Hikma za Nahjul Balagha 78 - 81 (71)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 78 (81) ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama zilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi hiki. Ingawa hii ni sehemu ya 78 (81) ya mfululizo huu, lakini hikma tunayoichambua leo ni ya 71.
إِذَا تَمَّ العَقلُ نَقَصَ الکَلامُ
Akili inapokuwa timamu, maneno huwa machache.
Imam Ali AS anasema katika hikma hii ya 71 ya Nahjul Balagha kwamba, mtu kuwa na maneno machache ni ishara ya kuwa na akili timamu.
Katika hikma hii muhimu, Imam Ali AS anaashiria uhusiano wa karibu uliopo baina ya akili na maneno. Kadiri akili inavyokuwa kamilifu zaidi, ndivyo maneno yanavyozidi kupungua na kuwa machache zaidi. Katika fasihi ya lugha ya Kiarabu, neno "Aql" asili yake ni kukataza na kuzuia kitu. Tab'an, kuna maana nyingine za "Aql" ambazo zinahusiana na maana yake ya asili. Kwa mfano, kifaa kinachotumika kufunga goti la ngamia kinaitwa “Aqal” kwa sababu kinamzuia ngamia kutembea na kuendelea na safari. Akili ya mwanadamu pia inaitwa akili kwa sababu inamzuia na ujinga na kutenda matendo maovu.
Ulimi wa mwanadamu umepewa nguvu na Mwenyezi Mungu ya kunyanyuka na kuzunguka upande huu na ule ili uweze kuzungumza na kubainisha hisia za ndani ya nafsi ya mtu. Lakini matamanio, hasira, ghadhabu na ghariza nyingine zilizomo ndani ya mwanadamu zinajaribu kumdhibiti mwanadamu kikamilifu. Hivyo akili ina muhimu mkubwa sana katika kumwokoa mwanadamu na mabalaa ya ghariza na hawaa za nafsi. Ni jambo lisilo na shaka kwamba, wakati ulimi unapodhibitiwa na kunyanyuliwa pale tu panapohitajika, uwezo wa akili wa kuudhibiti ulimi huo huongezeka na ulimi nao hufika wakati ukawa umezoea kufuata amri ya akili na mwishowe huwa haunyanyuki kutamka neno ila baada ya kulipitisha akilini kwanza ili liangaliwe ni sawa litamkwe au ni baya lisitamkwe. Ni kwa sababu hii pia ndio maana tunaona kwamba matamshi ya watu watukufu na mawalii wa Mwenyezi Mungu huwa hayapitwi na wakati hata baada ya kupita karne nyingi sana kwani matamshi hayo yalitolewa baada ya kupitia kwenye mchujo wa akili salama. Lakini watu wanaopenda kuropoka, watu wenye maneno mengi, mara nyingi huwa hawapati nafasi ya kufikiri kwanza kabla ya kutamka maneno hayo na ndio maana mara kwa mara watu hao hutamka maneno yanayogongana. Baadhi ya wakati mtu huyo hutamka maneno yanayowakasirisha wengine na kuwafanyia kejeli na istihzai, na kimsingi mdhurika wa kwanza wa maneno hayo huwa ni mtu mwenyewe aliyeyatamka kwani hupoteza kitu cha thamani sana, nacho ni hadhi na heshima yake.
Suala jengine muhimu ni kwamba, kwa hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu maasumu AS, madhambi makubwa ya mwanadamu yanatokana na ulimi. Hivyo mtu muumini hujiepusha sana na kusema maneno mengi ili kujiwekea kinga katika hatari za kutumbukia kwenye makosa. Vile vile kuzungumza sana kunapoteza bure nishati na nguvu za mwanadamu na hupelekea kuzuka uadui na hasira za watu wengine. Imepokewa hadithi kutoka kwa Imam Husain AS ambaye amesema, akili ya mwanadamu kila siku inakaribia zaidi kwenye viunga vingine vya mwili na inaviambia mnaendeleaje? Viungo vinajibu kwa kusema, iwapo utatuachia huru tutaendelea vyema. Muogope Mwenyezi Mungu na usitushughulishe na mambo mengine. Baadaye viungo vingine vya mwili vinaujibu ulimi kwa kuuambia, sisi hupata malipo mema kwa sababu yako na tunapata adhabu pia kwa sababu yako.
Unapoizingatia hadhithi hiyo utaona kuwa, ulimi ni kiungo muhimu sana na ndiyo sababu ya kupata adhabu au kusalimika viungo vingine vya mwili.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.