Jumatatu, Februari 5, 2024
Leo ni Jumatatu tarehe 24 Rajab 1445 Hijria sawa na tarehe 5 Februari 2024.
Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita, ngome ya Khaibar ambayo ilikuwa moja ya ngome madhubuti na imara zaidi za Mayahudi ilitekwa na kudhibitiwa na Imam Ali (as), mkwewe Mtume Mtukufu (saw).
Mayahudi ambao hawakuacha kueneza uadui wao wa jadi dhidi ya Uislamu walikuwa wakiendeshea njama zao huko Khaibar kaskazini mwa mji mtakatifu wa Madina, ambako walikuwa wamejenga ngome saba muhimu, ambazo waliamini kuwa hazingepenyeka wala kudhibitiwa na adui.
Katika mwaka wa saba Hijiria Mtume (saw) alibashiri kutekwa kwa mji wa Khaibar. Muda si mrefu na baada ya kuvunja mzingiro uliokuwa umewekwa na maadui, jeshi la Kiislamu lilifanikiwa kudhibiti ngome kadhaa kati ya hizo saba isipokuwa mbili.
Hatimaye Mtume aliwahutubu makamanda wa jeshi hilo kwa kusema: 'Kesho nitampa bendera mtu ambaye anampenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake, naye Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanampenda pia, na Mwenyezi Mungu ataiteka ngome hii kupitia mikono yake. Siku iliyofuata, Mtume alimpa Imam Ali (as) uongozi wa jeshi ambapo alipigana vita vya kishujaa na hivyo kuweza kudhibiti ngome ya mwisho ya Mayahudi huko Khaibar.
Katika siku kama ya leo miaka 1106 iliyopita, Abu Nasr Muhammad Farabi, Mwanafalsafa, mwanahesabati na msomi mashuhuri wa Iran aliaga dunia.
Alizaliwa mwaka 259 Hijiria katika mji wa Farab ilioko kusini mwa nchi ya Kazakhstan ya leo. Baada ya kupata masomo ya msingi katika mji huo, Farabi aliamua kwenda mjini Baghdad huko Iraq ili kuendeleza masomo yake na hasa ya mantiki na falsafa. Werevu mkubwa aliokuwanao ulimuwezesha kusoma masomo mengi ya zama zake lakini alizingatia zaidi somo la falsafa.
Mwanafalsafa huyo mashuhuri aliyefahamika zaidi kwa majina ya Muallim ath-Thani, Ustadh wa Falsafa na Malik al-Hukamaa alifanya juhudi kubwa za kuunganisha fikra za wanafalsafa tofauti na hasa za Aristotle na Platon, akiamini kulikuwa na falsafa moja tu.
Miaka 233 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Allamah Sayyid Muhammad Mahdi Bahrul-Ulum, mtaalamu wa elimu ya irfan na msomi mkubwa wa Kiislamu.
Alizaliwa mwaka 1155 Hijiria katika mji mtukufu wa Karbala, Iraq na kusoma elimu za dini ya Kiislamu katika mji huo kwa baba yake mzazi ambaye alikuwa mmoja wa maulama wakubwa wa zama hizo na kwa wasomi wengine. Akiwa kijana, Allamah Bahrul-Ulum alifanikiwa kukwea daraja za juu za elimu na kufikia ijtihadi, na baada ya hapo akaelekea Najaf. Msomi huyo alijishughulisha na kazi mbalimbali za kijamii na alipendwa sana na watu. Sayyid Bahrul-Ulum aliiishi miaka saba mjini Mash’had, Iran na miaka miwili huko Hijaz, Saudi Arabiia ambapo pia aliendelea kujishughulisha na kazi za kielimu kiasi cha kumfanya imam wa Msikiti wa Makkah wakati huo, kujiunga na madh’habu ya Shia.
Vitabu vya ‘Al-Maswaabih’ ‘Mishkaatul-Hidaayah’ ‘Fawaaidulr-Rijaaliyah’ na diwani ya mashairi ni miongoni mwa athari za msomi huyo.
Katika siku kama ya leo miaka 143 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria, mwanafalsafa na mtaalamu mashuhuri wa masuala ya mashariki wa Scotland, Thomas Carlyle.
Mwanafalsafa huyo alizaliwa mwaka 1795 katika familia ya watu wa kijijini na mbali na lugha ya Kijerumani, alijifunza pia lugha ya Kiarabu na baadaye alianza kufunza lugha hiyo katika Chuo Kikuu cha Cambridge,London. Katika safari zake nyingi katika nchi za Kiislamu, mwanahistoria huyo alijifunza utamaduni na ustaarabu wa Kiislamu na kuathirika mno na dini hiyo.
