Apr 24, 2025 03:31 UTC
  • Alkhamisi, Aprili 24, 2025

Leo ni Alkhamisi tarehe 25 Mfunguo Mosi Shawwal 1446 Hijria sawa na Aprili 24 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 1297 iliyopita Imam Ja'far Sadiq, mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw), aliuawa shahidi kwa amri ya mtawala dhalimu wa Kiabbasi, Mansur al Dawaniqi.

Imam Sadiq alizaliwa mwaka 83 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 31 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Muhammad Baqir. Imam Sadiq ambaye kipindi cha uongozi wake kilisadifiana na zama za mapigano makali kati ya watawala wa Kiumawi na Kiabbasi, alitumia fursa hiyo kueneza elimu na maarifa sahihi ya Kiislamu. Alifanikiwa kulea na kutayarisha wasomi hodari katika taaluma mbalimbali kama tiba, kemia, hesabati, nujumu hadithi na kadhalika. Jabiri bin Hayyan ambaye anatambuliwa hii leo kuwa ndiye baba wa elimu ya kemia alikuwa mwanafunzi wa Imam Ja'far Saqid (as).

Ushawishi wa Imam ulienea kwa kasi katika ulimwengu wa Kiislamu, jambo ambalo halikuwafurahisha watawala wa Kiabbasi. Hatimaye mtawala Mansur al Dawaniqi aliamuru Imam apewe sumu. Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa sumu hiyo katika siku kama ya leo na akazikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.

Siku kama ya leo miaka 1473 iliyopita kwa mujibu wa mahesabu ya wanahistoria wengi, iliasisiwa kwa mara ya kwanza taasisi ya kuandika na kutarjumu vitabu duniani hapa nchini Iran.

Uamuzi huo ulichukuliwa na Khosrow Anushirvan, mfalme wa Sasani nchini hapa. Taasisi hiyo ilijengwa sambamba na maktaba na vilikamilishwa kujengwa mwaka huo huo.

Vitabu tofauti vilikusanywa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia kwa ajili ya kutarjumiwa na mfalme huyo alimtuma daktari wake kwenda nchini India kwa ajili ya kukusanya vitabu kwa ajili ya shughuli hiyo.   

Katika siku kama ya leo miaka 754 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 April mwaka 1271, mtalii Marco Polo wa Venice alianza safari ya kihistoria ya kutembelea bara Asia.

Kabla yake baba na ami yake walitembelea China kupitia njia ya Asia Ndogo na Iran. Baada ya kurejea ndugu wa Polo kutoka Ulaya, Marco Polo akifuatana na baba yake kwa mara nyingine walielekea China na kutembelea ardhi ya nchi hiyo na visiwa vya kusini mshariki mwa Asia.

Baada ya kurejea nchini kwake, Marco Polo aliandika kumbukumbu ya safari iliyoitwa "Maajabu" kuhusiana na hali ya kijiografia ya ardhi za China, Turkemanistan, Mongolia na sehemu za kusini mashariki mwa Asia. Safari ya Marco Polo barani Asia ilichukua karibu miaka 20.   

Marco Polo

Tarehe 24 Aprili mwaka 1916 kulianza harakati ya tatu ya raia wa Ireland kwa ajili ya kujipatia uhuru wao kutoka kwa serikali ya Uingereza.

Harakati hiyo ilienda sambamba na kujiri kwa vita vikali vya kidini baina ya Waprotestanti na Wakatoliki. Vita hivyo vilimalizika kwa kufikiwa makubaliano baina ya David Lloyd George, Waziri Mkuu wa wakati huo wa Uingereza na kiongozi wa harakati ya raia wa Ireland waliokuwa wanataka kujitenga hapo mwaka 1922. 

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 24 April mwaka 1927 chanjo ya B.C.G iligunduliwa.

Chanjo hiyo iligunduliwa na madaktari wa kifaransa Albert Calmette na Guerin, baada ya kufanya uchunguzi wa miaka mingi. Chanjo ya B.C.G hutumika kukinga maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu au TB.

Kugunduliwa chanjo hiyo kumepunguza vifo vya watu wanaopatwa na ugonjwa wa TB duniani kote.   

Siku kama ya leo miaka 85 iliyopita, kwa mara ya kwanza kulianzishwa Idara ya Redio nchini Iran na kurushwa matangazo ya moja kwa moja. Awali kituo cha redio kilikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Posta, Simu na Telegrafu. Miaka mitano baada ya kuanzishwa kituo cha redio mjini Tehran, hatua kwa hatua huduma hiyo ilipanuliwa katika miji mbalimbali hapa nchini.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu 1979, zilianzishwa redio na televisheni kadhaa, zikiwemo zile za matangazo ya ng'ambo, zinazotangaza kwa lugha mbalimbali za kigeni ikiwemo Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyoanzishwa mwaka 1994.