Hikma za Nahjul Balagha (63)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 63 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki. Ingawa hii ni sehemu ya 63 ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoendelea kuichambua ni ya 56.
الْغِنَى فِی الْغُرْبَةِ وَطَنٌ وَ الْفَقْرُ فِی الْوَطَنِ غُرْبَةٌ
Kuwa na utajiri ni kuwa mwenyeji hata nje ya mji wako na kuwa na umaskini ni kuwa mgeni hata ndani ya mji wako.
Katika hikma hii ya 56 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anagusia athari za mali na umasikini na kusema:
الْغِنَى فِی الْغُرْبَةِ وَطَنٌ وَ الْفَقْرُ فِی الْوَطَنِ غُرْبَةٌ
Yaani mtu anapokuwa tajiri huwa ni mwenyeji hata anapokwenda nje ya mji wake lakini mtu anapokuwa maskini huwa ni mgeni hata ndani ya mji wake.
Neno "watan" maana yake ni eneo ambalo mtu amezaliwa na kufumbua macho kwenye eneo au nchi hiyo na kuona ndugu na jamaa zake wakiwa wamemzunguka na ni eneo ambalo mtu huwa ana marafiki katika kila kona. Kwa lugha nyepesi ni mwenyeji wa eneo hilo. Katika upande wa pili, mtu huambiwa yuko ugenini anapokosa mambo yaliyofafanuliwa kuhusu watan ikiwa ni pamoja na kutokuwa na jamaa ya marafiki katika eneo hilo. Imam Ali AS katika hikma hii ya 56 anasema: Tajiri ana uwezo wa kupata marafiki popote aendapo kutokana na mali yake na watu wengi watavutika kwake kwa sababu ya utajiri wake, hivyo tajiri huwa hajihisi mpweke wala mtu aliyetengwa popote aendapo kwani dhati ya wanadamu ni kuvutiwa na mali na utajiri. Lakini maskini huwa haheshimiwi hata katika nchi yake na hiyo ndiyo kawaida ya wanadamu walio wengi hata watu maarufu na wenye ushawishi. Kwa bahati mbaya, baadhi ya wakati utaona mtu anakataliwa na hata familia yake na kutupwa na hata marafiki zake wa karibu kwa sababu ya umaskini na ufukara wake na mwishowe anakuwa kiumbe aliyesahaulika.
Tunapouzingatia uhakika huo tutaona hikma iliyojificha ndani ya maneno hayo yenye thamani kubwa ya Imam Ali AS, kwamba, kama unataka kupata heshima katika ulimwengu huu basi jipinde kwa kazi na juhudi kwa ajili ya kuupiga vita umaskini na pia tusijiweke katika mazingira ya kuwategemea watu wengine katika kila kitu bali wenyewe tujifanyie mambo yetu hadi pale inaposhindikana kabisa. Tab'an ni vyema kuongeza kusema hapa kwamba dunia ni mahali pa kupimwa viumbe, ni sehemu ya kutahiniwa wanadamu kuona wameweza vipi kutumia vipawa walivyopewa na Allah. Hivyo ni wajibu wa watu matajiri kutambua kwamba utajiri walio nao ni amana waliyokabidhiwa na Mwenyezi Mungu, wawape maskini haki zao ili asibakie maskini hata mmoja katika jamii ya Waislamu. Watambue kuwa furaha ya kweli hailetwi kwa kujilimbikizia mali nyingi. Lakini maskini nao wanapaswa kutambua kuwa wanaweza kufikia furaha ya kweli kwa kuwa na subira mbele ya matatizo na kufanya jitihada kubwa za kutafuta riziki za halali.
Ndio maana pia katika sehemu nyingine tunamuoma Imam Ali AS anaomba dua ya kuondolewa matatizo ya kimaisha na kiuchumi na Mola wake Mlezi. Anasema: Ewe Mola wangu, nihifadhie heshima yangu kwa kunifanya nikutegemee Wewe tu nisiwategemee viumbe na usinitie kwenye umaskini ikawa sababu ya kudhalilika utu wangu.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.