Jumatano, tarehe 7 Februari, 2024
Leo ni Jumatano tarehe 26 Rajab 1445 Hijria sawa na tarehe 7 Februari 2024.
Siku kama ya leo miaka 1448 iliyopita Abu Twalib ami ya Mtume Muhammad (SAW) na baba wa Imam Ali (A.S) alifariki dunia wakati Waislamu walipokuwa chini ya mzingiro wa washirikina wa Makka. Abu Twalib alikuwa pamoja na Waislamu wengine huko katika Shiibi Abi Twalib akimlinda na kumhami mtukufu huyo mbele ya adha za washirikina. Mtume Muhammad (SAW) alikuwa chini ya uangalizi wa Abu Twalib tangu alipokuwa na umri wa miaka minane, baada ya kuaga dunia babu yake Abdul Muttalib. Abu Twalib alisilimu baada ya kubaathiwa Mtume na alikuwa muungaji mkono na mtetezi mkubwa wa Mtume Mtukufu dhidi ya washirikina wa Kikuraishi.

Siku kama ya leo miaka 546 iliyopita, alizaliwa Thomas More, mwanafalsafa na msomi mashuhuri wa nchini Uingereza.
Mwanzoni More alisomea elimu ya sheria na baada ya kujiunga bungeni akapewa mazingatio na malkia wa wakati huo na kutunukiwa hadhi ya Ulodi. Hata hivyo Thomas More alitofautiana kinadharia na mfalme wa wakati huo wa Uingereza na hivyo akatiwa jela na kuhukumiwa kifo.
Hatimaye More akanyongwa mnamo tarehe sita Julai mwaka 1535 Miladia akiwa na umri wa miaka 57.
Siku kama ya leo miaka 162 iliyopita, alizaliwa mjini Newcastle Edward Granville Browne, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati, mtafiti na fasihi wa nchini Uingereza.
Awali Browne alisomea fani ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Cambridge na kuhitimu masomo yake chuoni hapo. Hata hivyo kutokana na kupendelea kwake kusoma tamaduni za Mashariki mwa dunia alifanya safiri nchini Iran akiwa na umri wa miaka 25. Aidha mtafiti huyo aliitaja lugha ya Kifarsi kuwa njia bora ya kunakili fikra na tamaduni za Wairani kuelekea maeneo mengine ya dunia.
Ni kwa msingi huo ndio maana akaandika vitabu kadhaa kuhusiana na historia na utamaduni wa Wairani. Mwishoni Edward Granville Browne alijikita katika kufundisha lugha ya Kifarsi na Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Cambridge, na kufariki dunia mwaka 1926 akiwa na umri wa miaka 54.
Miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi dogo ya Grenada iliyoko katika Amerika ya Kaskazini ilijipatia uhuru.
Kisiwa hicho kiligunduliwa mwaka 1498 na Christopher Columbus mvumbuzi wa Kihispania na ikaunganishwa na nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1674 Ufaransa ikaidhibiti Grenada.
Baada ya takribani karne moja yaani mwaka 1783, Waingereza waliifanya Grenada kuwa koloni lao na hali hiyo ikadumu kwa takribani karne mbili. Hatimaye mwaka 1974 na katika siku kama ya leo, Grenada ikajikomboa na kujipatia uhuru.
Tarehe 18 Bahman miaka 40 iliyopita aliuawa Jenerali Gholam-Ali Oveissi aliyehusika na mauaji ya wananchi wakati wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.
Jenerali Oveissi ambaye alikuwa Kamanda Mkuu wa jeshi la utawala wa kifalme wa Shah alihusishwa na mauaji ya wananchi wa Iran mwaka 1962 na 1978 katika vuguvugu la wananchi wa Iran la kutaka kuanzishwa Jamhuri ya Kiislamu na kuuondoa madarakani utawala wa dhalimu wa kifalme.
Oveissi alikimbia nchi mwezi mmoja kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na hata kabla ya Shah Pahlavi kutoroka nchi. Mwezi mmoja baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jenerali Oveissi alifanya jitihada za kuwakusanya tena waungaji mkono wa utawala wa kifalme nchini Iran na kutoa dharba kwa Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo njama hizo zilishindwa na hatimaye kibaraka huyo wa Shah aliuawa katika siku kama hii leo akiwa Paris nchini Ufaransa.