Jun 29, 2025 08:30 UTC
  • Jumapili, 29 Juni, 2025

Leo ni Jumapili 03 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hijria mwafaka na 29 Juni 2025.

Siku kama ya leo miaka 1440 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, inayosadifiana na tarehe 3 Muharram mwaka wa 7 Hijria, Mtume Muhammad SAW aliwatumia barua wafalme wa tawala mbalimbali duniani na kwa hatua hiyo akawa ameanza rasmi kuwalingania watu Uislamu kimataifa.

Baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani kati ya Mtume SAW na washirikina wa Makka huko Hudaibiya, Mtume Muhammad SAW alipata fursa ya kuwalingania dini ya Uislamu viongozi wa tawala kubwa duniani bila wasiwasi. Wanahistoria wanasema kuwa, Mtume aliandika barua 12 hadi 26 kwa watawala mbalimbali katika kipindi hicho wakiwamo watawala wa Roma, Iran, Uhabeshi, Bahrain, Yemen na maeneo mengine makubwa katika zama hizo ambapo kila mmoja kati ya watawala hao alionesha radimalia yake.

Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilionesha wazi kuwa dini ya Kiislamu inalingania haki kwa kutumia mantiki na hoja madhubuti.   

Miaka 1386 iliyopita yaani tarehe 3 Muharram mwaka 61 Hijria, jeshi la Umar bin Saad liliwasili katika ardhi ya Karbala.

Baada ya Hurr bin Yazid kumzingira Imam Hussein AS na maswahaba zake katika ardhi ya Karbala na kuwazuia wasisonge mbele, Ubaidullah bin Ziyad aliyekuwa kibaraka wa Yazid huko Kufa alikabidhi jukumu la ukamanda wa jeshi la Yazid kwa Umar bin Saad alikuwa na jeshi la wapiganaji elfu nne.

Umar bin Saad alikubali kuongoza jeshi la kumuua mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), watu wa familia yake na masahaba zake kwa sharti la kupewa utawala wa eneo kubwa la Rei, ndoto ambayo alikwenda nayo kaburini.

Siku kama ya leo miaka 618 iliyopita, alizaliwa Ibn Khallouf mtaalamu wa fasihi, mwandishi na malenga mkubwa wa Kiislamu.

Akiwa kijana mdogo alifanya safari mjini Makkah na baadaye Quds, Palestina huku akisafiri pia mjini Cairo, Misri baada ya kuwa ni kijana. Lengo la safari hizo ilikuwa ni kwa ajili ya kutafuta elimu kiasi kwamba, akiwa na umri wa miaka 26 alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika vyuo vikubwa vya nchini Misri.

Mbali na hayo ni kwamba Khallouf alikuwa akisoma pia mashairi ya kumsifu Mtume Muhammad (saw) na watu wa familia yake. Hadi leo turathi za msomi huyo zipo katika maktaba za Bairut, Lebanon na Damascus, Syria. 

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita vilianza Vita vya Pili vya Balkan kati ya Bulgaria na umoja wa nchi za Serbia, Ugiriki, Montenegro, Romania na utawala wa Othmania. 

Karibu mwaka mmoja kabla ya hapo katika Vita vya Kwanza vya Balkan, Bulgaria, Serbia, Ugiriki na Montenegro zilizokuwa sehemu ya utawala wa Othmania, zilianzisha uasi dhidi ya ufalme huo, na kutokana na kudhoofika utawala huo nchi hizo zilifanikiwa kupata uhuru. Kwa msingi huo karibu asilimia 80 ya nchi zilizokuwa chini ya himaya ya Othmania huko Ulaya zikatoka chini ya udhibiti wa dola hilo. 

Hata hivyo nchi zilizoshinda katika Vita vya Kwanza vya Balkan hazikuweza kufikia makubaliano ya kugawana ardhi zilizokombolewa sababu iliyopelekea kuanza Vita vya Pili vya Balkan. Vita vya Balkan viliandaa mazingira ya kuanza kwa Vita vya Kwanza vya Dunia.   

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita yaani tarehe 29 Juni mwaka 1976, muungano wa visiwa vya Ushelisheli ulipata uhuru na kila siku kama hii huadhimishwa katika visiwa hivyo kama siku ya taifa. 

Hadi kufikia katikati ya karne ya 18, wakati ambao Wareno walikuwa wakiikalia kwa mabavu ardhi hiyo, sehemu kubwa ya visiwa vya Ushelisheli ilikuwa bado haijagunduliwa na haikuwa na wakazi. Mwishoni mwa karne ya 18 wakati ulipopamba moto wa mapinduzi ya Ufaransa, wanajeshi wa Uingereza waliokuwa katika eneo la Afrika waliivamia Ushelisheli.

Mapambano ya kuikomboa nchi hiyo yalipamba moto mwaka 1960 na kuendelea, na miaka 16 iliyofuata visiwa vya Ushelisheli vikawa huru na kuasisi mfumo wa Jamhuri. Ushelisheli inaundwa na visiwa kadhaa vilivyoko katika bahari ya Hindi ikipakana na Madagascar.   

Tarehe 29 Juni miaka 33 iliyopita aliuawa Mohamed Boudiaf aliyekuwa Mkuu wa Baraza la Serikali ya Algeria. 

Mohamed Boudiaf alikuwa rais wa nne wa Algeria tangu nchi hiyo ilipopata uhuru. Alijiunga na harakati za siri za kupinga ukoloni wa Ufaransa akiwa bado kijana na kupanda ngazi katika harakati ya wananchi wa Algeria iliyokuwa ikiendesha harakati za siri dhidi ya wakoloni wa Kifaransa. Baada ya ushindi wa mapinduzi ya wananchi wa Algeria hapo mwaka 1962 Mohamed Boudiaf aliunda serikali ya kisoshalisti akishirikiana na Ahmed Ben Bella. Alikimbilia nje ya nchi kufuatia mapinduzi ya Houari Boumediene dhidi ya serikali Ben Bella na kurejea Algeria baada ya kujiuzulu Chadli Bendjedid na kuunda baraza la uongozi. 

Kama walivyokuwa viongozi wengi wa baada ya uhuru wa Algeria, Mohamed Boudiaf alikuwa mpinzani mkubwa wa fikra za Kiislamu na baada ya kushika madaraka alivunja harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo iliyokuwa imeshinda uchaguzi wa Bunge na kubatilisha matokeo ya uchaguzi huo. Hatua hiyo ilisababisha machafuko ya ndani nchini Algeria na tarehe 29 Juni 1992 alipigwa risasi na kuuawa na mmoja wa walinzi wake.

Mohamed Boudiaf