Jumapili, 08 Juni, 2025
Leo ni Jumapili 12 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1446 Hijria sawa na 8 Juni 2025 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 973 iliyopita alizaliwa Hakim Abul-Majd Majdūd ibn Ādam Sanā'ī Ghaznavi, malenga, tabibu na mwanairfani mkubwa wa Iran. Akiwa kijana mdogo alianza kusoma mashairi ya kuwasifu watawala. Hata hivyo muda mfupi baadaye aliachana na mwenendo huo na kuanza kusoma elimu ya irfan (ya kumjua Mwenyezi Mungu). Kuanzia wakati huo alianza kuishi maisha ya kuwatumikia wananchi sambamba na kutunga mashairi ya kuwakosoa watawala dhalimu na mafisadi. Alianzisha pia mfumo wa aina yake katika tungaji wa mashairi. Miongoni mwa athari za Sanai Ghaznawi ni pamoja na kitabu cha 'Hadiqatul-Haqiqah' ambacho ndani yake ameeleza wazi fikra zakke za kiakhlaqi na irfani. Vitabu vingine mashuhuri vya malenga huyo ni 'Ilahi Nameh' 'Karnameh Balkh' na 'Twariqut-Tahqiq".

Miaka 506 iliyopita na katika siku kama ya leo yaani tarehe 12 Dhul-Hijja mwaka 940 Hijria, aliaga dunia Ali bin Hassan Karaki Amili mmoja wa mafakihi wakubwa wa Kiislamu. Alipata elimu ya msingi katika eneo alikozaliwa la Jabal Amil nchini Lebanon. Akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu, Ali bin Hassan Karaki alifanya safari katika nchi kdhaa za Kiislamu. Mhakiki Karaki kama anavyojulikana zaidi, ameacha athari nyingi za vitabu zenye thamani kubwa. Jamiul Maqaasid na Risatul Adalah ni baadhi ya vitabu mashuhuri vya msomi huyo.

Siku kama ya leo miaka 195 iliyopita inayosadiafiana na tarehe 8 Juni 1830, Camberz mbunifu wa Kijerumani alivumbua utengenezaji wa kiberiti. Tofauti kubwa ya kiberiti hicho cha awali na hiki kinachotumiwa hivi sasa, ni uwakaji wake uliokuwa wa taratibu. Baada ya Camberz walijitokeza watafiti wengine kadhaa waliofanya utafiti wao kuhusiana na kiberiti, na hatimaye Phillips raia wa Kimarekani alifanikiwa kutengeneza kiberiti kama hiki ambacho kinatumika leo hii. ***

Tarehe 8 Juni miaka 170 iliyopita, Lisbon mji mkuu wa Ureno uliharibika kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi na moto uliosababishwa na zilzala hiyo. Karibu wakazi arubaini elfu (40,000) wa mji huo walipoteza maisha yao na thuluthi mbili ya nyumba na taasisi za kiuchumi za mji huo zilibomolewa. Mbali na maafa hayo, karibu meli elfu mbili, boti na ngarawa (ngalawa) nyingi zilizokuwa katika bandari za Ureno zilizama. Mtetemeko huo ni moja ya mitetemeko mikubwa zaidi ya ardhi kuwahi kuikumba Ureno.
Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, shirika la kijasusi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Mossad, lilifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya kiongozi mwingine wa Kipalestina katika moja ya nchi za kigeni. Siku hiyo maajenti wa Mossad walimuuwa Atef Bseiso mmoja wa viongozi wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO huko Paris, Ufaransa. Licha ya kwamba hakukuwepo shaka juu ya kuhusika utawala wa Kizayuni katika mauaji hayo, lakini utawala huo ghasibu ulikana kufanya jinai hiyo ya kinyama kwa kuhofia hasira za walimwengu. Hata hivyo miaka saba baadaye, polisi ya Ufaransa ilitangaza kwamba shirika hilo la ujasusi la Israel Mossad ndilo lililopanga na kutekeleza mauaji hayo. ***
