Jan 11, 2026 02:30 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumapili 21 ya mwezi Rajab 1447 kwa kalenda ya Kiislamu, sawa na 11 Januari 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1199 iliyopita mwezi wa Rajab mwaka 284 Hijiria, alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu, Abu Hatam, Sahal bin Muhammad Sajestani. Abu Hatam alikuwa ametabahari katika elimu ya Qur'ani, Hadithi, fasihi na mashairi. Mbali na kuwa alikuwa akiisoma Qur'ani Tukufu na kuifundisha kwa mapenzi makubwa, Abu Hatam pia alijishughulisha na masuala ya kijamii. Msomi huyo ameacha vitabu vingi, miongoni mwavyo ni I'irabul Qur'an', na Akhlaqul Insan.

 

Siku kama ya leo miaka 701 iliyopita mji wa Mexico ambao hivi sasa ni mji mkuu wa nchi ya Mexico, uliasisiwa na mmoja wa wafalme wa silsila ya Aztec. Waaztec walikuwa miongoni mwa makabila ya Wahindi Wekundu wa Amerika ya Latini ambao waliwasili huko Mexico katika karne ya 12 na kutawala eneo hilo mwanzoni mwa karne hiyo.

 

Siku kama ya leo miaka 148 iliyopita alizaliwa Ayatullah Sadruddin Sadr, mmoja wa maulama wakubwa wa ulimwengu wa Kiislamu kkatika mji wa Kadhimiyya, Iraq. Alipata kusoma alimu ya msingi katika mji aliozaliwa na baada ya hapo akasoma elimu ya fasihi na hisabati huku akijiunga na hauza ya elimu ya mjini Najaf na kufikia daraja ya ijtihadi. Akiwa na umri wa miaka 32 alielekea mjini Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran ambapo alisalia mjini hapo hadi mwaka 1348 Hijiria, ambapo alielekea nchini Iraq. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Mukhtasar Taarikhul-Islami.' 

 

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita aliaga dunia Ustadh Abulqassim Sahab, mmoja wa wasomi wakubwa wa elimu ya jiografia na mtafiti mashuhuri wa Kiirani. Alizaliwa mwaka 1266 Hijria Shamsiya katika mji wa Tafresh nchini Iran. Abulqassim Sahab alijifunza fiqih na usul kwa maulamaa wa mji huo na mbali na kupata elimu hiyo alizungumza pia lugha za Kiingereza na Kijerumani.  

 

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita sawa na tarehe 11 Januari mwaka 1992, Rais Shazli bin Jadid wa Algeria alijiuzulu baada ya Harakati ya Uokovu wa Kiislamu ya Algeria (FIS) kupata mafanikio makubwa katika uga wa kisiasa na matukio ya baadaye nchini humo. Rais Shazli alichaguliwa kuwa rais wa Algeria mwaka 1979 baada ya kifo cha Houari Boumediene, rais wa zamani wa nchi hiyo. Mwaka 1988 Shazli bin Jadid aliahidi kutekeleza marekebisho na kufanya mabadiliko ya katiba ya Algeria, ambapo kwa mujibu wake suala hilo lingetoa mwanya wa kutambuliwa rasmi vyama vya kisiasa.

 

Miaka 14 iliyopita katika siku kama hii ya leo msomi wa nyuklia wa Iran, Mustafa Ahmadi Roshan aliuawa shahidi na maajenti wa utawala haramu wa Israel. Ahmadi Roshan alikuwa msomi wa nne wa nyuklia wa Iran kuuawa na magaidi wa Israel na washirika wake. Mbali na kujishughulisha na masuala ya nyuklia msomi huyo alifanya utafiti mkubwa katika masuala ya elimu na sayansi. Ahmadi Roshani aliuawa yeye na dereva wake mjini Tehran akiwa njiani kueleka kazini kwake. Siku kadhaa baadaye genge la magaidi waliomuua msomi huyo wa nyuklia wa Iran na wenzake lilitiwa nguvuni na wanachama wake wakakiri kuwa wana uhusiano na utawala haramu wa Israel na kwamba walipewa mafunzo na maajenti wa utawala huo haramu kwa ajili ya kuwaua kigaidi wasomi wa nyuklia wa Iran.