Ijumaa, tarehe 6 Disemba, 2024
Leo ni Ijumaa tarehe 4 Jumadilthani 1446 Hijria sawa na Disemba 6 mwaka 2024.
Katika siku kama ya leo miaka 246 iliyopita yaani tarehe 6 Disemba mwaka 1778, alizaliwa Joseph Louis Gay-Lussac mwanafizikia na mwanakemia wa Ufaransa.
Gay-Lussac alifanya tafiti nyingi na kugundua vitu mbalimbali katika kipindi cha maisha yake. Miongoni mwa mambo yaliyogunduliwa na mwanakemia huyo ni gesi ya sumu ya halogen, kipimio cha ulevi, hydromita au chombo cha kupimia uzito wa maji na viowevu na kuitambua Chloride na Iodine kama elementi mpya.
Miongoni mwa kazi zake muhimu za kisayansi alizofanya mwanakemia huyo ni kuweka kanuni ya kupanuka kwa gesi. Kanuni hiyo iliyopewa jina lake pamoja na la mshirika wake ilijulikana kama Law of Charles and Lussac. Gay-Lussac alifariki dunia mwaka 1850.
Miaka 103 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Finland iliyokuwa chini ya utawala wa Russia ilijipatia uhuru. Kuwa jirani Finland na Russia kuliwatia wasiwasi mno viongozi wa Finland, kiasi kwamba, katika karne ya 12 waliiomba Sweden iwahami dhidi ya Moscow. Badala yake Wasweden waliikalia kwa mabavu Finland. Mwaka 1721 Russia iliivamia Finland na kudhibiti sehemu ya ardhi ya nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1917 vikosi vamizi vya Russia vililazimika kuondoka nchini Finland na nchi hiyo ikajitangazia uhuru. *****
Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, inayosadifiana na 16 Azar 1332 Hijria Shamsia, upinzani wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tehran dhidi ya safari ya Richard Nixon, Makamu wa Rais wa Marekani katika kipindi hicho hapa nchini, ulipelekea wanachuo watatu kuuawa na askari vibaraka wa utawala dhalimu wa Shah.
Safari hiyo ilifanyika miezi mitatu na nusu tu baada ya mapinduzi ya Marekani dhidi ya serikali ya Dakta Muswaddeq. Siku ya pili baada ya mauaji hayo, Richard Nixon alitunukiwa shahada ya heshima ya uzamivu wa sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran.
Kwa mnasaba huo, tarehe 16 Azar kila mwaka huadhimishwa nchini Iran kama "Siku ya Mwanachuo" hapa nchini.
Katika siku kama ya leo miaka 71 iliyopita Sayyid Mujtaba Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini.
Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah.
Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.
Tarehe 6 Disemba miaka 33 iliyopita, Wahindu wenye misimamo mikali waliubomoa Msikiti wa Babri katika mji wa Faizabad kwenye jimbo la Uttar Pradesh nchini India.
Msikiti huo ulijengwa mwaka 1528 na Zahiruddin Muhammad Babur juu ya kilima na tangu wakati huo ulijulikana kwa jina la Msikiti wa Babri. Baada ya kupita karne tatu tangu ujengwe yaani mwaka 1855, mtawala mmoja Muingereza alipotosha ukweli kwa makusudi na kuandika kuwa msikiti huo umejengwa kwenye magofu ya jumba la ibada ya masanamu la Wahindu. Suala hilo lilikuwa chanzo cha fitina na ugomvi mkubwa kati ya Waislamu na Wahindu. Mwaka 1992 Wahindu wenye misimamo ya kufurutu mipaka walivamia Msikiti wa Babri na kuubomoa kikamilifu, suala ambalo lilizusha vita baina ya Waislamu na Wahindu.