Jul 25, 2025 02:53 UTC
  • Ijumaa, tarehe 25 Julai, 2025

Leo ni Ijumaa tarehe 29 Mfunguo Nne Muharram 1447 Hjria sawa na Julai 25 mwaka 2025.

Siku kama ya leo miaka 544 iliyopita alifariki dunia mwanahistoria wa Kiislamu, Muhammad Heravi, katika mji wa Herat nchini Afghanistan.

Heravi alizaliwa katika familia mashuhuri kwenye mji wa Balkh huko kaskazini mwa Afghanistan ingawa aliishi kipindi kirefu katika mji wa Herat. Muhammad Haravi aliheshimiwa mno na waziri msomi wa utawala wa kizazi cha Gurkanian, Amir Alishah Navai, ambaye alikuwa akiwaenzi na kuwaheshimu mno wasomi na wanazuoni. 

Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwanahistoria huyo wa Kiislamu ni kile cha "Tarikh Raudhatu Safa" ambacho kinazungumzia historia ya dunia nzima tangu kuumbwa kwake hadi kipindi cha msomi huyo. *

Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita, vita kati ya Uchina na Japan vilianza kwa mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la Japan dhidi ya maeneo ya pwani ya Uchina.

Vita hivyo vilitokea baada ya mashambulio yaliyofanywa na Japan kwa lengo la kuiteka ardhi kubwa ya Peninsula ya Korea na kaskazini mwa China.

Japan ndiyo iliyoshinda katika vita hivyo kutokana na kujizatiti vyema kwa silaha za kisasa. 

Katika siku kama ya leo miaka 87 iliyopita, Wapalestina 62 wasio na hatia  waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika milipuko miwili ya mabomu iliyotokea kwa nyakati tofauti katika soko la kuuzia mboga za majani huko Palestina.

Makundi ya kigaidi ya Wazayuni ndiyo yaliyotega mabomu hayo mawili na lengo lao lilikuwa kuzusha hali ya machafuko na ukosefu wa amani kwa Wapalestina.   

Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo mnamo tarehe 3 mwezi Mordad mwaka 1361 Hijria Shamsiya, alifariki dunia Dakta Hamid Inayat, mwandishi na mtarjumi mahiri wa Kiirani.

Dakta Hamid alielekea nchini Uingereza baada ya kupata shahada ya chuo kikuu nchini Iran na akiwa huko alihitimu shahada ya udaktari katika taaluma ya uchumi na sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha London. Dakta Hamid Inayat baadaye alirudi Iran na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran.

Dakta Inayat ameandika na kutarjumu vitabu vingi vya falsafa na fikra za kisiasa. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni Uislamu na Usoshalisti na Fikra za Kisiasa za Magharibi. 

Hamid Inayat

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi makubwa ya anga na baharini huko kusini mwa Lebanon.

Mashambulizi hayo yalikuwa operesheni kali zaidi ya kijeshi kuwahi kufanywa na Wazayuni dhidi ya Lebanon baada ya mashambulio waliyoyafanya dhidi ya ardhi nzima ya Lebanon mwaka 1982.