Jumatano, tarehe 09 Aprili, 2025
Leo ni tarehe 10 Shawwal 1446 Hijria sawa na Aprili 09, 2025.
Siku kama ya leo miaka 1118 iliyopita alifariki dunia Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi, maarufu kwa jina la 'Ibn Muqlah', mwandishi, mchora hati na mvumbuzi wa hati tofauti za uchoraji.
Alizaliwa Baghdad na kujifunza masomo ya dini kwa wasomi mashuhuri wa mji huo kipindi hicho. Akiwa kijana Ibn Muqlah aliingia katika idara ya vyombo vya mahakama katika utawala wa Ibn Abbas. Hata hivyo muda mfupi na kutokana na upinzani wake mkali dhidi ya utawala na mienendo iliyokuwa kinyume na dini ya watawala hao, walipatwa na hasira na hivyo kumtia jela Ibn Muqlah. Hatimaye na kutokana na amri ya mtawala wa wakati huo, watumishi wa utawala walimkata ulimi na mikono msomi huyo na kisha kumuua shahidi muda punde baadaye. Umashuhuri wake mwingi ulishuhudiwa katika sekta ya uchoraji.
Miongoni mwa vitabu vya Abu Ali Muhammad Ibn Abdullah Baghdadi ni pamoja na 'Risaalat fi Ilmil-Khat wal-Qalam' na 'Risalat fi Mizaanul-Khat.'

Tarehe 9 Aprili miaka 399 iliyopita aliaga dunia mwanafalsafa maarufu wa Uingereza, Francis Bacon.
Awali, Bacon alijishughulisha na masuala ya kisiasa na baadaye alikamatwa na kufungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kula rushwa. Kipindi cha kufungwa jela kilikuwa fursa mwafaka kwa Francis Bacon kudhihirisha kipawa chake. Mwanafalsafa huyo alitoa mchango mkubwa katika kueneza sayansi asili nchini Uingereza na kuhuisha sayansi na falsafa barani Ulaya.
Bacon ameandika vitabu kadhaa kikiwemo kile cha New Atlantis. Msomi huyo wa Uingereza alifariki dunia mwaka 1626.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, utawala ghasibu wa Israel ulifanya mauaji ya kinyama katika kijiji cha Deir Yassin huko magharibi mwa Baitul Muqaddas.
Mauaji hayo yalifanyika wakati wa vita vya kwanza vya Waarabu na Israel na yalitekelezwa na Wazayuni wa kundi la Irgun lililokuwa likiongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Israel, Menachem Begin.
Eneo la Dier Yassin lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Wazayuni kutokana na kuwa katika njia ya Baitul Muqaddas na karibu na pwani. Baada ya kukivamia kijiji cha Deir Yassin, Wazayuni hao waliwaua kinyama wakazi 270 ambao hawakuwa na hatia yoyote wa kijiji hicho.
Mauaji hayo yaliwalazimisha Wapalestina wengi wa eneo hilo kukimbia makazi yao kwa kuhofia kukaririwa mauaji kama hayo ya kinyama.
Miaka 33 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Waserbia wa Bosnia waliokuwa wakiungwa mkono na kusaidiwa na dikteta wa zamani wa Yugoslavia Slobodan Milosevic, walianza mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo katika mji wa Belgrade.
Mauaji hayo yalianza baada ya kutangazwa matokeo ya kura ya maoni hapo tarehe Mosi Machi 1992 ambayo kwa mujibu wake asilimia 99 ya washiriki walipiga kura ya kujitenga Bosnia Herzegovina na Yugoslavia ya zamani. Hata hivyo Waserbia wachache wa Bosnia walipinga suala hilo la kuanzisha uasi kisha baadaye wakajitangazia mamlaka ya Seribia katika maeneo yao.
Milosevic aliwaunga mkono Waserbia na kuanzisha vita vikubwa zaidi vya mauaji ya kimbari barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Hadi vita hivyo vinamalizika mwaka 1995 zaidi ya Waislamu laki moja wa Bosnia walikuwa wameuawa kwa umati. Zaidi ya Waislamu wengine milioni mbili pia walilazimika kuwa wakimbizi.

Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita, iliyosadifiana na tarehe 20 Farvardin 1385 Hijria Shamsia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilifanikiwa kupata teknolojia ya kurutubisha madini ya urani kwa ajili ya matumizi ya kiraia.
Wasomi na wataalamu wa Iran walifanikiwa kukamilisha mfumo wa kuzalisha nishati ya nyuklia licha ya mbinyo na vikwazo vya nchi za kibeberu. Kwa utaratibu huo Iran ikaingia katika orodha na kundi la nchi zenye teknolojia ya nyuklia duniani.
Mwaka mmoja baadaye Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kuzalisha nishati hiyo viwandani. Mafanikio hayo makubwa ya Iran yalipatikana chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Hata hivyo baadhi ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinapinga vikali miradi ya nishati ya nyuklia ya Iran kutokana na sera zao za kindumakuwili na za kibaguzi.
Siku hii inafahamika katika kalenda ya Iran kwa jina la "Siku ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia.
