Jumanne, 25 Machi, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 24 Ramadhani 1446 Hijria, sawa na tarehe 25 Machi, 2025.
Siku kama ya leo miaka 736 iliyopita, alifariki dunia Qutbuddin Shirazi, tabibu, mwanahesabati, mwanafikizia na mwanafalsafa wa Kiirani katika mji wa Tabrizi huko kaskazini magharibi mwa Iran.
Qutbuddin Shirazi alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Khaja Nasiruddin Tusi. Alibobea pia katika elimu za mantiki na irfani. Alifanya hima kubwa kutafuta elimu ya tiba na alihudumu kwa miaka mingi kama tabibu katika hospitali ya Shiraz, kusini mwa Iran.
Qutbuddin Shirazi alikuwa mtu wa kwanza kufanya uchunguzi kuhusu upinde wa mvua na kupata tafsiri ya kisayansi kuhusu suala hilo. Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameandika vitabu vingi katika taaluma mbalimbali. ***

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, mkataba wa kuasisi Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya au kwa jina jingine Soko la Pamoja la Ulaya ulisainiwa huko Roma mji mkuu wa Italia kati ya wawakilishi wa nchi mbalimbali za bara hilo.
Jumuiya hiyo iliundwa kwa lengo la kuasisi umoja wa forodha kati ya nchi wanachama ili kufuta ushuru wa bidhaa na baada ya hapo, ubadilishanaji wa bidhaa, nguvu kazi, vitega uchumi na huduma nyinginezo pia ukawa huru kati ya nchi wanachama.
Jumuiya hiyo ilikuwa utangulizi wa kuundwa Umoja wa Ulaya mwaka 1992. ***
Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, Mfalme wa wakati huo wa Saudi Arabia, Faisal bin Abdulaziz, aliuawa na mwana wa ndugu yake mwenyewe, Faisal bin Saaid bin Abdulaziz.
Faisal bin Saaid alifanya mauaji hayo akilalamikia kupunguzwa kwa mshahara wake. Japokuwa hitilafu katika kizazi cha wafalme wa Saudi Arabia zimekuwepo siku zote na zimekuwa zikipamba moto mara kwa mara lakini mauaji ya Mfalme Faisal yalikuwa ya kwanza ya mfalme wa nchi hiyo kutokana na hitilafu kama hizo.
Muuaji wa Mfalme Faisal pia alikatwa kichwa mbele ya umati wa watu tarehe 18 Juni mwaka 1975. Baada ya Faisal, Khalid mwana mwingine wa Abdulaziz alishika kiti cha ufalme wa Saudi Arabia. ***

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, vikosi vamizi vya Marekani ambavyo mwezi Disemba 1992 viliwasili nchini Somalia kwa kisingizio cha kukomesha uasi nchini humo, hatimaye vililazimika kuondoka katika nchi hiyo baada ya kushindwa vibaya na bila ya kutarajia.
Mwaka 1991 makundi mbalimbali ya Somalia yalimpindua dikteta wa nchi hiyo Muhammad Siad Barre. Hata hivyo makundi hayo yalishindwa kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya mseto na mkwamo huo wa kisiasa ukapelekea kuzuka vita vya ndani nchini humo.
Marekani ilituma wanajeshi wake huko Somalia katika fremu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa ili kulinda maslahi yake nchini humo, kutokana na nafasi muhimu ya Somalia katika eneo la Pembe ya Afrika. Jeshi la Marekani lilikabiliwa na mapambano makali ya Wasomali na kupoteza askari karibu 100. ****
