Jumatano, tarehe 17 Julai, 2024
Leo ni Jumatano tarehe 11 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria, sawa na tarehe 17 Julai mwaka 2024.
Siku kama ya leo miaka 1385 iliyopita, yaani tarehe 11 Muharram mwaka 61 Hijiria, msafara wa mateka wa familia ya Bwana Mtume Muhammad (saw), baada ya tukio chungu la mauaji ya siku ya Ashura, ulianza safari ya kelekea Sham, yalikokuwa makao makuu ya utawala wa dhalimu wa Yazidi bin Muawiya.
Baada ya majeshi ya Yazidi yaliyokuwa yakiongozwa na Omar bin Sa’ad kumuua shahidi Imam Hussein (as) na masahaba wake, majeshi hayo ambayo hayakuwa na chembe ya ubinadamu moyoni, yalianza kupora vitu vya thamani vya msafara wa watu wa familia ya Mtume (saw). Askari hao sanjari na kuchoma moto mahema ya Imam Hussein (as) na watu wake, waliwanyang’anya pia wanawake mapambo yao na kila walichokuwa nacho.
Jioni ya siku kama ya leo msafara wa familia ya Imam Hussein uliokuwa ukiongozwa na Imam Sajjad (as) na Bibi Zainab (as), ulielekea Kufa na baadaye Sham.
Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita Profesa Roger Garaudy, mwanafalsafa na mwanafikra wa Ufaransa alizaliwa huko katika mji wa Marseille.
Garaudy alipata shahada ya udaktari katika taaluma tatu za masomo ya falsafa, fasihi na utamaduni. Roger Garaudy alifungwa jela katika kambi ya mateka wa kivita wa Ujerumani tangu mwaka 1940 hadi 1943 kutokana na mapambano yake dhidi ya ufashisti wa Adolph Hitler wakati Ufaransa ilipokaliwa kwa mabavu na Ujerumani.
Profesa Garaudy alikuwa mwanachama wa chama cha Kikomonisti cha Ufaransa kwa miaka 36 na pia mwanachama wa kamati kuu ya chama hicho kwa miaka 25. Hata hivyo mitazamo ya kikomunisti na kiliberali haikuweza kukata kiu ya kutafuta ukweli ya msomi huyo wa Ufaransa na hatimaye alikubali dini ya tukufu ya Uislamu baada ya kufanya utafiti mkubwa. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran mwaka 1979 ulikuwa na taathira kubwa katika mitazamo ya Profesa Roger Garaudy.
Katika siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, chama cha Baath cha Iraq kilichukua hatamu za uongozi kupitia mapinduzi yaliyoongozwa na Ahmad Hassan al-Bakr na kumpindua Rais Abdulrahman Aarif.
Baada ya kuchukua madaraka chama cha Baath, Saddam Hussein ambaye alikuwa kiongozi nambari mbili wa chama hicho alianza kuwauwa wapinzani wake nchini Iraq na vikosi vya usalama na vya jeshi la nchi hiyo pia vikaanzisha hujuma kali dhidi ya wapinzani wa Kikurdi, wazalendo, wanaharakati wa Kiislamu na hata Wakomonisti.
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Azimio hilo lilizitaka nchi mbili za Iran na Iraq kusitisha vita na kufanya suluhu. Jamhuri ya Kiislamu ilikubali azimio hilo kutokana na baadhi ya vipengele vyake hususan kile kinachohusiana na kuitambulisha Iraq kuwa ndiye mchokozi katika vita hivyo na kuitaka iilipe Iran fidia ya hasara za vita hivyo.
Hata hivyo utawala wa Saddam Hussein ambao pia ulikubali azimio hilo la Baraza la Usalama, uliendeleza mashambulizi dhidi ya ardhi ya Iran.