Aug 30, 2016 04:27 UTC
  • Jumanne, Agosti 30, 2016

Leo ni Jumanne tarehe 27 Dhulqaada 1437 Hijria sawa na tarehe 30 Agosti 2016.

Siku kama ya leo mwaka mmoja uliopita yaani tarehe 27 Dhulqaada 1436 Hijria winchi lililokuwa limewekwa katika eneo la mashariki ndani ya Msikiti mtakatifu wa Makka lilianguka na kuua idadi kubwa ya mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu. Katika tukio hilo lililotokea saa 17.1 kwa wakati wa Makka, mahujaji 107 waliuawa na wengine 238 walijeruhiwa. Mahujaji wengi waliopoteza maisha katika tukio hilo ni kutoka nchi za India, Pakistan, Indonesia na Iran. Serikali ya Saudi Arabia ilitangaza kuwa sababu ya kuanguka winchi hiyo ni upepo na tufani kali iliyovuma mjini Makka.

Tukio hilo lililodhiohirisha uzembe wa serikali ya Saudia na la lile la maafa ya Mina katika siku ya Idi Kubwa mwaka huo huo ni miongoni mwa matukio machungu zaidi katika historia ya ibada ya Hija. Maelfu ya Waislamu walifariki dunia katika maafa ya Mina wakati wa kuelekea kwenye eneo la kumpiga mawe shetani.

Tarehe 30 Agosti miaka 17 iliyopita, wananchi wa Timor ya Mashariki huko kusini mashariki mwa bara Asia walishiriki katika kura ya maoni na kuchagua kujitenga nchi hiyo na Indonesia. Kisiwa cha Timor ya Mashariki sambamba na visiwa vingine vya Indonesia kilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kireno mwaka 1511 Miladia. Timor Mashariki iliunganishwa na Indonesia mwaka 1976.

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, Jamhuri ya Azerbaijan ilitangaza uhuru wake kutoka Urusi ya zamani. Ardhi ya Azerbaijan ilitekwa na kukaliwa kwa mabavu na silsila ya Kiirani ya Wasasani tangu mwanzoni mwa karne ya Tatu Miladia na katika kipindi kikubwa cha historia yake ilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Vita kati ya Urusi ya zamani na Iran vilijiri mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, kufuatia kupenda kujitanua kwa utawala wa kifalme wa Tsar huko katika Umoja wa Kisovieti. Iran ilipata pigo katika vita hivyo na kupelekea sehemu moja ya ardhi ya kaskazini ya Azerbaijan kukaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani mwaka 1813 kwa mujibu wa mkataba wa Golestan.

   Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita, alizaliwa Ernest Rutherford, mtaalamu mkubwa wa fizikia wa nchini Uingereza maarufu kwa jina la baba wa nishati ya nyuklia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali eneo alikozaliwa, Ernest alielekea katika mji wa kielimu wa Cambridge na kujiunga na chuo kikuu cha mji huo. Kuanzia mwaka 1919 Rutherford alitokea kuwa mhadhiri mwenye tajriba katika uga wa fizikia chuoni hapo, huku akijiunga na jumuiya ya kifalme ya mjini London hapo mwaka 1903. Mwaka 1904, msomi huyo alisambaza kitabu chake alichokipa jina la ‘Shughuli za Mionzi’. Baadaye Ernest Rutherford aliongoza kundi la utafiti katika chuo kikuu cha Manchester, kundi ambalo haraka liliweza kuandaa nadharia mpya kuhusiana na muundo wa atomiki. Mwaka 1908, msomi huyo alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na shughuli zake hizo na kupata umaarufu mkubwa katika uga huo.