Jun 05, 2025 02:11 UTC
  • Alkhamisi, 5 Juni, 2025

Leo ni Alkhamisi 9 Mfunguo Tatu Dhulhija 1446 Hijria mwafaka na 5 Juni 2025.

Leo ni siku ya Arafa tarehe 9 Dhilhija.

Arafa ni jina la jangwa kubwa linalopakana na mlima Jabalur Rahma ulioko kusini mashariki mwa Makka. Tangu adhuhuri ya siku hii mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, husimama katika uwanja wa Arafa na hadithi nyingine za Kiislamu zimetaja fadhila na utukufu mkubwa wa kisimamo hicho.

Hadithi zinasema kuwa Mwenyezi Mungu SW ameifanya ardhi ya Arafa ambayo ilikuwa medani ya matukio mengi muhimu ya kihistoria, kuwa mahala pa kuwapokea wageni wake wanaokwenda Hija na ameweka meza na karamu yake pembeni ya mlima wa Jabalur Rahma.

Ni vyema kukumbusha kuwa magharibi ya siku hii ya leo mahujaji wanaondoka uwanja wa Arafa na kuelekea Mash'arul Haram na kujitayarisha kwa ajili na amali nyingine za Hija. 

Siku kama ya leo miaka 1386 iliyopita, Muslim bin Aqil binamu wa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS aliuawa shahidi mjini Kufa Iraq.

Alikuwa mmoja wa shakhsia wakubwa na wacha Mungu katika zama zake. Alielekea Kufa, Iraq akiwa na lengo la kwenda kutathmini ni kwa kiwango gani watu wa mji huo walikuwa wakimtii Imam Hussen, baada ya watu wa mji huo kumwandikia maelfu ya barua Imam huyo wakimtaka aende mjini humo na kwamba wako tayari kumuunga mkono katika harakati yake dhidi utawala dhalimu wa Yazid bin Muawiya.

Watu wa Kufa walimsaliti Muslim bin Aqil baada ya kuhadaika kwa hila na uongo wa Ubeidullah bin Ziyad, mtawala wa wakati huo wa Kufa na wakamuacha Muslim bin Aqiil peke yake.   

Mahali lilipo kaburi la Muslim bin Aqil, Kufa

Katika siku kama ya leo miaka 242 iliyopita baluni lilirushwa angani kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya jitihada za mwanadamu za kutaka kupaa angani.

Baluni hilo lilikuwa na watu wawili, mmoja wao akiwa ni mwanafizikia wa Kifaransa aliyejulikana kwa jina la Jean-Francois Pilatre de Rozier. Tangu alipokuwa shuleni de Rozier alikuwa akifikiria jinsi ya kutengeneza chombo cha kupaa angani na hatimaye baada ya kutengeneza baluni, naye pia alitengeneza baluni lake na akapaa angani nalo katika siku kama hii ya leo.

Mwanafizikia huyo alianguka chini na kufariki dunia katika moja ya safari zake za uhakiki angani.

Miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo yalianzishwa mapambano ya wapigania ukombozi Wairani yaliyoongozwa na Mirza Kuchak Khan Jangali dhidi ya utawala wa kiimla na uliokuwa dhalili wa Qajar na dhidi ya uporaji wa utajiri wa Iran uliokuwa ukifanywa na mkoloni Muingereza; ambapo siku iliyofuata yaani tarehe 6 Juni Mirza Kuchak Khan alitangaza "serikali ya muda ya Jamhuri".

Kazi ya kuratibu harakati ya mapambano hayo ilitekelezwa na Kamati ya Umoja wa Uislamu iliyoundwa kwa ilhamu aliyopata katika fikra za wanafikra na warekebishaji umma kama Sayyid Jamaluddin Asad Abadi, Sayyid Abdurahman Kawakibi na Sheikh Muhammad Abdou; lengo likiwa ni kuleta umoja baina ya nchi za Kiislamu kwa madhumuni ya kupambana na watawala madikteta na ushawishi wa maajinabia.

Kwa mtazamo wa Mirza Kuchak Khan hali ya Iran ilikuwa ya tafrani; na nchi ilikuwa imedhibitiwa na maajinabia. Kwa kufuata mielekeo ya umoja wa Uislamu alidhamiria kuunda vuguvugu la kijeshi kwa ajili ya kupambana na udikteta wa ndani na ukoloni wa nje ili kuiokoa Iran. Licha ya mapambano yaliyoendeshwa na Mirza Kuchak Khan na wafuasi wake, baadhi ya waungaji mkono wa utawala wa kikomunsti wa Urusi waliokuwemo kwenye safu za wafuasi wake waliifanyia uhaini na usaliti harakati yake.

