Jul 12, 2024 03:00 UTC
  • Ijumaa, Julai 12, 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 06 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria sawa na Julai 12 mwaka 2024.

Tarehe sita Muharram mwaka 61 Hijria yaani miaka 1385 iliyopita katika siku kama hii ya leo mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) aliyekuwa Karbala alimwandikia barua fupi lakini muhimu sana ndugu yake, Muhammad bin Hanafiyya na wafuasi wake kadhaa waliokuwa Madina. Barua hiyo ilisema: "Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu. Hakika anayejiunga nami atapata daraja ya kuuawa shahidi, na ambaye hatajiunga nami hatapata ushindi." 

Barua hii ilikuwa na ujumbe kadhaa, miongoni mwa ujumbe hizo ni kwamba, Imam Hussein alikuwa akijua kuwa, atauawa shahidi yeye na masahaba wake katika mapambano yake na mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya.

Pili ni kwamba aliweka wazi hatima ya wale wote watakaofuatana naye katika mapambano ya Karbala na kwamba wote watauawa, na hivyo mtu yeyote mwenye malengo tofauti bora arejee Madina.

Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita, Habib Bin Madhahir, mmoja wa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na mfuasi wa kweli wa Imam Hussein (as), aliwalingania watu wa kabila la Bani Asad kwa ajili ya kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah.

Katika siku hiyo, sahaba huyo wa Mtume aliomba idhini kwa Imam Hussein (as) kwa kusema: “Ewe mjukuu wa Mtume, katika maeneo haya jirani wanaishi watu wa kabila la Bani Asad, ikiwa utaniruhusu nitaenda kwao nikawalinganie, huenda Mwenyezi Mungu akakuokoa kutokana na shari ya watu hawa makatili kupitia uwepo wa watu wa kabila la Bani Asad.” 

Imam Hussein alimruhusu Habib Bin Madhahir ambaye alitoka majira ya usiku kwenda kwa watu wa kabila hilo akiwaomba wamsaidie mjukuu wa Mtume. Akiwa katika linganio hilo, sahaba huyo wa Mtume alisema: “Kwa kuwa nyinyi ni watu wa ukoo na kabila langu, ninakulinganieni kufuata njia hii, leo ninakuombeni msikie usia wangu na mfanye haraka kwenda kumsaidia Imam Hussein (as) ili mpate utukufu wa dunia na Akhera.” 

Kutokana na wito huo, watu wachache kutoka kabila hilo wanaokadiriwa kufikia 90 walisimama na kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Mtume. Hata hivyo baadaye walitoroka na kurejea makwao baada ya kufahamu kwamba, jeshi la Yazid likiongozwa na Omar Bin Sa’ad lilijua nia yao, hivyo walihofia kuuawa na jeshi hilo. Baada ya Imam Hussein kusikia habari hiyo, alisema: “Laa haula walaa quwwata illa Billah.” 

Siku kama ya leo miaka 1313 iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia ya mapambano ya Waislamu, akiwa na jeshi kubwa la Kiislamu Twariq bin Ziyad aliweza kuingia Uhispania.

Ushindi huo ulikuwa mwanzo wa maendeleo ya Waislamu barani Ulaya ambapo uliendelea hadi Ufaransa ya sasa. Twariq bin Ziyad aliwasili Uhispania baada ya kuvuka lango bahari kati ya Morocco na Uhispania linalojulikana kwa jina lake mwenyewe yaani "Jabal Tariq." Mlango bahari huo unatumika kama njia ya mawasiliano kati ya Bahari za Atlantic na Mediterranean.

Waislamu walitawala kwa karne nane huko Uhispania na kueneza mafunzo na utamaduni wa Kiislamu barani Ulaya baada ya kutekwa Andalusia, moja ya maeneo ya hispania ya leo.   

Twariq bin Ziyad

Siku kama ya leo miaka 1040 iliyopita inayosadifiana na tarehe 6 Muharram mwaka 406 Hijria, alifariki dunia Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi, msomi mashuhuri, mwanafikra na mshairi wa Kiislamu.

