Jumatatu, 12 Mei, 2025
Leo ni Jumatatu tarehe 14 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1446 Hijria sawa na tarehe 12 Mei 2025.
Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, alizaliwa Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko Florence nchini Italia.
Nightingale aliyejulikana kwa jina mashuhuri la 'mwanamke mwenye taa mkononi' alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya 'mwanamke mwenye taa mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku.
Alifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi nchini Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi bila kuchoka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba, alipofuka macho mwishoni mwa umri wake, na hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910.

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, Berlin mji mkuu wa Ujerumani iligawanywa katika sehemu mbili za Mashariki na Magharibi.
Kwa mujibu wa mapatano yaliyofikiwa baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia kati ya nchi nne zilizoikalia kwa mabavu Ujerumani, mji huo uligawanywa na kudhibitiwa na Russia, Ufaransa, Uingereza na Marekani. Muda mfupi baadaye mji huo ulizingirwa na Urusi ya zamani.
Harry Truman rais wa wakati huo wa Marekani alichukua uamuzi wa kuvunja mzingiro na udhibiti huo wa Urusi. Katika kutekeleza hatua hiyo Marekani ilikaribia kupigana vita na Urusi. Matokeo mengine ya mgogoro huo ilikuwa kugawanywa Ujerumani katika sehemu mbili za Ujerumani Magharibi na Mashariki. ***
Miaka 17 iliyopita, katika siku kama ya leo, tetemeko lenye ukubwa wa 7.9 kwa kipimo cha Rishta, liliukumba mji wa Sichuan ulioko kusini magharibi mwa China.
Katika tetemeko hilo la kutisha watu wapatao 87,000 walifariki dunia na wengine laki tatu na 80,000 kujeruhiwa. Tukio hilo la kutisha liliwaacha mamilioni ya watu bila makazi.

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, na kwa mujibu wa azimio nambari 278 la Umoja wa Mataifa nchi ya Bahrain ilijitenga na ardhi ya Iran.
Kabla ya kudhihiri Uislamu, nchi hiyo ndogo iliyo katika Ghuba ya Uajemi ilikuwa katika utawala wa Iran na baada ya kubuniwa utawala wa Kiislamu ikawa inadhibitiwa na makhalifa wa Kiislamu.
Mwanzoni mwa karne ya 7 Hijiria kwa mara nyingine tena nchi hiyo iliunganishwa na Iran na baada ya hapo ikawa chini ya himaya ya Uingereza. Licha ya hayo Iran iliendelea kudai udhibiti na utawala wake kwa Bahrain na kulalamikia vikali hatua ya Uingereza ya kuitawala nchi hiyo.
