Jumamosi, 21 Septemba, 2024
Leo ni Jumamosi 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1446 Hijria mwafaka na 21 Septemba 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1499 iliyopita kwa mujibu wa nukuu na kauli za maulama wengi wa Kiislamu, alizaliwa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Makka. Baba yake, Abdullah alifariki dunia kabla ya kuzaliwa Mtume na mama yake, Amina binti Wahab, alifariki dunia mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka sita. Katika kipindi cha mwanzoni mwa ujana wake Muhammad alikuwa akijitenga na jamii ya kijahilia ya watu wa Makka na kwenda kwenye pango la Hiraa lililoko karibu na mji wa Makka na kuketi huko kwa masaa kadhaa akitafakari katika maumbile ya dunia na kufanya ibada. Malaika Jibrilu alimteremkia mtukufu huyo akiwa katika pango hilo na kumpa ujumbe wa Mola Muumba. Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) alikumbana na mashaka mengi katika jitihada zake za kufuta ibada ya masanamu na kueneza imani ya Tauhidi na kumwabudu Mungu Mmoja.
Katika siku kama ya leo miaka 1363 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa mjukuu wa Mtume saw, Imam Ja'far Swadiq (as) katika mji mtakatifu wa Madina. Kipindi cha maisha yake kilikuwa zama za kuchanua elimu na maarifa, tafsiri ya Qur'ani na kuenea elimu mbalimbali. Imam Swadiq (as) alitumia fursa hiyo ambayo ilisadifiana na kuanza kuporomoka utawala wa Bani Umayyah na kuchukua madaraka utawala wa Bani Abbas, kwa ajili ya kueneza maarifa asili ya Kiislamu na kulea kizazi cha wasomi na maulama katika nyanja mbalimbali. Kwa minasaba hii adhimu Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote duniani.
Siku kama ya leo miaka 192 iliyopita, inayosadifiana na 21 Septemba 1832, aliaga dunia Sir Walter Scott, mwandishi wa riwaya, mshairi na mwanahistoria mahiri wa Uskochi. Alizaliwa 15 Agosti mwaka 1771 na baada ya kuhitimu masomo yake katika taaluma ya sheria, alifanya kazi ya uwakili kwa muda wa miaka 14. Hata hivyo, Sir Scott alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na taaluma ya fasihi ya lugha.
Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita, yaani 21 Septemba 1909, alizaliwa Dakta Osagyefo Kwame Nkrumah mwanasiasa na shujaa wa uhuru wa Ghana. Nkrumah alishiriki kikamilifu katika harakati za kupigania uhuru za wananchi wa Ghana dhidi ya mkoloni Muingereza. Baada ya kujipatia uhuru, kulijitokeza na kushuhudiwa njama kadhaa za kutaka kumuondoa madarakani na hata kumuua Nkrumah. Mwaka 1966 wakati Dakta Nkrumah akiwa safarini nchini China, Jenerali Joseph Ankrah alifanya mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali Nkrumah. Mwanamapinduzi huyo aliaga dunia mwaka 1972 akiwa uhamishoni nchini Romania. Kwame Nkrumah alikuwa na nafasi muhimu katika kuasisiwa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM pamoja Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika OAU.
Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, majeshi ya dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein yalianza kufanya mashambulio makubwa ya anga na nchi kavu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo vita vya miaka minane vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran vikawa vimeanza. Jeshi la Iraq lilikuwa limefanya uvamizi na mashambulizi kadhaa katika maeneo ya mpakani ya Iran miezi kadhaa nyuma. Magari ya deraya na vikosi 12 vya jeshi la nchi kavu la Iraq viliyashambulia maeneo ya mipaka ya kusini magharibi mwa Iran. Mapambano makali ya wananchi wa Iran yaliwalazimisha askari wa Saddam kurejea nyuma hadi kwenye mipaka inayotambulika kimataifa.
Katika siku kama ya leo miaka 30 iliyopita Bunge la Taifa la Ufaransa lilipasisha sheria iliyopiga marufuku vazi la staha la mwanamke wa Kiislamu, hijabu katika shule za nchi hiyo. Ufaransa ilipasisha sheria hiyo inayowazuia wanafunzi wa kike Waislamu kwenda mashuleni wakiwa na vazi la hijabu licha ya kudai kuwa ni kitovu cha demokrasia na uhuru. Baadaye sheria hiyo ilipanuliwa zaidi na kupiga marufuku vazi la hijabu katika vyuo vikuu na idara za umma. Wachambuzi wengi walikosoa vikali sheria hiyo wakisema inapingana na Katiba ya Ufaransa na Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu zinazosisitiza kuwa kila mtu ana uhuru wa kukubali na kutekeleza itikadi zake za kidini maadamu hazina madhara kwa watu wengine.
Na leo Septemba 21 ni Siku ya Alzheimer's Duniani.
Ugonjwa wa Alzheimer's hutokana na tatizo la neva na husababisha kufa taratibu kwa seli za ubongo na kuzuia matatizo ya kumbukumbu, kufikiri na katika mienendo ya mgonjwa. Pia, ugonjwa huu ndiyo sababu maarufu zaidi ya tatizo la akili la ugonjwa wa kupoteza fahamu, dementia. Kulingana na ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Afya Duniani (WHO), mtu mmoja ulimwenguni hugunduliwa na ugonjwa wa Alzheimer kila sekunde 68. Hivi sasa, zaidi ya watu milioni 50 duniani wanasumbuliwa na ugonjwa wa Alzheimer, na inatabiriwa kuwa idadi ya watu wenye tatizo la akili la dementia itafikia milioni 82 ifikapo 2030, na milioni 152 ifikapo 2050. Siku ya Alzheimer Duniani ni kampeni ya kimataifa ambayo hufanyika kila mwezi Septemba ili kuongeza ufahamu na kupinga unyanyapaa wa watu wenye tatizo hilo la akili. Kauli mbiu na mada ya kampeni ya Siku ya Alzheimer Duniani ya 2023 ni: "Never too early never too late" (Kamwe si mapema sana wala hujachelewe sana). Lengo la kaulimbiu hiyo ni kusisitiza jukumu kuu la kutambua sababu za hatari ya tatizo hilo na kuchukua hatua haraka za kuzuia hatari hiyo.