Jumatano, tarehe 31 Januari, 2024
Leo Jumatano tarehe 19 Rajab mwaka 1445 Hijria sawa na 31 Januari 2024.
Siku kama ya leo miaka 1436 vilitokea vita vya Tabuk baina ya Waislamu na jeshi la Roma. Vita vya Tabuk ni miongoni mwa vita vya mwisho vya Mtume Muhammad (saw).
Sababu ya kutokea vita hivyo ni kwamba, msafara wa kibiashara wa Sham ulimtaarifu Mtume (saw) kwamba mfalme wa Roma ametayarisha jeshi na kulituma Madina. Kwa msingi huo Mtume Muhammad (saw) aliwaamuru Waislamu kujitayarisha kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la mfalme wa Roma.
Waislamu wengi walijitayarisha kwa ajili ya vita hivyo licha ya masafa marefu, msimu wa joto kali, mashaka ya safari hiyo ngumu na kuwadia msimu wa mavuno. Hatimaye jeshi na wapiganaji elfu 30 la Waislamu liliwasili eneo la vita lakini halikukuta jeshi la mfalme wa Roma eneo hilo.
Japokuwa hakukutokea mapigano wakati huo, lakini tukio hilo lilidhihirisha nguvu ya Waislamu, utayarifu wao wa kukabiliana na majeshi vamizi na moyo wao wa kujitolea kwa ajili ya Allah.
Vita hivyo vya Tabuk pia vinajulikana kwa jina la "al Fadhiha" kwa maana ya mfedheheshaji kutokana na kwamba, vililifedhehesha kundi la wanafiki waliokataa kujiunga na msafara huo kwa ajili ya kukabiliana na jeshi la Roma. *

Miaka 971 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 19 Rajab mwaka 474 Hijria Qamaria Abul Walid Sulaiman bin Khalaf Maliki, faqihi maarufu wa karne ya Tano Hijria Qamaria aliaga dunia huko Andalusia ambayo leo inajulikana kama Uhispania.
Alikuwa hafidh na mfasiri wa Qur'ani Tukufu mbali na kubobea katika fasihi na mashairi. Abul Walid awali alifunza Fiqhi na taaluma ya Hadithi za Mtume SAW huko Andalusia na kisha akaendelea kufundisha huko Makka na Baghdad.
Baadhi ya vitabu mwanazuoni huyo ni, "Tafsirul Qur'an", "An-Nasikh Walmansukh" na Al-Isharah."

Siku kama ya leo miaka 425 iliyopita, ilianzishwa kampuni ya kwanza ya Uingereza ya India Mashariki nchini India kwa amri ya Malkia Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza.
Kampuni hiyo iliimarisha ukoloni wa Uingereza katika maeneo yenye utajiri huko kusini mwa Asia na baada ya hapo shughuli za ukoloni zikaimarika zaidi katika mataifa ya kusini mwa Asia kupitia kampuni hiyo. Baada ya kuasisiwa kampuni hiyo, nchi nyingine kama vile Uholanzi, Ureno na Ufaransa zilielekeza nguvu zao katika bara Hindi kwa lengo la kuhudumia ukoloni wao.
Baada ya karne 3 za kuanzishwa shirika hilo, ushawishi na kuimarika utawala wa Uingereza nchini India vilisababisha nchi hiyo kutangazwa kuwa sehemu ya Uingereza na Malkia Viktoria akavikwa taji la kuwa mtawala wa India na Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 174 iliyopita, ilianzishwa harakati kubwa ya uasi ya wananchi wa China iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Taiping.
Harakati hiyo ilianzishwa kutokana na hali mbaya na umasikini uliokuwa ukiwasumbua wananchi wa nchi hiyo na hasa matabaka ya watu wa vijijini, iliyosababishwa na ukoloni wa kigeni na utawala wa familia isiyofaa ya Manchu.
Lengo kuu la harakati hiyo iliyoendelea kwa muda wa miaka 14 lilikuwa ni kuhakikisha kunakuwepo usawa katika kugawana ardhi kati ya wanawake na wanaume.
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita gwaride la mwisho na kimaonyesho la vikosi vya majeshi ya utawala wa Shah lililokuwa na lengo la kuwatia hofu na woga wananchi Waislamu wa Iran, lilifanyika katika mitaa mbalimbali ya Tehran.
Katika gwaride hilo, wanajeshi wengi walionesha mshikamano wao na kuungana na wananchi Waislamu wa Iran na kuamua kuanza mapambano dhidi ya utawala wa kibeberu wa Shah.
