Oct 25, 2024 02:42 UTC
  • Ijumaa, Oktoba 25, mwaka 2024

Leo ni Ijumaa tarehe 21 Mfunguo Siba Rabiuthani 1446 Hijria sawa na Oktoba 25 mwaka 2024.

Siku kama ya leo miaka 213 iliyopita, mwanakijiji mmoja aligundua alama za awali za mabaki ya miji miwili ya kihistoria ya Pompeii na Herculaneum nchini Italia.

Mji wa Pompeii ulijengwa na kaumu ya Oscan mwanzoni mwa karne ya 6 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa Masih (as) na ulikuwa na bandari maarufu na yenye ustawi mkubwa hadi karne ya kwanza baada ya kuzaliwa Nabii Issa (as).

Mji huo na ule wa Herculaneum ilizikwa na kufunikwa kikamilifu na volcano ya Mlima Vesuvius mwaka 79 Miladia.

Siku kama ya leo, miaka 212 iliyopita, alizaliwa Évariste Galois, mtaalamu wa hesabati wa nchini Ufaransa, karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Paris.

Kufikia umri wa miaka 12, Galois hakufunzwa na mtu yeyote isipokuwa mama yake na alianza kusoma vitabu vya jiometri na hivyo kuinukia kielimu. Baada ya hapo alijiunga na chuo, ambapo alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani katika kila somo.

Baadaye Évariste Galois alianza kutalii elimu ya hisabati. Akiwa na umri wa miaka 18 alikamilisha kazi ya uandishi wa kitabu cha hisabati na baada ya hapo akaandika vitabu vitatu vipya katika taaluma hiyo na kujipatia umashuhuri mkubwa.  Galois aliuawa  akiwa na umri wa miaka 21 hapo tarehe 29 mwezi Mei mwaka 1832 baada ya kutiwa jela wakati wa harakati zake za kisiasa nchini Ufaransa.

Weledi wanaamini kuwa, kama Galois hangeuawa mapema, basi angepiga hatua kubwa katika uga wa hisabati duniani. 

Évariste Galois

Siku kama ya leo miaka 143 iliyopita, alizaliwa Pablo Picasso mchoraji mashuhuri wa Kihispania.

Picasso alikuwa mwasisi wa harakati ya Cubist ambayo ilienea kwa kasi kubwa miongoni mwa wachoraji wa Ufaransa. Pablo Picasso alichora picha nyingi na daima alikuwa akifanya juhudi za kuendeleza harakati hiyo.

Mchoro wa 'The Girls of Avignon' wa mchoraji huyo ndio uliokuwa mwanzo wa mtindo wa Cubism na kazi kubwa zaidi ya Picasso katika mtindo huo ni 'Guernica'. Katika mchoro huo Pablo Picasso anaonesha hofu iliyompata kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na ndege za kivita za Ujerumani na Italia dhidi ya mji wa Guernica.

Picasso alifariki dunia Aprili mwaka 1973.

Pablo Picasso

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, Imam Ruhullah Khomeini baada ya kuachiwa huru kutoka katika jela ya utawala wa Shah alitoa hotuba kali akishambulia vikali kitendo cha kupasishwa sheria ya Capitulation au sheria ya kuwapatia kinga ya kutofikishwa mahakamani raia wa Marekani waliofanya uhalifu nchini Iran. 

Katika hotuba hiyo Imam Khomeini alizishambulia vikali Marekani na utawala ghasibu wa Israel.

Hotuba hiyo iliwaamsha wananchi na kuukasirisha utawala wa kiimla wa Shah kiasi kwamba uliamua kumuwekea vizuizi vingi kiongozi huyo wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu. Siku chache baadaye Imam alipelekwa uhamishoni nchini Uturuki na baadaye Iraq.

Imam Ruhullah Khomeini

Katika siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, televisheni ya taifa ya Iran ilianza kurusha matangazo yake kwa majaribio.

Katika muongo wa 1330 Hijria Shamsia kulijadiliwa suala la kuanzishwa televisheni ya taifa ya Iran ingawa utekelezaji wa mpango huo uliakhirishwa kwa miaka mingi. Uzalishaji wa picha tena kwa masaa kadhaa tu, halikuwa jambo rahisi kwani lilihitajia fedha na uwekezaji binafsi na wa kila wiki.

Ni kwa msingi huo, ndio maana Habibullah Thabit Pasal mwekezaji wa sekta binafsi akaipendekezea serikali ya wakati huo ya Iran ianzishe mnara wa televisheni, pendekezo ambalo lilikubaliwa.

Baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran redio na televisheni ya taifa ilibadilishwa jina na kuwa Shirika la Utangazaji la Radio na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kupiga hatua kubwa mno katika uwanja huo.

Hii leo shirika hili lina makumi ya kanali za televisheni na radio zikiwemo zile za kitengo cha matangazo ya ng'ambo ambapo kuna makumi radio na televisheni za lugha za kigeni kama, Kiingereza, Kifaransa, Kiswahili, Kihispania, Kiarabu, Kihindi, Kipashto, Kijapan, Kiurdu, Kihausa, Kichina, Kirusi na kadhalika.   

Miaka 44 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Khorramshahr wa Iran ulikaliwa kwa mabavu na jeshi la dikteta wa zamani Iraq Saddam Hussein. 

Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane.

Mji huo ulikombolewa tarehe 3 Khordad ambayo inajulikana katika utamaduni wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa jina la "Siku ya Istiqama na Ushindi.   

Ukombozi wa Khorramshahr