Thomas Carlyle anasema kuhusu Qur'ani kwamba: "Qur'ani ni sauti isiyokuwa na wasita kutoka kwenye roho ya ulimwengu, na wanadamu wanapaswa kuisikiliza, la sivyo hawapaswi kusikiliza maneno mengineyo."
Mwanafalsafa huyo wa Scotland anasema kuhusu Mtume Muhammad (SAW) kwamba: Mwenyezi Mungu amemfunza hikima na elimu shakhsia huyu adhimu. Alijiepusha na kupenda jaha na ni miongoni mwa watu waliotakaswa na kupendwa mno na Mola Muweza.

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia na kufuatia amri ya Imam Khomeini MA ya kutangaza kuundwa serikali ya muda ya Mapinduzi nchini Iran, mamilioni ya wananchi Waislamu na Wanamapinduzi wa Iran waliandamana katika miji mbalimbali nchini ili kuuunga mkono na kuidhinisha uamuzi huo wa Imamu Khomeini (M.A).
Katika siku hiyo wananchi Waislamu wa Iran walimiminika kwenye mitaa mbalimbali na kwa sauti moja wakitaka kuondoka madarakani serikali kibaraka ya Bakhtiyar. Siku hiyo hiyo pia Jenerali Huyser, Mjumbe Maalumu wa Marekani ambaye alitumwa Tehran ili kusaidia kuubakisha madarakani utawala wa Pahlavi na kutangaza uungaji mkono wa Marekani kwa makamanda wa jeshi la Shah na kuandaa uwanja wa kujiri mapinduzi dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu hatimaye alirejea nchini kwake mwezi mmoja baada ya kufeli jitihada zake hizo katika uwanja huo.
Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA lilikiri kushindwa kutabiri masuala ya Mapinduzi ya Kiislamu. Maafisa wa CIA walikiri kuwa shirika hhilo limeshindwa kutabiri matukio ya Iran. Walisema, kitu ambacho hatukukitabiri kabisa ni mtu mmoja mzee wa miaka 78 ambaye alibaidishwa nje ya nchi kwa muda wa miaka 14, kuweza kuwaunganisha kiasi chote hiki wananchi wa Iran.

Miaka 26 iliyopita katika siku hii, yaani tarehe 16 Bahman 1376 Hijiria Shamsia, alifariki dunia mtumishi wa Mwenyezi Mungu, Hujjatul Islam "Jalil Honrovar Khoei."
Jalil Honravar Khoei alizaliwa mwaka 1305 Hijria Shamsia yaani mwaka 1345 Hijria Qamaria katika mji wa Khoei wa mkoa wa Azarbaijan Magharibi nchini Iran. Alianza mapema kusoma masomo ya dini. Katika miaka kumi na minne ya umri wake, alijifunza fasihi na usul na kutabahari katika fani hizo.
Kuanzia mwaka 1337 Hijria Shamsia, alichukua jukumu la kusimamia chuo muhimu cha kidini cha mji huo kwa muda wa miaka 20. Katika kipindi hiki na hadi mwisho wa maisha yake, alifundisha sayansi ya dini na kufunza makumi ya masheikh na walimu mahiri waliondeleza juhudi zake baada yake. Alikuwa akitumia siku nzima kuanzia asubuhi hadi jioni kufundisha mafundisho ya Ahlul-Bayt AS.
Alikuwa akitumia muda wake mwingine kutatua masuala ya watu, kuhudumia Waislamu, kutatua hitilafu zao, kujibu maswali yao ya kidini, kusimamia misikiti na shule, na alikuwa akisoma vitabu mbalimbali katika wakati wake wa faragha. Alikuwa na umahiri mkubwa wa Tafsir ya Qur’ani, tarikhi, hadithi na fasihi ya Kiarabu na Kiajemi na ameirithisha vizazi vya baada yake turathi yenye thamani kubwa.
Miongoni mwa athari za thamani za Hojjatul Islam Jalil Honravar Khoei, ni kitabu cha "Ufafanuzi wa Majina" ambacho kimehifadhi maelezo ya majina ya Mitume na Manabii, Maimamu, wanazuoni wa Kishia na Kisunni, pamoja na wasifu wa mmoja wa wanazuoni wakubwa.