Jumatatu, 25 Mei, 2026
Leo ni Jumatatu tarehe 8 Mfunguo Tatu Dhulhija 1447 Hijria, mwafaka na 25 Mei 2026.
Leo tarehe 8 Dhulhija ni siku ya Tarwiya.
Siku hii imepewa jina la siku ya Tarwiya kwa maana ya kijitosheleza kwa maji kwa sababu katika zama za Nabii Ibrahim (as) maji hayakuwa yakipatikana katika jangwa na Arafat na kwa msingi huo watu walikuwa wakipeleka maji eneo la Arafat kutoka Makka tarehe 8 Dhulhija wakijitayarisha kwa ajili ya mahitaji ya maji ya kesho yake yaani tarehe tisa Dhilihija. ***
Katika siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Imam Hussein bin Ali (AS), mjukuu wa Mtume Muhammad SAW aliondoka Makka na kuelekea Kufa nchini Iraq baada ya kukataa kumbai na kutoa kiapo cha utiifu kwa Yazid bin Muawiya.
Miezi minne kabla ya hapo, Imam Hussein alikuwa amewasili mjini Makka akiwa pamoja na familia yake na alikitumia kipindi cha kuweko waumini waliotoka pembe mbalimbali za dunia kwa ajili ya kufanya ziara katika Nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu, kuwaamsha na kuwabainishia dhulma na ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanywa wa utawala wa Yazid mwana wa Muawiya.
Wakati huo huo kutokana na wito wa mara kwa mara wa watu wa Kufa na njama za utawala wa Yazidi za kutaka kumuuwa, Imam Hussein aliondoka Makka na kueleka Kufa. ***
Tarehe 4 Khordad kwa mujibu wa kalenda ya Iran ya Hijria Shamsia imepewa jina la Siku ya Kusimama Kidete Dezful, ambao ni moja ya miji ya kusini mwa Iran.
Sababu ya siku hii kupewa jina hilo ni muqawama na ungangari wa watu wa Dezful kukabiliana na hujuma na mashambulio ya makombora ya utawala wa Kibaathi wa Iraq wakati wa vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Wakati vilipoanza vita hivyo vya Kujihami Kutakatifu, mji wa Dezful ulishambuliwa kwa makombora zaidi ya 200 na kwa risasi zaidi ya elfu ishirini mpaka ukajulikana kwa jina la mji wa makombora.
Pamoja na yote hayo wananchi katika mji wa Dezful waliendelea kuonyesha muqawama na uhimilivu kiasi kwamba hata katika mazingira hayo Sala ya Ijumaa iliendelea kusaliwa kila wiki kwa kuhudhuriwa na wananchi na wapiganaji waliokuwa kwenye medani za vita. ***
Siku kama ya leo, miaka 666 iliyopita, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1360 kundi la mabaharia wa Kifraransa lilidai kugundua Ghuba ya Guinea.
Ghuba ya Guinea iko magharaibi mwa bara la Afrika katika bahari ya Atlantiki. Baada ya muda kupita tangu kugunduliwa Ghuba ya Guinea, ushawishi wa Ufaransa ndani ya bara hilo ulianza, na taratibu ikaanza kuidhibiti ardhi iliyokuja kujulikana baadaye kama Guinea. Nchi ya Guinea ilianzisha harakati za mapambano ya miaka mingi mpaka ikafanikiwa kupata uhuru wake mwaka 1958.
Guinea ina eneo lenye ukubwa wa kilomitamraba zaidi 245,000 na imepakana na nchi za Senegal, Guinea Bissau, Mali, Ivory Coast, Liberia na Sierra Leone. ***
Miaka 105 iliyopita katika siku kama ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, Sayyid Ziauddin Tabatabai aliondolewa katika wadhifa wa Waziri Mkuu kwa amri ya Ahmad Shah Qajar.
Ziauddin alishiriki katika mapinduzi ya Reza Khan ya 1299 Hijria Shamsia kwa himaya ya Uingereza. Katika siku za kwanza za kuwasili kwa vikosi vya Kazakh mjini Tehran, Sayyid Ziauddin alikutana na Ahmad Shah na akapokea agizo la kuwa Waziri Mkuu akiwa na mamlaka kamili. Katika siku ya kwanza ya uongozi wake, alichukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwakamata takriban viongozi mia mbili wa nchi na wanazuoni.
Kuporomoka kwa serikali ya Sayyid Ziauddin Tabatabai, kunakojulikana kama Serikali ya nyeusi na Baraza la Mawaziri la Siku Mia, kunapaswa kutambuliwa katika kutofautiana kwake na kamanda mkuu wa majeshi. ****
Miaka 63 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 25 Mei mwaka 1963, Hati ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) ilisainiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 32 za bara hilo.
Marais Gamal Abdel Nasser wa Misri, Kwame Nkrumah wa Ghana na Ahmed Sekou Toure wa Guinea walikuwa miongoni mwa waasisi wa jumuiya hiyo. Jumuiya ya OAU ilielekeza jitihada zake katika kuleta umoja kati ya nchi za Afrika, kutatua hitilafu kati ya nchi hizo, kutetea haki ya kujitawala ya nchi wanachama na ukombozi wa nchi nyingine za Kiafrika zilizokuwa zingali zinakoloniwa.
Mnamo mwezi Julai mwaka 2002, viongozi wa nchi wanachama wa OAU walifanya kikao nchini Afrika Kusini na kuamua kubadilisha jina la jumuiya hiyo kutoka Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) na kuwa Umoja wa Afrika (AU) sambamba na kuanzisha taasisi kadhaa kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya umoja huo na kustawisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama.
Hivi sasa Umoja wa Afrika una nchi 54 wanachama. Makao Makuu ya umoja huo yako Addis Ababa, Ethiopia na kikao cha viongozi wa nchi wanachama hufanyika kila mwaka katika moja ya nchi hizo. ***