Jumanne, tarehe 3 Juni, 2025
Leo ni Jumanne tarehe 07 Dhulhija 1446 Hijria sawa na tarehe 3 Juni 2025.
Katika siku kama ya leo, tarehe 7 Dhulhija miaka 1332 iliyopita, aliuawa shahidi Imam Muhammad Baqir AS, mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharifu katika kizazi chake.
Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama, na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya "Baqir", yaani mchimbua elimu.
Kipindi cha uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah, suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu.
Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa. Redio Tehran inatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote kwa mnasaba huu mchungu wa kuuliwa shahidi Imam Baqir (AS).

Siku kama ya leo miaka 523 iliyopita Vasco da Gama mwanabaharia wa Ureno alifanya mauaji ya umati na ya kinyama huko Calicut nchini India.
Calicut ambayo hii leo inajulikana kwa jina la Kozhikode ni bandari iliyoko Madras huko kusini mwa India. Hii ndiyo iliyokuwa sehemu ya kwanza kwa Vasco da Gama kutia nanga na kuiteka katika safari yake ya kuelekea India mwaka 1498.
Kama walivyokuwa wakoloni wenzake, da Gama alijitambua kuwa ndiye mmiliki halisi wa India. Wakati wafanyabiashara 800 wa Kiarabu walipofika katika eneo hilo kwa lengo la kufanya biashara ya mchele, Vasco da Gama alitoa amri wafanyabiashara hao wakatwe mikono, masikio na pua na kisha wauawe kwa umati baada ya kuteketeza meli zao.

Miaka 358 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya elimu ya tiba na upasuaji, ilifanyika kazi ya kuhamishia damu kwenye mwili wa mwanadamu.
Kazi hiyo ilifanywa na tabibu wa Kifaransa aliyejulikana kwa jina la Jean Baptiste Denis. Kuigizwa damu kwenye miili yawagonjwa kulizusha mageuzi makubwa katika elimu ya tiba kwani hadi kipindi hicho wagonjwa wengi walikuwa wakifariki dunia kutokana na kuvuja damu kwa wingi au kwa upungufu wa damu.
Katika utafiti wake wa kwanza tabibu huyo Mfaransa alitia damu ya mbuzi ndani ya mwili wa mwanadamu lakini baadaye alifanikiwa kuweka damu ya mwanadamu katika mwili wa mwanadamu mwingine.

Siku kama ya leo miaka 168 iliyopita alizaliwa, Jacques de Morgan, mtaalamu wa historia ya maumbile na mwanasayansi wa masuala ya ardhi wa nchini Ufaransa.
Awali alisafiri nchi tofauti kwa ajili ya kuvumbua madini mbalimbali ambapo kwa muda fulani alijishughulisha pia na uvumbuzi wa masuala ya historia nchini Misri. Tangu mwaka 1889 Miladia na kwa muda wa miaka mitatu Morgan alifanya utafiti kuhusiana na masuala ya kale nchini Iran huku akiandika vitabu katika uwanja huo. Kuanzia mwaka 1889 na kuendelea kwa miaka 15 baadaye alikuwa msimamizi wa kamisheni ya masuala ya kihistoria nchini Ufaransa ambapo aliendeleza utafiti wake katika maeneo mbalimbali ya dunia.
Jacques de Morgan alifariki dunia mwaka 1924. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na kitabu cha 'Mwanadamu Kabla ya Historia' 'Operesheni ya Kielimu Mjini Paris' na 'Utangulizi wa Historia ya Mashariki.'

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita Imam Khomeini (M.A), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitoa hotuba kali ya kihistoria dhidi ya utawala wa kitwaguti wa Iran, kwa mnasaba wa Ashura ya Imam Husseini (A.S).
Imam Khomeini alitoa hotuba hiyo mbele ya hadhara kubwa ya wananchi na wanazuoni katika Madrasa ya Faidhiya katika mji mtakatifu wa Qum hapa nchini, licha ya vizuizi na vitisho vya utawala wa Shah. Imam alikosoa vikali usaliti wa utawala wa Shah na vibaraka wake dhidi ya wananchi Waislamu wa Iran. Katika sehemu moja ya hotuba hiyo Imam Khomeini ilisema: "Watu hawa wanapinga Uislamu na wanazuoni na wana nia ya kuitokomeza dini hii.
Enyi wananchi, dini yetu ya Uislamu na nchi yetu viko hatarini na tuna wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Iran." Mwisho wa kunukuu.

Na miaka 9 iliyopita katika siku kama hii ya leo gwiji wa uzani wa juu wa ndondi duniani, Muhammad Ali Clay aliaga dunia.
Muhammad Ali ambaye jila lake la awali lilikuwa Cassius Marcellus Clay anatambuliwa kuwa miongoni mwa wanamasumbwi mashuhuri na wakubwa zaidi duuniani. Baada ya kukubali dini tukufu ya Uislamu, Muhammad Ali Clay alijihusisha pia na harakati za kisiasa nchini Marekani na aliwahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 5 jela kutokana na misimamo yake ya kisiasa.
Muhammad Ali aliaga dunia tarehe 3 Juni mwaka 2016 baada ya kusumbuliwa na maradhi ya Parkinson's kwa miaka mingi.
