Jumamosi, 07 Disemba, 2024
Leo ni Jumamosi 5 Mfunguo Tisa Jamad al-Thani 1446 Hijria ambayo inasadifiana na 7 Disemba 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1018 iliyopita, inayosadifiana na tarehe na tarehe 5 Mfunguo Tisa Jamadi Thani mwaka 428 Hijria, alifariki dunia Abul Hassan Mahyar Deilami, mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiirani. Awali msomi huyo alikuwa mfuasi wa dini ya Kizartoshti, hata hivyo kutokana na kupata elimu na miongozo kutoka kwa wasomi mashuhuri katika zama zake, hatimaye alisilimu na kuingia katika dini ya Kiislamu. Kwa muda mrefu Deilami alisoma kwa mwalimu wake Sayyid Radhi.
Katika siku kama ya leo miaka 826 iliyopita, aliaga dunia huko Damascus Syria Ibn Qudamah Moqaddasi fakihi na mpokezi hadithi wa Kiislamu. Ibn Qudamah alihitimu masomo yake ya awali na ya utangulizi huko Damascus ambapo alijifunza Qur'ani na hadithi. Baadaye alifanya safari huko Baghdad katika Iraq ya leo na kuhudhuria masomo ya maulama na wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Ibn Qudamah hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi wa vitabu na amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vyenye thamani kubwa. Kitabu cha Raudhatun Nadhir ni moja tu kati ya vitabu hivyo.
Miaka 774 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia Maulana Jalaluddin Balkhi maarufu kwa jina la Moulavi mmoja wa malenga na washairi mahiri wa Iran. Moulavi alikuwa mshairi mkubwa na mwenye uwezo na kipaji kikubwa katika karne ya 7 Hijria. Alizaliwa mwaka 604 Hijria katika mji wa Balkhi kaskazini mwa Afghanistan ya leo. Miongoni mwa athari kubwa za Maulana au Jalaluddin Balkhi ni kitabu cha mashairi cha Masnavi Manavi.
Tarehe 7 Disemba miaka 135 iliyopita gari la kwanza la kisasa duniani lilitengenezwa. Gari hilo lililokuwa na uwezo wa kutembea kilomita 12 kwa saa lilitengenezwa na msomi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Karl Friedrich Benz. Gari hilo lilitumia nishati ya petroli au alkoholi. Karl Benz alifariki dunia mwaka 1929.
Miaka 83 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, wakati Vita vya Pili vya Dunia vilipokuwa vimeshadidi barani Ulaya, ndege mia mbili za kivita za Japan zilishambulia kituo cha jeshi la Marekani katika bandari ya Pearl (Pearl Harbor). Shambulizi hilo lilifanyika wakati Japan ilipokuwa katika mazungumzo na Marekani kuhusu masuala ya mashariki mwa Asia. Sambamba na mashambulizi hayo ambayo yaliharibu meli 19 za kivita za Marekani, jeshi la Japan pia lilifanya mashambulizi makubwa katika nchi za kusini mwa Asia. Baada ya mashambulizi hayo Marekani ilitangaza vita dhidi ya Japan na Vita vya Pili vya Dunia vikapanuka zaidi hadi mashariki mwa Asia.

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, Abdul Wahhab Kayyali mmoja wa wanamapambano wa Palestina aliuawa na magaidi wa Kizayuni mjini Beirut. Aliingia katika masuala ya kisiasa akiwa mwanafunzi na risala yake ya shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha London pia ilihusu masuala ya Palestina na mapambano ya Waarabu dhidi ya ukoloni na Uzayuni.