Nov 24, 2024 02:26 UTC
  • Jumapili, 24 Novemba, 2024

Leo ni Jumapili 22 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1446 Hijria ambayo inasadifiana na 24 Novemba 2024 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 392 iliyopita, alizaliwa Baruch de Spinoza mwanafalsafa na mtaalamu wa elimu jamii wa Uholanzi. Spinoza alisoma kwa bidii na kukwea daraja za kielimu. Hata hivyo ukosoaji wake wa dini ya Kiyahudi ulimfanya akabiliwe na chuki na uhasama wa maulama wa dini hiyo. Njia na fikra za kifalsafa za Spinoza zilikaribiana na itikadi za kisufi. Msomi huyo wa elimu ya falsafa wa Uholanzi ameandika pia vitabu kadhaa kama The Philosophy of Spinoza na The Road to Inner Freedom. Baruch de Spinoza alifariki dunia mwaka 1677. 

Baruch de Spinoza

 

Katika siku kama ya leo miaka 193 iliyopita, Michael Faraday mwanafizikia stadi wa Kiingereza aligundua mkondo wa umeme unaojulikana kitaalamu kama ''Electric Current''. Kwa ugunduzi huo Faraday akawa amefanikiwa kupiga hatua kubwa katika elimu ya fizikia. Faraday alizaliwa mwaka 1791 na awali alikuwa akifanya kazi katika duka la kuuza vitabu. Ni kipindi hicho ndipo taratibu alipoanza kusoma vitabu mbalimbai na kuanza kuvutiwa na masuala ya kielimu. Miaka michache baadaye akawa msaidizi wa maabara. Akiwa katika maabara hiyo Faraday alifanya utafiti mwingi kuhusiana na jinsi ya kutengeneza balbu za umeme. Miongoni mwa mafanikio mengine makubwa yaliyoletwa na mtaalamu huyo ni pale alipogundua mota ya umeme pamoja na kubadilisha nguvu za sumaku kuwa nguvu za umeme.

Michael Faraday

 

Katika tarehe kama ya leo miaka 160 iliyopita, alizaliwa mchoraji na msanii mkubwa wa Ufaransa, Henri Toulouse Lautrec. Familia ya Lautrec ilikuwa ya kipato cha wastani na licha ya kukabiliwa na matatizo mengi ya kimaisha, Lautrec alitokea kuwa miongoni mwa wasanii mashuhuri na hodari wa Ufaransa kutokana na kipawa chake kikubwa. Msanii huyo alifariki dunia mwaka 1901. 

Henri Toulouse Lautrec

 

 

Miaka 74 iliyopita katika siku kama yya leo, Tume ya Mafuta ya Bunge la Taifa la Iran, ilipinga mkataba ziada wa mafuta kati ya Iran na Uingereza. Mkataba huo ulikuwa na lengo la kuimarisha nafasi ya Uingereza na kuzidisha uwezo wa nchi hiyo kuchimba mafuta huko kusini mwa Iran. Vilevile mkataba huo uliotayarishwa katika kilele cha ushindani wa Marekani na Uingereza wa kupora utajiri wa mafuta wa Iran, ulitambuliwa kuwa ni tishio kwa maslahi ya taifa.

 

Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, alifariki dunia Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani, mmoja wa Marajii Taqlidi na maurafaa wakubwa wa Kishia. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria Shamsia katika mji wa Fouman ulioko katika mkoa wa Gilan kaskazini mwa Iran. Baada ya kupata elimu ya msingi ya kidini, mwaka 1308 Hijria Shamsia alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Ayatullah Bahjat alikuwa mashuhuri sana kutokana na uchaji Mungu wake. Kitabus Swalat, Jamiul Masail na Wasilatun Najat ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.

Ayatuhil Udhma Muhammad Taqi Behjat Foumani

 

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 81 Muhammad Hadi Farzaneh, maarufu kwa jina la Hakim Farzaneh, mtaalamu mkubwa wa elimu ya theolojia na falsafa. Hakim Farzaneh alizaliwa mwaka 1302 Hijiria katika moja ya maeneo ya mji wa Isfahan. Alisoma elimu ya msingi eneo alikozaliwa na kisha kuelekea mjini Isfahan kwa ajili ya kuendelea na masomo yake ambapo alipata kusomea elimu mbalimbali muhimu hususan theolojia na falsafa. Aliweza kuinukia kielimu na kuwa msomi mkubwa kiasi kwamba mwishoni mwa umri wake alikuwa miongoni mwa wataalamu wa taaluma hizo. Baadaye alirejea katika mji alikozaliwa na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji hadi alipofariki dunia. ***

Muhammad Hadi Farzaneh

 

Miaka 58 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 4 Azar 1345 Hijria Shamsia, alifariki dunia mhadhiri wa chuo kikuu Jabbar Baghche Ban baada ya kutumia muda wake mwingi katika kuwahudumia kwa moyo mkunjufu viziwi wa Iran. Mnamo mwaka 1302 Hijria Shamsia, Baghche Ban alianzisha kituo cha kuwafunza na kuwalea watoto viziwi katika mji wa Tabriz, ulioko kaskazini magharibi mwa Iran na huo ndio uliokuwa mwanzo wa jitihada za muda mrefu za mhadhiri huyo za kuwafundisha watoto viziwi. Aliwafundisha watoto hao kusoma na kuandika kwa kugundua mbinu mpya za kujifunza alfabeti ambayo inatumika siku hizi. Baghche Ban pia mwaka 1313 Hijiria Shamsia alianzisha shule ya kwanza ya wanafunzi viziwi nchini Iran. ***

Jabbar Baghche Ban

 

Na siku kama ya leo miaka 11 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi 6 zinazounda kundi la 5+1 zilitia saini makubaliano ya muda ya nyuklia mjini Geneva huko Uswisi. Kutiwa saini makubaliano hayo kulitayarisha uwanja mzuri na kufungua njia ya mazungumzo zaidi kati ya Iran na nchi hizo sita ambazo ni Marekani, Ufaransa, Uingereza, Russia, China na Ujerumani kwa ajili ya kutia saini makubaliano kamili ya nyuklia na kuondoa hitilafu kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia hapa nchini, na mwishowe kufutwa vikwazo vya kidhalimu vilivyowekwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.