Hatimaye tofauti za baina ya viongozi na njama za wakoloni wa nje ziliivuruga harakati ya Mirza Kuchak Khan na pigo la mwisho lililoizima harakati hiyo lilikuwa ni la kuuliwa Mirza mwenyewe na utawala wa Reza Khan Pahlavi.

Mirza Kuchak Khan

Miaka 78 iliyopita, yaani tarehe Juni 1947 George Marshall, waziri wa mambo ya nje wa wakati huo wa Marekani alitangaza mpango wa utoaji mkopo wa dola bilioni tano wa kuzisaidia nchi kadhaa za Ulaya Magharibi zilizokuwa zimeathiriwa na vita.

Lengo la mpango huo uliokuwa maarufu kama "Mpango wa Marshall" lilikuwa ni kuzikarabati na kuzijenga upya nchi wafuasi wa Marekani, kufutilia mbali uwezekano wa kujitokeza mielekeo ya Ukomunisti katika nchi hizo; na muhimu zaidi kuliko yote kupanua satua ya kiuchumi na kuhodhiwa Ulaya kisiasa na Marekani.

Mkopo huo wa Marekani uliopambwa na nguvu za kijeshi na kipropaganda za serikali ya Washington, uliibadilisha nchi hiyo; na kwa muda mrefu baadaye ikaja ikawa moja ya madola mawili makuu yenye nguvu duniani sambamba na Urusi.

George Marshall

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, wananchi Waislamu wa Iran baada ya kupata habari kwamba Imam Khomeini (MA) alikuwa amekamatwa na utawala dhalimu wa Shah, walifanya maandamano makubwa kote nchini dhidi ya utawala huo.

Siku kadhaa nyuma, Imam alikuwa ametoa hotuba kali katika Chuo cha Kidini cha Faidhiyya akifichua maovu yaliyokuwa yakifanywa na utawala wa Shah, jambo lililouchukiza sana utawala huo na kuamua kumtia nguvuni, Imam. Suala hilo liliwakasirisha sana wananchi wa Iran ambao waliamua kufanya maandamano ya kushinikiza kuachiliwa kwake mara moja. Ili kukabiliana na wimbi la malalamiko hayo, utawala wa Shah uliamua kuwashambulia waandamanaji na kkuua na kujeruhi wengi kati yao.

Harakati hiyo ya mapambano ambayo inafahamika hapa nchini kama Mapambano ya Tarehe 15 Khordad, kwa hakika ulikuwa mwanzo wa mapambano ya Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi shupavu wa Iran dhidi ya utawala wa kitaghuti wa Shah, mapambano ambayo yaliainisha mustakbali wa kisiasa na kijamii wa Iran. Mapambano hayo yaliendelea kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi hapo mwaka 1979. 

Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, vita vya tatu vikuu kati ya utawala ghasibu wa Israel na nchi za Kiarabu vilianza.

Katika uvamizi wa kushtukiza na wa ghafla, ndege za kivita za Israel ziliingia katika anga ya nchi za Misri, Syria na Jordan na kushambulia kwa muda wa masaa mawili mfululizo majeshi na taasisi za anga za nchi hizo na kukaribia kuvitokomeza kabisa. 

Baada ya hapo jeshi la nchi kavu la Israel lililokuwa likiungwa mkono na Marekani pamoja na Uingereza, kwa muda wa siku sita, lilivamia kwa silaha nzitonzito na za kisasa majeshi ya nchi tatu zilizotajwa za Kiarabu na kuyashinda kabisa. 

Miaka 21 iliyopita katika siku kama hii ya leo Ronald Reagan, rais wa zamani wa Marekani aliaga dunia kutokana na ugonjwa wa kusahau wa Alzheimer.

Alizaliwa mwaka 1911 na kuhitimu masomo yake ya juu katika taaluma ya uchumi na masuala ya kijamii. Reagan alianza kufanya kazi kwenye redio na kisha akawa msanii kwenye televisheni. Taratibu alianza kujishughulisha na masuala ya siasa ambapo kwanza alikuwa mwanachama wa chama cha Democrats na kisha kujiunga na chama cha Republicans.

Mwaka 1970 aliteuliwa na chama hicho kuwa gavana wa California na kisha mwaka 1980 akafanikiwa kuwa rais wa Marekani baada ya kumshinda mpinzani wake Jimmy Carter.

Katika kipindi cha uongozi wake wa miaka minane Reagan alitekeleza siasa za kijeshi na kichokozi dhidi ya nchi nyingine za dunia. Alianzisha mpango wa kijeshi wa Star Wars na kutoa amri ya kufanyika mashambulio ya kijeshi dhidi ya baadhi ya nchi. Pia alichochea na kuunga mkono kijeshi, kifedha, kipropaganda na kisiasa uvamizi wa utawala wa kidekteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ronald Reagan