Alkhamisi, tarehe 31 Oktoba, 2024
Leo ni Alkhamisi tarehe 27 Rabiuthani 1446 Hijria sawa na Oktoba 31 mwaka 2024.
Miaka 110 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya wakati huo ya Iran ilitangaza kutofungamana na upande wowote katika Vita vya Kwanza vya Dunia.
Hata hivyo udhaifu wa kisiasa wa watawala wa wakati huo, matatizo ya ndani, matatizo ya kivita na kupenda kujitanua kwa nchi zilizokuwa zikipigana katika vita hivyo ni mambo yaliyopelekea nchi hii kwenda kinyume na ahadi yake ya kutofungamana na upande wowote katika vita hivyo.
Ni kutokana na hali hiyo, ndipo Iran ikajikuta katika hujuma na mashambulizi ya majeshi ya Uingereza, Urusi ya zamani na jeshi la Othmania na kuisababishia hasara kubwa. ***
Katika siku kama ya leo miaka 44 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Aban 1359 Hijria Shamsia, alikamatwa mateka Mhandisi Muhammad Jawad Tondguyan Waziri wa Mafuta wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na maafisa kadhaa wa wizara hiyo.
Operesheni hiyo ilifanywa na majeshi ya Iraq mwezi mmoja tu baada ya majeshi ya Iraq kushambulia ardhi ya Iran. Mhandisi Tondguyan alikwenda kusini mwa Iran kwa shabaha ya kukagua visima na viwanda vya mafuta katika eneo hilo.
Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia.
Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini.
Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea ma lufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr.
Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu.
Tarehe 31 Oktoba 1984 yaani siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, aliuawa Bi. Indira Gandhi, Waziri Mkuu wa wakati huo wa India.
Mauaji hayo yalifanywa na walinzi wawili wa kiongozi huyo ambao walikuwa Masingasinga. Masingasinga hao walifanya mauaji hayo baada ya Gandhi kutoa amri ya kushambuliwa hekalu la dhahabu lililoko katika jimbo la Punjab, ambalo lilihesabiwa na masingasinga kuwa ni eneo takatifu.
Masingasinga ambao wanaunda asilimia mbili ya watu wa India na wengi wao wanaishi katika jimbo la Punjab, walikusanya silaha zao kwenye hekalu hilo kwa shabaha ya kufanya uasi na kutaka kujitenga jimbo hilo.
Na katika siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, aliaga dunia Federico Fellini mtengenezaji filamu maarufu wa Kiitalia. Fellini ni miongoni mwa watengenezaji na waongozaji filamu wakubwa wa karne ya ishirini. Fellini alianza kazi ya kuandika filamu tangu mwaka 1938 na baadaye akajiingiza katika utengenezaji filamu.
Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1945, Federico Fellini akiwa msaidizi wa mtengeneza filamu aliyejulikana kwa jina la Roberto Rossellini walitengeneza filamu iliyojulikana kwa jina la "Rome Open City". Mwaka 1993, yaani miezi sita kabla ya kifo chake, Fellini alitunukizwa tuzo ya Oscar kutokana na kazi zake za thamani katika ulimwengu wa filamu.