Jumanne, 03 Disemba, 2024
Leo ni Jumanne tarehe Mosi Mfunguo Tisa Jamaduthani 1446 Hijria mwafaka na tarehe tatu Disemba, 2024.
Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita, alizaliwa Dakta Rajendra Prasad, mwanasiasa na mwanafilosofia wa India huko katika mojawapo ya vijiji vya jimbo la Bihar.
Rajendra Prasad aliweza kuendelea na masomo na kufikia daraja ya udaktari, licha ya hali duni ya kifedha ya familia yake. Alishirikiana na wananchi wa India katika mapambano ya kupigania uhuru wa nchi yao.
Prasad vilevile alikuwa bega kwa bega na Mahatma Gandhi katika mapambano ya kisiasa dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na kwa mara kadhaa aliteuliwa kuongoza chama cha Congress ya Kitaifa ya India.
Rajendra Prasad aliteuliwa kuwa Rais wa kwanza wa India baada ya uhuru na kuasisiwa mfumo wa jamhuri nchini humo mwaka 1950.
Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 3 mwezi Disemba mwaka 1984, kulitokea janga kubwa la kuvuja gesi ya kemikali katika kiwanda kimoja cha Marekani katika mji wa Bhopal huko katikati mwa India.
Kiwanda hicho kilikuwa kikimilikiwa na kampuni ya Kimarekani iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Union Carbide. Uzembe wa maafisa wa kiwanda hicho na kutozingatiwa viwango vya usalama kulipelekea kuvuja kwa gesi ya sumu ya sianidi (cyanide) kutoka katika kiwanda hicho na kuenea katika hewa.
Wakazi wasio na hatia wa mji wa Bhopal wasiopungua 2500 walipoteza maisha yao na mamia ya wengine pia kujeruhiwa katika janga hilo.
Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, mkutano wa kwanza wa Kiislamu kuhusiana na Palestina ulifanyika hapa mjini Tehran.
Mkutano huo ulifanyika katika fremu ya mfungamano wa walimwengu na mapambano ya Intifadha ya Palestina na kukabiliana na wimbi la kuhajiri Mayahudi kuelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Ajenda kuu ya mkutano huo ilikuwa kuchunguza chanzo cha mapambano ya Intifadha ya wananchi Waislamu wa Palestina, Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi hao pamoja na taathira ya matukio ya Mashariki ya Kati kwa taifa la Palestina.

Miaka 13 iliyopita katika siku hii, tarehe 13 Azar 1390 Hijiria Shamsiya mamlaka ya kijeshi ya Iran ilitangaza kuidhibiti ndege ya kijasusi ya Marekani isiyo na rubani au drone aina ya RQ-170 mashariki mwa nchi.
Ndege hii iliyokuwa imepaa kutoka nchini Afghanistan, iliangukia kwenye mtego wa vitengo vya vita vya kielektroniki vya Iran katika umbali wa kilomita 200 ndani ya Iran na kudhibitiwa na wataalamu wa Iran.
Ndege hiyo ya RQ-170 ni mojawapo ya ndege za kisasa zaidi zisizo na rubani za jeshi la Marekani.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuchukua udhibiti wa ndege ambayo ina uwezo wa kukwepa rada, ilionyesha uwezo wake katika uwanja wa vita vya kielektroniki na kusababisha mshangao mkubwa miongoni mwa wataalamu wa kijeshi wa Marekani. Baada ya miaka mitatu, wataalamu wa Iran waliweza kunakili teknolojia ya uundaji wake na miaka mitatu baadaye walitengeneza mfano wake.

Na tarehe 3 Disemba imetangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa ni siku ya Kimataifa ya Walemavu.
Lengo la hatua hiyo ni kuboresha nafasi ya watu wenye ulemavu katika jamii za kibinadamu
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu nusu bilioni duniani ni walemavu. Vilevile watu wenye ulemavu ni moja ya kumi ya wakazi wa nchi nyingi duniani.
Inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya walemavu wanaishi katika nchi zinazoendelea, kwa sababu ulemavu mwingi unasababishwa na utapiamlo, umaskini, ukosefu wa huduma za afya na elimu na mambo mengine ambayo ni matokeo ya kubakia nyuma kimaendeleo.