Aalim huyo pia alijulikana kwa jina la Sayyid Radhi. Alipata elimu za wakati huo katika kipindi cha ujana wake akiwa pamoja na ndugu yake, Sayyid Murtadha, ambaye pia alikuwa msomi mtajika. Sayyid Radhi aliinukia kuwa msomi mkubwa katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani Tukufu na elimu nyingine za Kiislamu. Msomi huyo alikuwa wa kwanza kuasisi chuo kikuu kwa mtindo wa kisasa na ameandika zaidi ya vitabu 20 katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani, historia na fasihi ya Kiarabu.

Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Nahjul Balagha ambacho kinakusanya semi, hotuba, amri, barua na mawaidha ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as).   

Kaburi la Sayyid Radhi

Miaka 791 iliyopita katika siku kama ya leo, bandari ya kihistoria ya Alexandria huko Misri ilizingirwa na meli za kivita za Jeshi la Msalaba.

Wakati huo Salahuddin Ayyubi alikuwa gavana wa Alexandria na hakuweko katika mji huo wakati maadui walipofanya mashambulizi. Hata hivyo wapiganaji wa Kiislamu walikabiliana kwa nguvu na Jeshi la Msalaba hadi gavana Salahuddin alipowasili.

Wanajeshi wa Uholanzi waliokuwa katika safu ya mbele walipigwa vibaya na kulazimika kurudi nyuma.   

Alexandria

Siku kama ya leo miaka 207 iliyopita, alizaliwa Henry David Thoreau, msomi na mwanaharakati wa Kimarekani.

David alikuwa akiheshimu mazingira asilia kama viumbe vya Mwenyezi Mungu na alisifika kwa kuwa na akhlaqi na maadili mema. Henry David alikuwa akisisitiza kuwa, haifai kuangamiza maisha ya wanadamu kwa tamaa ya kufikia mali na fedha nyingi. Aidha mwanaharakati huyo, aliamini kuwa kama vile ambavyo serikali inavyomuadhibu mtu mkosefu, kadhalika inapotokea serikali hiyo ikashindwa kutekeleza wadhifa wake wa kiuongozi, basi wananchi nao wanatakiwa kuipa adabu serikali hiyo sanjari na kuiondoa madarakani.

Miongoni mwa athari muhimu za Henry David Thoreau ni pamoja na kitabu cha 'Uasi wa Kiraia' na alifariki dunia mwaka 1862. 

Henry David Thoreau

Tarehe 12 Julai miaka 78 iliyopita, Hoteli ya Mfalme Daud huko Baitul Muqaddas iliripuliwa kwa bomu na kundi la Kizayuni la Irgun.

Hoteli hiyo ilikuwa ikitumiwa sana na raia wa Palestina. Bomu lililokuwa limetegwa ndani ya hoteli hiyo liliripuka na kuuawa watu zaidi ya 200. Kuweko Wayahudi watano miongoni mwa waliouawa katika mlipuko huo kunabainisha wazi namna Wazayuni wasivyothamini hata maisha ya Wayahudi ili kufikia malengo yao ya kujitanua na kuzusha hofu miongoni mwa Wapalestina.   

Hoteli ya Mfalme Daud

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilifanya mashambulizi ya anga na baharini huko Lebanon.

Utawala wa Kizayuni ulifanya mashambulizi hayo kwa kisingizio cha kukamatwa mateka wanajeshi wake wawili na wapiganaji wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon kupitia oparesheni yake ya kujilinda.

Tel Aviv ilifanya mashambulizi hayo ya kijeshi huko Lebanon ikiungwa mkono na Washington lengo lake kuu likiwa ni kuvunja uwezo wa kijeshi wa Hizbullah na kuipokonya silaha harakati hiyo inayohesabiwa kuwa nguvu kuu ya mapambano huko Lebanon mbele ya jeshi ghasibu la utawala wa Kizayuni. 

 

Tags