Jul 07, 2026 03:34 UTC
  • Jumanne, 7 Julai, 2026

Leo ni Jumanne tarehe 22 Mfunguo Nne Muharram 1448 Hijria sawa na 07 Julai mwaka 2026.

Katika siku kama hii ya leo miaka 988 iliyopita, tarehe 22 Muharram mwaka 460 Hijria aliaga dunia Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi, aliyepewa laqabu ya Sheikh Tusi na Sheikhul Twaifa, msomi wa Hadithi na mmoja wa wanazuoni wakubwa wa fiqhi katika ulimwengu wa Kiislamu.

Alizaliwa mwaka 385 Hijria huko Tus, mji ulioko kaskazini mashariki mwa Iran, na baada ya kumaliza elimu yake ya msingi, alielekea Iraq kwa alimu ya juu. Alipata elimu kwa wasomi wakubwa wa Kiislamu kama Sheikh Mufid na Sayyid Murtaza Alamul-Huda, na baada ya muda, alipata kalianza kufundisha. Miaka kadhaa baadaye, Sheikh Tusi aliweka misingi ya kwanza ya hauza na chuo kikuu cha kidini katika mji wa Najaf, nchini Iraq. Kituo hicho cha kidini kina umri wa miaka elfu moja na ni mojawapo ya vituo vya sayansi na maarifa ya Kiislamu.

Sheikh Tusi ameandika vitabu vingi muhimu katika nyanja za tafsiri ya Qur'ani, sheria, kanuni za sheria, na Hadithi. Miongoni mwa vitabu vyake ni tafsiri ya Qur'ani ya Al Tibyan, yenye juzuu kumi, al Tahdhib na al Istibsar. ****

Miaka 219 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, ulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Tilsit katika mji wenye jina hilo huko Russia kati ya Alexander wa Kwanza, mfalme wa Urusi na Napoleon Bonaparte wa Ufaransa.

Kwa mujibu wa mkataba huo Urusi na Ufaransa zilikubaliana kuwa, ikiwa nchi yoyote ingeishambulia nchi moja wapo kati ya hizo, zingesaidiana kumpiga adui. Mkataba huo wa urafiki, uliendelea hadi mwaka 1810.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, tarehe 16 Tir 1301 Hijiria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Zainul Abidin Marandi.

Msomi huyo mkubwa alisoma elimu za awali katika mji aliozaliwa wa Marand, huko katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki nchini Iran.

Baada ya hapo alielekea mjini Najaf, Iraq na kupata kusoma kwa maulama wakubwa kama vile Ayatullah Sayyid Mohammed Hassan Husayni Nouri Shirazi na Habib Allah Rashti. Baada ya muda fulani Ayatullah Marandi alikuwa marjaa taqlidi katika maeneo ya Azerbaijan na hatimaye akafariki dunia siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 72 na kuzikwa katika makaburi ya Wadi-al Salaam mjini Najaf.  ***  

Katika siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, visiwa vya Solomon vilivyoko kaskazini mashariki mwa Australia katika bahari ya Pacific vilipata uhuru.

Visiwa hivyo viligunduliwa na watu kutoka Ulaya mwaka 1567. Mwaka 1885 Ujerumani ilidai umiliki wa visiwa vya kaskazini mwa Solomon na ndiyo maana ikachukua hatua ya kuvishambulia na kisha kuvikalia kwa mabavu.

Muongo mmoja baadaye, Uingereza ilivishambulia visiwa hivyo na kuvidhibiti. Harakati ya kupigania uhuru ilianzishwa katika visiwa hivyo baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kuzaa matunda katika tarehe kama ya leo ambapo visiwa hivyo vilipata uhuru.   ***

Tarehe 7 Julai mwaka 2005 kulitokea mlipuko katika basi na milipuko mingine katika vituo vitatu vya treni ya chini ya ardhi katikati mwa mji mkuu wa Uingereza, London na kusababisha vifo vya watu 50 na wengine wapatao 700 kujeruhiwa.

Mashambulio hayo yalifanywa sambamba na kikao cha Viongozi wa Nchi Tajiri Kiviwanda Duniani G8 huko nchini Scotland kaskazini kwa Uingereza. Mashambulio hayo ya mabomu yalitekelezwa ili kupinga ushirikiano wa London na Washington katika kuikalia kwa mabavu Afghanistran na Iraq na kuuawa kiholela wananchi wa nchi hizo.

Serikali ya Uingereza ilidai kwamba, Waislamu walihusika na tukio hilo, na kwa muktadha huo mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Uingereza yaliyoanza baada ya mashambulio ya Septemba 11, 2001 yakashadidi zaidi.   ***