Jan 31, 2024 23:32 UTC
  • Alkhamisi, tarehe Mosi Februari, 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Rajab 1445 Hijria inayosadifiana na tarehe Mosi Februari 2024.

Miaka 1432 iliyopita katika siku kama hii ya leo, vilitokea vita vya Yarmuk kati ya jeshi la Kiislamu na jeshi la utawala wa kifalme wa Roma ya Mashariki katika bonde lililojulikana kwa jina hilo huko Palestina. Ushindi wa Waislamu huko Sham, yaani Syria ya sasa ulimpelekea mfalme wa Roma kuandaa jeshi kubwa kwa ajili ya kupigana na Waislamu. Lakini, Waislamu waliweza kutoa pigo kwa wanajeshi wa mfalme wa Roma licha ya kuwa na idadi ndogo ya wapiganaji na suhula chache za kivita. Kufuatia ushindi huo Waislamu walisonga mbele na kufika eneo la Mashariki la Ufalme wa Roma na mwaka mmoja baada ya hapo Waislamu wakafanikiwa kuchukua udhibiti wa mji wa Baitul Muqaddas pasina umwagaji damu. 

Katika siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, kulitokea vita vikali na vya umwagaji damu mkubwa maarufu kwa jina la Routier katika eneo lenye jina kama hilo karibu na Mto Ob kati ya jeshi lililokuwa na askari laki moja na 60 elfu la vikosi vya waitifaki wa nchi za Prussia, Austria na Sweden na jeshi lililokuwa na askari elfu 42 la Ufaransa chini ya uongozi wa Napoleon. Katika vita hivyo jeshi la Ufaransa lilishindwa vibaya na waitifaki kutokana na kutokuwa na moyo wa kupigana na uchache wa wapiganaji wake.   

Napoleon

Tarehe Mosi Februari miaka 66 iliyopita iliundwa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu ya Syria na Misri.

Baada ya kumalizika vita vya Suez na kurudi nyuma askari wa Uingereza, Ufaransa na utawala ghasibu wa Israel kutoka katika ardhi ya Misri, Gamal Abdul Nasser alitambuliwa kuwa kiongozi dhidi ya ukoloni wa Magharibi na dhidi ya Uzayuni katika ulimwengu wa Kiarabu na kupata umashuhuri mkubwa.

Hatua ya kwanza ya kuanzisha muungano wa nchi za Kiarabu dhidi ya utawala haramu wa Israel na waungaji mkono wake wa Magharibi ilichukuliwa tarehe Mosi Februari 1958 baada ya Syria kutia saini makubaliano ya kuungana na Misri na muungano huo ulianza rasmi baada ya kura ya maamuzi ya tarehe 22 Februari 1958 katika nchi hizo mbili.

Gamal Abdul Nasser akisaini mkataba wa kuanzisha muungano wa nchi za Kiarabu

Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita Imam Khomein (MA) Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, alirejea nchini na kupokelewa kwa shangwe kubwa na wananchi baada ya kuishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 15.

Mapokezi hayo makubwa ya wananchi wa Iran kwa Imam Khomeini hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika historia ya sasa ya dunia.

Baada ya kutoa hotuba fupi katika uwanja wa ndege wa Mehrabad, Imam Khomein alielekea moja kwa moja kwenye makaburi ya mashahidi waliouawa katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa heshima kwa mashahidi hao ambako pia alitoa hotuba katika umati mkubwa wa wananchi. Kwa mara nyingine Imam aliitaja serikali ya Shapour Bakhtiar kuwa kibaraka wa Shah sanjari na kutangaza kuunda serikali mpya kwa msaada wa wananchi.

Siku kumi baada ya kurejea nchini Imam, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi kamili na kipindi hicho cha siku kumi za baina ya kurejea Imam nchini hadi kupata ushindi kamili Mapinduzi ya Kiislamu, kinajulikana hapa nchini kama "Alfajiri Kumi".

Imam Khomeini akiwasili Tehran

Na katika siku kama ya leo miaka 11 iliyoita, Dakta Hassan Habibi mwanasiasa na mwanasheria wa Kiirani alifariki dunia.

Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1936. Hassan Habibi alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu (PhD) katika taaluma ya sosholojia na sheria katika Chuo Kikuu cha Sorbonne mjini Paris Ufaransa.

Hassan Habibi aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali kama Waziri wa Miongozo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Juu. Aidha alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran kuanzia mwaka 1989 hadi 2001 katika kipindi cha Urais wa Akbar Hashemi Rafsanjani na Sayyid Muhammad Khatami.

Dakta Hassan Habibi