Apr 27, 2025 02:23 UTC
  • Jumapili, 27 Aprili, 2025

Leo ni Jumapili 28 Mfunguo Mosi Shawwal 1446 Hijria sawa na 27 Aprili 2025 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 973 iliyopita alizaliwa Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran katika eneo la Ghaznin, moja ya miji ya kale ya Iran na ulioko katika Afghanistan ya sasa. Akiwa kijana mdogo alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusomea elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kusoma mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Sanā'ī Ghaznavi alianzisha mfumo wa aina yake katika usomaji wa mashairi. Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho kina muundo wa mashairi ambapo pia ndani yake ameweka wazi fikra za kiakhlaqi na irfani za malenga. Vitabu vya 'Ilahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq,' ni miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi. 

Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi,

 

Katika siku kama hii ya leo miaka 504 iliyopita, Ferdinand Magellan, baharia wa Kireno aliuawa na wenyeji wa Ufilipino kutokana na kuingilia mambo yao. Alizaliwa mwaka 1470 na kuanzia mwaka 1519 Miladia baharia huyo alianza safari yake kubwa ya baharini akiwa na meli tano. Ferdinand Magellan aligundua lango bahari huko kusini mwa bara la Amerika baada ya kuwasili katika pwani ya Amerika ya Latini. Lango bahari hilo limepewa jina la baharia huyo wa Kireno yaani Lango Bahari la Magellan. ***

Ferdinand Magellan

 

Miaka 65 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, nchi ya Togo inayopatikana huko katika pwani ya magharibi mwa Afrika ilipata uhuru. Wareno walikuwa watu wa kwanza kuikoloni Togo na nchi hiyo ilijulikana sana kwa jina la "Pwani ya Watumwa"  kwa kuwa nchi za Ulaya  zilikuwa zikiitumia nchi  hiyo kama kituo cha kusafirishia watumwa kuelekea Ulaya. Togo inapakana na nchi za Ghana na Benin na mji mkuu wake ni Lome. ***

 

Miaka 64 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Sierra Leone moja ya makoloni makongwe ya Uingereza magharibi mwa Afrika ilijipatia uhuru. Sierra Leone ilianza kukoloniwa na Ureno tangu karne ya 15 na nchi hiyo ilikuwa mojawapo ya vituo muhimu vya kuuzia watumwa waliokuwa wakipelekwa Ulaya. Uingereza ilianza kuikoloni Sierra Leone mwishoni mwa karne ya 18 hadi mwaka 1961 wakati nchi hiyo ilipopata uhuru. Baada ya uhuru, nchi hiyo ilikumbwa na mapinduzi na uasi mwingi. Kijiografia  Sierra Leone iko Magharibi mwa Afrika ikiwa na ukubwa wa kilomita mraba 71,000 na inapakana na Guinea na Liberia. ***

 

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita alifariki dunia Kwame Nkrumah, mwanasiasa mashuhuri wa Kiafrika na mpigania uhuru wa Ghana. Nkrumah alizaliwa mwaka 1909 na baada ya kupata shahada ya uzamivu nchini Marekani alianza kujishughulisha na masuala ya kisiasa. Baadaye Kwame Nkrumah aliasisi chama cha Kitaifa cha Watu wa Ghana na kuanza mapambano dhidi ya wakoloni wa Kiingereza. Mwaka 1951 alishiriki katika uchaguzi wa Bunge na kuwa Waziri Mkuu. Baada ya Ghana kupata uhuru mwaka 1960 Kwame Nkrumah alikuwa Rais wa nchi hiyo lakini Februari 24 mwaka 1966 aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi na wafuasi wa nchi za Magharibi akiwa safarini nchini Uchina. Baadaye alielekea Guinea ambako aliishi hadi kufariki dunia. Kwame Nkrumah anatambuliwa kuwa miongoni mwa wanamapambano mashuhuri wa Afrika waliofanya jitihada kubwa katika kupata uhuru na kujitawala nchi za bara hilo. ***

Kwame Nkrumah