpenda sana mtoto huyo.     

Kaburi la Ibrahim, mwana wa kiume wa Mtume wetu Muhammad (saw)

Tarehe 18 Rajab miaka 1019 iliyopita alifariki dunia Ibn Samh huko katika mji wa mjini Andalucia.

Msomi huyo wa Kiislamu alikuwa mtaalamu wa hesabu, nyota na tabibu. Alizaliwa katika mji wa Cordoba, Andalucia mnamo mwaka 370 Hijiria. Msomi huyu wa Kiislamu alifanya utalii na utafiti mwingi katika elimu za hesabu na nyota, sambamba na kuwalea wanafunzi wa zama zake.

Kuna vitabu kadhaa vilivyoandikwa na Ibn Samh kwa lugha ya Kiarabu na miongoni mwa vitabu hivyo ni "Al Madkhalu Ila al Handasah", "Al Muamalat" na "Kitabuz Ziyj."   

Siku kama ya leo miaka 90 iliyopita, kilianza kipindi cha uongozi wa Adolph Hitler, dikteta mbaguzi wa Kinazi wa Ujerumani.

Chama cha Taifa cha Kisoshalisti cha Wafanyakazi wa Ujerumani ambacho kiliasisiwa na Hitler kilishinda viti 107 vya bunge katika uchaguzi wa mwaka 1930. Adolph Hitler alijitangaza kuwa kiongozi wa Ujerumani mwaka 1934 baada ya kuwa Kansela na Rais wa nchi hiyo. Hitler aliwafanya mamilioni ya wanadamu kuwa wahanga wa malengo yake ya kibaguzi. Hatua ya Adolph Hitler ya kuivamia Poland mwezi Septemba mwaka 1939 ilichochea Vita vya Pili vya Dunia na hatimaye Ujerumani na waitifaki wake walishindwa katika vita hivyo.

Hitler alijiua mwaka 1945 baada ya Ujerumani kushindwa katika vita hivyo.   

Katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita kiongozi wa taifa la India na mpigania uhuru wa nchi hiyo, Mohandas Karamchand Gandhi aliuawa na kijana mmoja wa Kihindu aliyekuwa na misimamo mikali.

Gandhi alizaliwa mwaka 1869 na baada ya kukamilisha masomo alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya sheria nchini Uingereza. Mohandas Gandhi kwa muda fulani pia alikuwa kiongozi wa wanamapambano wa Kihindi huko Afrika Kusini.

Gandhi pia aliwaongoza wananchi wa India dhidi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza katika kupigania ukombozi wa nchi hiyo. India ilipata uhuru mwaka 1947 chini ya uongozi wa Gandhi.   

Mohandas Karamchand Gandhi

Katika siku kama ya leo miaka 76 iliyopita Orville Wright, mmoja wa waundaji wa ndege ya kwanza inayotumia injini duniani, alifariki dunia. 

Orville alizaliwa mnamo Agosti 19, 1871 katika jimbo la Ohio huko Marekani na alikuwa mdogo kwa miaka minne kuliko kaka yake, Wilbur. Orville na Wilbur walikuwa watoto wa padri ambaye hakuweza kumudu gharama za masomo yao kutokana na umaskini. Kwa hivyo, ndugu hawa wawili, ambao walivutiwa na kazi za ufundi na utengenezaji wa injini na mashine, walianzisha warsha ya kutengeneza baiskeli. Ndugu hawa wawili, ambao walikuwa na hamu kubwa ya kuruka angani, hatimaye walitimiza ndoto yao ya muda mrefu mnamo Desemba 17, 1903, na wakavumbua ndege ya kwanza yenye injini ulimwenguni ambayo iliruka angani kwa sekunde 59.

Orville na Wilbur Wright