Oct 22, 2024 02:26 UTC
  • Jumanne, Oktoba 22, 2024

Leo ni Jumanne tarehe 18 Rabiuthani 1446 Hijria sawa na tarehe 22 Oktoba 2024.

 Siku kama ya leo miaka 844 iliyopita, alizaliwa Abul Qasim Jafar bin Hassan Hilli maarufu kwa lakabu ya Muhaqiq Hilli, mmoja wa wanazuoni wakubwa na faqihi ya Kiislamu, katika mji mashuhuri wa Hillah, nchini Iraq.

Muhaqiq Hilli alikuwa msomi aliyekuwa na nafasi ya juu na mtaalamu wa sheria za Kiislamu na alibobea pia katika fasihi na uandishi wa mashairi. Baada ya kukamilisha masomo ya awali na kupaa daraja za juu za kiroho, alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa zama zake.

Kitabu muhimu zaidi cha Muhaqqiq al Hilli ni Sharaiul Islam, fii Masaailil-Halal Walharaam'. Mwanazuoni huyo pia ameandika vitabu vya "Al Nafi", "Maarij" na "al Tanbih". Muhaqqiq al Hilli alifariki dunia mwaka 676 Hijria akiwa na umri wa miaka 74.   

Miaka 118 iliyopita katika siku kama ya leo, Paul Cezanne mchoraji maarufu wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67.

Alikuwa na shauku na mapenzi makubwa na fani ya uchoraji tangu akiwa mdogo, lakini kutokana na msisitizo wa baba yake aliingia Chuo Kikuu na kusoma taaluma ya sharia.

Hatimaye akiwa na umri wa miaka 24, baba yake alimruhusu kuendelea na masomo katika taaluma ya uchoraji. Mwanzoni mabango ya uchoraji ya Paul Cezanne hayakupata wafuasi wengi na athari zake za uchoraji zilikabiliwa na ukosoaji mkubwa. 

Mwenendo huo uliendelea hadi alipofikisha umri wa miaka 50 ambapo hatua kwa hatua alianza kupata umashuhuri kutokana na kuuza mabango yake ya uchoraji.

Paul Cezanne

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, aliaga dunia Arnold Joseph Toynbee mwanahistoria mtajika wa Uingereza.

Alizaliwa mwaka 1889. Toynbee alikuwa akifundisha taaluma ya Historia ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha London.

Msomi huyo ameandika vitabu vingi katika uga wa historia na baadhi ya vitabu vyake ni A Study of History, Change and Habit, Choose Life na Civilization on Trial.

Arnold Joseph Toynbee

Miaka 47 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Sayyid Mustafa Khomeini, mtoto wa Imam Ruhullah Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa shahidi kufuatia njama iliyotekelezwa na askari usalama wa utawala wa Shah akiwa nyumbani kwake huko Najaf, nchini Iraq.

Al Haj Mustafa Khomeini alizaliwa mwaka 1309 Hijria Shamsia katika mji mtakatifu wa Qum na baadaye akajiunga na chuo cha elimu ya dini cha mji huo kwa ajili ya masomo ya juu baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Alikuwa hodari mno na alifikia daraja ya juu ya kielimu ya Ijtihadi akiwa na umri wa miaka 27.

Ayatullah Mustafa Khomeini alikuwa pamoja na baba yake, Imam Khomeini katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya utawala wa Shah.   

Sayyid Mustafa Khomeini

Miaka 13 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud aliyekuwa mrithi wa kiti cha Ufalme wa Saudia.

Sultan alikuwa mtoto wa 15 wa kiume wa Mfalme Abdul-Aziz, na mama yake ni Hussa Bint Ahmed Al-Sudairi. Vyombo vya Saudi vilitangaza kuwa, mwanamfalme Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud aliaga dunia katika mojawapo ya hospitali mjini New York, Marekani. Sultan bin Abdul-Aziz aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 85 baada ya maradhi ya saratani kuenea katika mwili wake wote. 

Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud

 

Tags