Aug 04, 2024 02:24 UTC
  • Jumapili, 04 Agosti, 2024

Leo ni Jumapili 29 Mfunguo Nne Muharram 1446 Hijria, mwafaka na tarehe 4 Agosti 2024

Siku kama ya leo miaka 543 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria wa Kiislamu, Muhammad Heravi, katika mji wa Herat nchini Afghanistan. Heravi alizaliwa katika familia mashuhuri kwenye mji wa Balkh huko kaskazini mwa Afghanistan ingawa aliishi kipindi kirefu katika mji wa Herat. Muhammad Haravi aliheshimiwa mno na waziri msomi wa utawala wa kizazi cha Gurkanian, Amir Alishah Navai, ambaye alikuwa akiwaenzi na kuwaheshimu mno wasomi na wanazuoni. Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwanahistoria huyo wa Kiislamu ni kile cha "Tarikh Raudhatu Safa" ambacho kinazungumzia historia ya dunia nzima tangu kuumbwa kwake hadi kipindi cha msomi huyo. ***

 

Miaka 232 iliyopita alizaliwa Percy Bysshe Shelley malenga wa Uingereza. Percy alianza kupenda taaluma ya fasihi tangu utotoni na kuonyesha kipawa kikubwa katika uwanja huo. Alikuwa mfuasi na muungaji mkono wa thamani za upendo, urafiki na uhuru na sababu hiyo ndiyo iliyomfanya avutiwe na Mapinduzi ya Ufaransa ambayo ndio kwanza yalikuwa yametokea. Percy Bysshe Shelley aliaga dunia mwaka 1822 akiwa na umri wa miaka 30 baada ya boti yake kuzama katika Bahari ya Mediterrania.   

Percy Bysshe Shelley

 

Miaka 219 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa William Rowan Hamilton mwanahisabati na mtaalamu wa elimu ya fizikia wa Ireland alizaliwa.  Alikuwa na kipaji cha hali ya juu kiasi kwamba akiwa na umri wa miaka 13 alikuwa amejifunza lugha 12 za dunia zikiwemo Kiarabu na Kifarsi. William Rowan Hamilton taratibu akaanza kuwa na mapenzi makubwa na elimu za fizikia na hisabati. Aidha alifanikiwa kuanzisha baadhi ya kanuni na mifumo muhimu katika elimu hizo. Akiwa na umri wa miaka 22 Hamilton alikuwa tayari ni mwalimu wa elimu ya nujumu. Msomi huyo aliaga dunia 1865. *** 

William Rowan Hamilton

 

Katika siku kama ya leo miaka 149 iliyopita, aliaga dunia Hans Christian Andersen mwandishi wa vitabu vya watoto wa nchini Denmark. Alizaliwa mwaka 1805 na tangu akiwa mdogo alikuwa na mapenzi makubwa na visa. Baada ya kuaga dunia baba yake, Hans Christian Andersen akiwa na umri wa miaka 11 aliacha shule na kuanza kufanya kazi. Baada ya kuingia katika maonyesho na michezo ya kuigiza ya kifalme, hali yake ya maisha iliboreka na hivyo akaamua kuendelea na masomo. Mwandishi huyo wa Kidenmark awali alianza kujihusisha na utungaji mashairi na kuandika visa na simulizi. Hata hivyo baadaye Andersen aliondokea kuwa na mapenzi makubwa na visa vya watoto na alionyesha kipaji kikubwa alichokuwa nacho katika uwanja huo.

Hans Christian Andersen

 

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, vikosi vilivyokuwa na mrengo wa utaifa nchini Uturuki vikiongozwa na Mustafa Kemal Ataturk vilianza kuwashambulia wanajeshi wa Ugiriki waliokuwa wameikalia kwa mabavu nchi hiyo. Baada ya kusambaratika utawala wa Othmania katika Vita vya Kwanza vya Dunia, ardhi asili ya utawala huo yaani Uturuki iliangukia mikononi mwa tawala waitifaki. 

Mustafa Kemal Ataturk akiwa na Reza Shah

 

 Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita Marekani ilishindwa katika vita vya baharini vilivyozishirikisha meli za kivita za Marekani na Vietnam ya Kaskazini katika Ghuba ya Tonkin inayopatikana kwenye Bahari ya China ya Kusini. Mikwaruzano hiyo ya kijeshi iliipa Marekani kisingizio cha kuingia vitani moja kwa moja na Vietnam ya Kaskazini. Wakati huo Washington ilikuwa ikiiunga mkono kwa pande zote Vietnam ya Kusini dhidi ya ile ya Kaskazini. Wanajeshi wa Marekani waliingia vitani moja kwa moja kupigana dhidi ya Vietnam ya Kaskazini. 

Vita vya Vietnam

 

Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Mordad 1367 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Allamah Sayyid A'ref Hussein Husseini, mwanachuo mashuhuri na mwanamapambano wa Pakistan katika mji wa Peshawar, kaskazini mwa nchi hiyo. Sayyid A'ref Husseini baada ya kupata elimu ya kidini nchini Pakistan, alifunga safari na kuelekea katika nchi za Iraq na Iran kwa shabaha ya kuongeza maarifa ya kidini. Wakati  wa kutokea  harakati za mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala wa Shah, Allamah A'ref Husseini alikuwa hapa nchini na kuwa bega kwa bega na wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah, jambo ambalo liliukasirisha utawala wa Shah na kuamua kumfukuza nchini. 

Allamah Sayyid A'ref Hussein Hussein

 

Tags