Alkhamisi, tarehe 22 Mei, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 24 Dhulqaada 1446 Hijria sawa na Mei 22, mwaka 2025
Tarehe Mosi Khordad mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsiya ni siku ya kumuenzi Muḥammad Sadruddin Qawwam Shirazi maarufu kama Ṣadrul-Mutaallihīn na Mulla Sadra, mwanafalsafa na arif mkubwa wa Kiislamu.
Alizaliwa tarehe 9 Jamadil Ula mwaka 980 Hijria huko Shiraz. Awali alielekea Qazvin ambayo katika zama hizo ilikuwa mji mkuu wa utawala wa Safavi na kuhudhuria darsa na masomo kwa walimu wakubwa kama Sheikh Bahai.
Alisoma fiqhi, usul, Hadithi na hisabati kwa Sheikh Bahai na mantiki, falsafa na Irfan kwa Mirdamad. Mulla Sadra alipa elimu kama sayansi asilia, hisabati, nujumu na nyota kwa Hakim Abul Qasim Mir Fendereski, mmoja wa maulamaa wakubwa wa zama zake.
Mulla Sadra ametoa mchango mkubwa sana kwa falsafa ya Kiislamu. Mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu amevirithisha vizazi vya baada yake zaidi ya vitabu 40 na kitabu cha al Asfar al-arba‘a ndio maarufu zaidi. Mwanafasafa na mwanachuoni huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 1050 Hijria huko Basra nchini Iraq akiwa na umri wa miaka 70 na akazikwa katika mji huo huo.

Siku kama ya leo miaka 1246 iliyopita Imam Ali bin Musa Ridha (a.s) alianza safari yake kutoka Madina kuelekea Marv huko kaskazini mashariki mwa Iran ya zamani.
Imam Ridha (a.s) alifanya safari hiyo kwa kulazimishwa na kushinikizwa na Maamun, khalifa na mtawala wa saba wa ukoo wa Bani Abbas. Lengo la safari hiyo lilikuwa kumuweka Imam Ridha chini ya uangalizi. Maamun alitoa pendekezo kwa Imam huko Marv kwamba akubali kuwaa mrithi wake. Maamun alifanya hivyo ili kujionyesha kuwa ni mtu mwenye mapenzi na Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad (s.a.w).
Hata hivyo katika fursa mbalimbali Imam Ridha si tu kwamba alionyesha kuwa hakubali kushirikiana na utawala wa Bani Abbas, bali pia aliutambua utawala huo kuwa ni wa kupenda makuu na wa kidhalimu.

Siku kama ya leo miaka 166 iliyopita, alizaliwa Arthur Conan Doyle mwandishi wa Scotland.
Awali Doyle alisomea elimu ya tiba, hata hivyo kutokana na kwamba hakufaulu katika uga huo ndipo akaamua kujiunga na taaluma ya uandishi. Licha ya kwamba Doyle aliandika visa vingi lakini kilichompa umashuhuri ni majmui ya visa vya polisi vilivyoitwa Sherlock Holmes. Arthur Conan Doyle alifariki dunia mwaka 1930.

Siku kama ya leo miaka 140 iliyopita aliaga dunia Victor Hugo mwandishi na malenga mashuhuri wa Kifaransa akiwa na umri wa miaka 83.
Hugo alikuwa muungaji mkono mkuu wa mabadiliko kwa maslahi ya matabaka ya wanyonge na masikini nchini humo.
Victor Hugo alijitosa kwenye uwanja wa kisiasa akiwa na umri wa miaka 25 na kufanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge. Lakini ulipofika wakati wa utawala wa Napoleon wa Tatu alijiengua kwenye uwanja huo na kubaidishwa kwa muda wa miaka 20 baada ya kupinga siasa za dikteta Napoleon wa Tatu.
Miongoni mwa kazi maarufu za mwandishi huyu wa Kifaransa, tunaweza kutaja riwaya "Les Miserables", "Hunchback of Notre Dame", "The Man Who Laughs" na "Workers of the Sea".

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita yaani mwaka 1912 alizaliwa Herbert Charles Brown mwanakemia wa Uingereza.
Brown alizaliwa mwaka 1912 mjini London na familia yake ikahamia Marekani kabla ya hata kutimiza miaka miwili. Alijiunga na chuo kikuu cha Chicago mwaka 1935 na kusomea kozi ya Kemia na kuendelea na masomo hadi alipofanikiwa kuwa mhazili wa chuo kikuu.
Mwaka 1979 alitunukiwa tunzo ya Nobel katika taaluma ya kemia kutokana na jitihada alizofanya katika ugunduzi wa michanganyiko mipya ya kemia kaboni au Organic Chemistry. Herbert Charles Brown alifariki dunia mwaka 2004.

Miaka 45 iliyopita tarehe Mosi Khordad mwaka 1359 Hijria Shamsia ulianza mzingiro wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani ilipoteza maslahi yake haramu nchini Iran, hivyo iliweka mzingiro wa kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kwa lengo la kuwashinikiza wananchi Waislamu na wanamapambano wa Iran. Lengo la mzingiro huo wa kiuchumi lilikuwa kuulazimisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ukubali kuwa na uhusiano wa kawaida na Marekani.
Kufuatia uamuzi huo wa utawala wa Marekani, Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhurii ya Kiislamu, alitangaza bayana kuwa uhai wa kiuchumi wa mataifa hautegemei madola makubwa. Alilihutubia taifa la Iran akisema: "Msitishwe hata kidogo na mashinikizo hayo ya kiuchumi. Iwapo watatuwekea vikwazo vya kiuchumi vitatuhamasisha zaidi na kuwa na maslahi kwetu. Watu wanaotishwa na vikwazo vya kiuchumi ni wale wanaoona kuwa uchumi ndio msingi wa kila kitu na dunia kuwa ndio mwanzo na mwisho wao."

Siku kama hii ya leo miaka 39 iliyopita Omar Tilmisani mmoja wa viongozi wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya Misri aliaga dunia.
Alizaliwa mwaka 1904 katika eneo la Tilmisan nchini Algeria. Tilmisani alihitimu masomo yake ya shahada katika taaluma ya sheria na mwaka 1928 akawa mwanachama wa Ikhwanul Muslimin baada ya kuasisiwa harakati hiyo. Tilmisani ambaye alimpita kwa miaka miwili Hassan al Banna kiongozi wa harakati hiyo anahesabiwa kuwa mmoja wa makada wakongwe wa harakati hiyo. Hatimaye Omar Tilmisani aliaga dunia tarehe 22 Mei 1986 akiwa na umri wa miaka 82 baada ya kupatwa na maradhi ya ini na figo.
