Jumapili, Mosi Disemba, 2024
Leo ni Jumapili 29 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1446 Hijria mwafaka na Mosi Disemba 2024 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 172 iliyopita, alizaliwa alimu na mtaalamu wa lugha wa Kiirani Ayatullah Sheikh Muhammad Qasim Ordubadi katika mji wa Tabriz ulioko kaskazini Magharibi mwa Iran. Baada ya kumaliza masomo yake ya kati alielekea Najaf nchini Iraq ambapo alipata elimu kwa Maulamaa mashuhuri wa mji huo. Msomi huyo mkubwa baada ya kufikia daraja ya ijtihadi alirejea katika mji wa Tabriz na kuanza kufundisha. Ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha "Al Shihabul Mubin fii I'jaazil Qur'an." Alifariki dunia mwaka 1333 Hijria.
Katika siku kama ya leo miaka 199 iliyopita, muungano wa kihistoria wa nchi za Ulaya uliojulikana kama Muungano Mtakatifu ulisambaratika baada ya kujiengua utawala wa Kikaitsar (Tsarist) wa Russia katika muungano huo. Baada ya kuanguka kwa utawala wa Napoleon, muungano huo ukaunda Congress ya Vienna, kati ya tawala za Russia, Austria na ufalme wa Pros na serikali hizo zikaafikiana kwamba nchi zilizo chini ya utawala wa muungano huo na katika uhusiano wa kimataifa zifuate misingi ya dini ya Kikristo.
Siku kama ya leo miaka 167 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria alifariki dunia Abdul Baqi bin Sulaiman Farooqi anayehesabiwa kuwa miongoni mwa wataalamu na malenga wa lugha ya Kiarabu. Alikuwa na kipawa cha kutunga mashairi ya kuvutia tangu akiwa kijana. Abdul Baqi alikuwa miongoni mwa wapenzi wa kizazi cha mtukufu Mtume Muhammad (saw) na alidhihirisha mapenzi yake hayo katika mashairi yake. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kile alichokipa jina la "Al Baqiyatus Swalihat."
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, Mirza Kuchak Khan Jangali, mwanaharakati na mpigania ukombozi wa Kiirani aliuawa shahidi na vibaraka wa Reza Khan, dikteta wa wakati huo wa Iran kwa ushirikiano wa madola ya Umoja wa Kisovieti na Uingereza. Mirza Kuchak Khan Jangali alijifunza masomo ya dini akiwa katika rika la ujana na kufanikiwa kukwea daraja za juu za kielimu. Baadaye alijiunga na safu ya wapigania uhuru hadi alipokamatwa na vibaraka wa Reza Khan na kuuawa kwa kukatwa kichwa kilichopelekwa kwa mfalme huyo kibaraka. ***
Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita David Ben-Gurion mmoja wa waasisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Waziri Mkuu wa kwanza wa utawala huo ghasibu aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87. Ben-Gurion alizaliwa tarehe 16 Oktoba 1886 katika mji wa Plonsk huko Uholanzi ambayo katika zama hizo ilikuwa sehemu ya ardhi ya ufalme wa Russia. Alielekea katika ardhi za Palestina mwaka 1906 akiwa na umri wa miaka 20 na kuasisisi harakati ya Kiyahudi. Katika Vita vya Kwanza vya Dunia David Ben-Gurion alikuwa na nafasi kubwa katika kuwahamisha taratibu Mayahudi kwenda ardhi za Palestina. Katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia harakati hiyo ilishika kasi chini ya uungaji mkono wa madola makubwa hususan Uingereza, kiasi kwamba mwaka 1948 sawa na tarehe 5 Mei na baada ya kupitishwa azimio na Umoja wa Mataifa la kuigawa Palestina katika pande mbili za Kiyahudi na Palestina, kulitangazwa rasmi kuanzishwa utawala haramu wa Kizayuni na wa kibaguzi wa Israel. Masaa machache baadaye, Marekani na Urusi ya zamani zikatangaza kuutambua utawala huo khabithi.
Na tarehe Mosi Disemba kila mwaka, nchi mbalimbali duniani huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ukimwi. Ukimwi ni ugonjwa wa kuambukiza ambao unatokana na kurundikana kwa virusi vya HIV mwilini ambavyo huharibu mfumo wa ulinzi wa mwili na kutayarisha mazingira ya kushambuliwa na maradhi nyemelezi. Ugonjwa huu ulibainika kwa mara ya kwanza kabisa nchini Marekani mwazoni mwa miaka ya 1980. Wakati huo baadhi ya wanaume wanaofanya ngono kinyume na maumbile huko New York na California waligundulika kuwa na kansa ambazo hazikukubali tiba ya aina yoyote. Japokuwa wakati huo, haikujulikana sababu ya maambukizi ya ghafla ya magonjwa hayo lakini tukio hilo limetambuliwa kuwa ndiyo mwanzo wa kujitokeza maradhi ya Ukimwi. Ugonjwa huo ambao haukuwa na jina ulienea kwa kasi kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja na hatimaye mwaka 1982 ulipewa jina la Ukimwi.
