Oct 21, 2024 02:21 UTC
  • Jumatatu, Oktoba 21, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 17 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria sawa na 21 Okktoba 2024 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 234 iliyopita, alizaliwa malenga wa Kifaransa Alphonse de Lamartine. 

De Lamartine alitambulika kuwa msanii na mwanafikra mkubwa nchini Ufaransa. Aliwahi pia kusafiri Mashariki na kuishi katika mji mkuu wa Lebanon, Bairut. Aidha miongoni mwa athari za malenga huyu, ni pamoja na "Safari ya Mashariki" na "Kimya cha Malaika". 

Alphonse de Lamartine alifariki dunia mwaka 1869.   

Alphonse de Lamartine

Miaka 191 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alizaliwa Alfred Nobel mkemia wa Sweden na mvumbuzi wa dynamite.

Nobel alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza sayansi ya kemia na baadaye akafanya utafiti mkubwa katika uwanja huo na kufanikiwa kuvumbua mada za mlipuko yaani (dynamite). Kinyume na alivyotarajia, majeshi ya nchi mbalimbali yalianza kutumia dynamite vitani na hivyo kusababisha mauaji ya raia wengi.

Mkemia Nobel ambaye alikuwa na utajiri mkubwa na hakufikiri kuwa dynamite ingeweza kutumiwa vibaya, aliamua kutoa utajiri wake kama tuzo na zawadi. Alfred Nobel alifanya hivyo kwa lengo kwamba, tuzo hiyo itolewe kila mwaka kwa shakhsiya aliyefanya kazi kubwa ya thamani duniani katika masuala ya sayansi, fasihi na amani.

Hata hivyo kinyume na matakwa yake, leo hii Tuzo ya Amani ya Nobel imechukua sura ya kisiasa na inatumiwa kama wenzo wa kutangaza na kueneza siasa za nchi za Magharibi duniani.

Alfred Nobel

Katika siku kama ya leo miaka 64 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Somalia ilipata uhuru na siku hii inajulikana nchini humo kama Siku ya Taifa.

Kijiografia Somalia ipo kaskazini mashariki mwa bara la Afrika katika eneo linalojulikana kama Pembe ya Afrika. Mji mkuu wa Somalia ni Mogadishu na lugha rasmi ya nchi hiyo ni Kisomali na Kiarabu. Asilimia 99 ya wananchi wa Somalia ni Waislamu.

Nchi hiyo kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya ukoloni wa Italia na Uingereza mpaka ilipojipatia uhuru mwaka 1960 katika siku kama ya leo. 

Tarehe 30 Mehr miaka 72 iliyopita, Dakta Hussein Fatimi, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Musadiq, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Iran wakati huo alitangaza habari ya kukatwa uhusiano wa kisiasa kati ya Iran na Uingereza.

Uamuzi huo ulikabidhiwa kwa balozi mdogo wa Uingereza mjini Tehran, baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri. Dakta Fatimi alisema Tehran imeamua kukata uhusiano na Uingereza kutokana na upuuzaji wa serikali ya London kwa matakwa ya wananchi wa Iran ya kujipatia haki zao, hususan katika uwanja wa kutaifisha sekta ya mafuta. Dakta Fatimi aliwataka viongozi wa London wabadili siasa zao kuhusiana na Iran.

Dakta Hussein Fatimi

Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita Brigedia Jenerali Mundhir Abu Ghazala, kamanda Jeshi la Majini la Palestina aliuawa na maajenti wa shirika la ujasusi la utawala ghasibu wa Kizayuni Mossad.

Wazayuni walimuuwa kigaidi kamanda huyo wa jeshi la majini la Palestina kwa kutega bomu ndani ya gari lake huko Athens mji mkuu wa Ugiriki.

Brigedia Jenerali Abu Ghazala ni miongoni mwa wahanga wa ugaidi wa kiserikali wa utawala wa kibaguzi wa Kizayuni unaoungwa mkono kwa hali na mali na Marekani. 

Jenerali Abu Ghazala

 

Tags