Jun 11, 2025 02:10 UTC
  • Jumatano, Juni 11, 2025

Leo ni Jumatano 15 Mfunguo Tatu Dhulhija 1446 Hijria mwafaka na 11 Juni 2025 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1231 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Ali Naqi (AS) mashuhuri kwa lakabu ya al-Hadi, mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW, katika mji mtakatifu wa Madina.

Baada ya kuuawa shahidi baba yake, yaani Imam Jawad AS, Imam Hadi alichukua jukumu zito la Uimamu na kuongoza Umma wa Kiislamu.

Zama za Uimamu wake zilisadifiana na kipindi cha utawala wa ukoo wa Bani Abbas, na Mutawakkil ndiye aliyekuwa ameshika hatamu za uongozi wakati huo.

Baada ya mtawala huyo kuhisi kuwa Imam Hadi (as) na wafuasi wake walikuwa hatari kwa utawala wake, aliamrisha Imam atolewe Madina na kuhamishiwa Samarra, Iraq ili amuweke chini ya uangalizi. Licha ya hayo yote, lakini Imam Naqi aliendelea kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 453 iliyopita sawa na tarehe 11 Juni mwaka 1572, alizaliwa Benjamin Jonson (Ben Johnson) mshairi na mwandishi wa filamu wa Uingereza.

Jonson kwa muda mrefu alikuwa mcheza tamthilia na rafiki wa Shakespare mwandishi maarufu wa Uingereza, ambapo urafiki wao ulikuwa na athari kubwa katika kukamilisha fasihi ya mshairi huyo.

Baadhi ya athari zilizoachwa na Benjamin Jonson ni Mwanamke Aliyezimwa' pamoja na Historia ya Dunia. Malenga huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1637.

Ben Johnson

Siku kama ya leo miaka 170 iliyopita inayosadifiana na tarehe 11 Juni mwaka 1855, mwanga wa jua ulitambuliwa kwa kutumiwa njia za taaluma ya uchanganuzi na wigo wa rangi.

Jaribio hilo lilifanywa kwa mara ya kwanza katika historia ya utafiti mpya wa fizikia na wanasayansi wawili wa Ujerumani walioitwa Kirchhoff na Bunsen.

Si vibaya kuashiria hapa kwamba, mionzi ya jua katika hewa wakati wa mvua pamoja na kutokea upinde wa mvua wenye rangi mbalimbali, ni tukio la kuvutia ambalo linasababishwa na kuchanganuliwa nuru ya jua na matone ya maji mawinguni. Hata hivyo suala hilo mwanzoni lilifafanuliwa na wanasayansi wa Kiislamu kama vile Ibn Sina, Ibn Haitham na Qutbuddin Shirazi na baadaye kuthibitishwa na Kirchhoff na Bunsen.

Miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Khordad mwaka 1353 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, alifariki dunia Daktari  Muhammad Khazaeli, mwasisi wa Tasisi ya Kuongoza na Kuwasaidia Vipofu ya Iran.

Khazaeli alipokuwa mtoto alipoteza nguvu ya kuona kutokana na ugonjwa wa ndui, na alipata elimu katika shule maalumu ya vipofu. Dakta huyo kwa kutumia uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi mambo, alipata mafanikio makubwa katika masomo yake na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamilifu ya sheria katika Chuo Kikuu cha Tehran.

Dakta Khazaeli alifahamu vyema lugha ya Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza na aliandika na kutafsiri vitabu mbalimbali.

Miongoni mwa masuala aliyojishughulisha nayo ni kupigania kupatiwa huduma muhimu vipofu katika uga wa kimataifa na alikuwa pia mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mashariki ya Kati katika Baraza la kitaifa la kuwahudumia vipofu na Jumuiya ya Kimataifa ya Vipofu. 

Dakta Khazaeli