Oct 24, 2024 02:13 UTC
  • Leo katika Historia, Alkhamisi tarehe 24 Oktoba 2024

Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Rabiuthanil 1446 Hijria sawa na tarehe 24 Oktoba 2024.

Tarehe 24 Oktoba miaka 95 iliyopita ulianza mgogoro mkubwa wa kiuchumi wa Marekani unaojulikana kwa jina la Wall Street.

Kimsingi Wall Street ni mtaa mashuhuri mjini New York ambao kutokana na kuwa na taasisi nyingi kubwa za kifedha na kibenki unatambuliwa kuwa kituo muhimu sana cha kiuchumi cha Marekani. Kituo hicho cha kiuchumi kilikumbwa na mgogoro mkubwa wa kifedha wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia na baada yake.

Oktoba 24 mwaka 1929 janga kubwa la kifedha liligubika makao ya hisa ya Marekani huko Wall Street na kupelekea kukosa kazi zaidi ya wafanyakazi milioni 13 wa Marekani, njaa kali, kufilisika kwa viwanda na mabenki na mamilioni ya watu kupoteza makazi na nyumba zao.

Katika siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, Umoja wa Mataifa ulichukua nafasi ya Jumuiya ya Mataifa.

Wawakilishi wa mataifa yaliyoafikiana katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, yaani Marekani, Urusi, Uingereza na Ufaransa, waliandaa mazingira ya kuundwa umoja huo; na hatimaye katika mkutano uliofanyika San Francisco, Marekani, wawakilishi kutoka nchi 50 duniani walipitisha sheria za kuundwa umoja huo.

Ijapokuwa umoja huo umefanikiwa katika baadhi ya mambo, lakini kuwepo haki ya veto kwa baadhi ya nchi ambazo ni Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, na China kunalifanya Baraza la Usalama la umoja huo kufuata kibubusa siasa za nchi zenye haki ya kupiga kura ya turufu, na hasa Marekani.

Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, Iran ilifanikiwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa hati ya Umoja wa Mataifa, mlango wa kujiunga na umoja huo uko wazi kwa mataifa yote yanayopenda amani na ambayo yanakubaliana na sheria na maaamuzi ya taasisi hiyo.

Nchini Iran, Umoja wa Mataifa una jumla ya ofisi 14 za uwakilishi na utendaji. 

Miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo, vita vya nne baina ya Waarabu na Israel vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Ramadhani vilifikia tamati.

Tarehe 6 Oktoba 1973 Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri akiwa na lengo la kufidia kushindwa katika vita vya Waarabu na Israel mwaka 1967, alifanya mashambulio ya kushtukiza katika ngome za Israel katika Mfereji wa Suez.

Muda mchache baada ya mashambulio hayo, wanajeshi wa Syria nao walifanya mashambulio katika miinuko ya Golan ambayo ilikaliwa kwa mabavu na Israel katika vita vya mwaka 1967  na kufanikiwa kuwatimua wanajeshi wote wa utawala huo haramu kutoka katika maeneo waliokuwa wakiyadhibiti.   

Na katika siku kama ya leo miaka 32 iliyopita aliaga dunia Abul Qassim Halat mshairi, mchekeshaji na mtarjumi wa zama hizi wa Kiirani.

Alianza kutunga mashairi akiwa na umri wa miaka 16 na akaondokea kubobea katika mashairi ya vichekesho. Malengo huyo alikuwa akizifahamu vyema lugha za Kifarsi, Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu. Miongoni mwa athari zake muhimu ni tarjama ya maneno yenye thamani kubwa ya Bwana Mtume (saw) na Imam Ali bin Abi Talib (as).

Abul Qassim Halat ameacha athari nyingi zenye thamani kubwa katika uga wa maishairi.

Abul Qassim Halat