Hadithi ya Uongofu (50)
Ni matumaini yangu kuwa, hujambo mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya mfululizo wa kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 50 ya mfululizo huu kitazungumzo maudhui ya kuamrishana mema na kukatazana maovu. Kuweni name hadi mwisho wa kipindi hiki kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo.
Katika dini tukufu ya Kiislamu mambo yote mazuri huitwa maaruf na mambo yote mabaya na maovu hujulikana kama munkar. Hii ni kutokana na kuwa, fitra na maumbile safi ya mwanadamu yanatambua kazi njema na nzuri na maumbile hayo yana ugeni na mambo maovu na machafu. Katika istilahi za kifikihi pia majimui ya mambo wajibu na mustahabu yanatajwa kuwa ni maaruf na mambo ya haramu na yanayochukiza yanatajwa kuwa ni munkar. Kwa msingi huo basi, mambo mazurio yaani maaruf na mambo maovu yaani munkari yana wigo mpana na hayaishii tu katika madhambi makubwa na yanaweza kutajwa na kuwekwa katika makundi mawili ya mambo yenye thamani na mambo yaliyo dhidi ya thamani. Mtume SAW anaelezea na kubainisha umuhimu wa faradhi hii ya kuamrishana mema na kukatazana maovu pale aliponukuliwa akisema kwamba:
Kila mtu ambaye anaamrisha mema na kukataza maovu ni mwakilishi wa Mwenyezi na Mtume wake katika mgongo wa ardhi.
Kupitia hadithi hii inafahamika vyema na kwa uwazi kwamba, faradhi hii kubwa ya kuamrishana mema na kukatazana maovu ni mpango wa Mwenyezi Mungu; na kutumwa Mitume AS na kuteremshwa vitabu vya mbinguni ni kwa ajili ya kutekeleza mpango huu. Katika kubainisha athari za faradhi ya kumarishana mema na kukatazana maovu, Imam Muhammad Baqir AS anasema:
Kuamrishana mema na kukatazana maovu ni njia na mbinu za Mitume wa Mwenyezi Mungu na ni mtindo wa waja wema na ni faradhi kubwa ambayo kupitia kwayo faradhi nyingine husimama (hutekelezwa); njia hutawaliwa na amani, vipato huwa vya halali, haki zilizoporwa hurejea kwa wenyewe, ardhi huboreshwa, haki huchukuliwa kutoka kwa adui na kazi huenda vizuri.
Tukirejea Qur'ani tukufu tunaona jinsi Mwenyezi Mungu alivyobainisha na kuweka wazi sifa nzuri za waumini.
Aya ya 71 ya Surat Tawba inasema:
Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa Zaka, na humt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Kwa mujibu wa aya hii waumini hutakiana hatima njema baina yao. Kwa hakika wao ni kama mwili mmoja ambapo kosa la mmoja na kukengeuka mmoja wao ni jambo ambalo huwa na taathira kwa jamii nzima. Jambo hilo huwa mithili ya maradhi ya kuambukiza ambayo kama hayatapatiwa kinga na tiba basi huwaambukiza watu wengi katika jamii na hivyo kuufanya uzima na usalama wa jamii kuwa hatarini.
Kwa mtazamo wa Uislamu sio tu kwamba, mtu ana masuuliya juu ya amali na matendo yake, bali anawajibika na ana jukumu pia kwa kheri na mambo mema kwa watu wengine na jamii pia kwa ujumla. Umuhimu wa kuamrishana mema na kukatazana maovu ndipo unapoanzia.
Kuhusiana na hili Bwana Mtume SAW anaashiria nukta moja ya kuvutia sana. Anasema:
"Mtenda dhambi aliyeko baina ya watu ni sawa mtu asiye na ufahamu ambaye yuko katika kundi la watu ambalo linasafiri katika meli, ambapo baada ya kufika katikati ya bahari, bwana huyu aamue kuchukua nyundo na kuanza kubomoa au kutoboa sehemu aliyokaa. Watu wakimlalamikia kwa kitendo hicho aje na kusema, kwa nini mnanipigia makelele ilhali mimi natoboa sehemu yangu tu niliyokaa? Endapo watu watamuacha aendelee na kazi yake hiyo yenye hatari kubwa, bila shaka hautapita muda mrefu maji yataanza kuingia ndani ya meli na matokeo yake ni watu wote kuzama baharini."
Kwa hakika, mwanaadamu ni kiumbe ambaye ni wa kijamii na hatima na majaaliwa yake yanafungamana na hatima na majaaliwa ya jamii anayoishi ndani yake. Madhara na faida anayopata mwanadamu hurejea kwake na vile vile kuwa na taathira kwa jamii anayoishi. Aidha amali na matendo ya watu wengine yana taathira katika maisha yake. Hivyo basi, kama ambavyo mwanaadamu anabeba dhima ya matendo na miamala yake, vivyo hivyo anabeba jukumu na masuuliya ya utendaji katika jamii anayoishi. Kimsingi ni kuwa, akthari ya harakati nyingi za mageuzi na urekebishaji katika historia ya mwanaadamu zilizofanywa na watu wa Mwenyezi Mungu, zilikuwa ni kwa ajili hii, yaani kupambana na mabaya na kueneza mambo mazuri katika jamii.
Katika jamii ya Kiislamu, Mwislamu anapaswa kufanya juhudi na kuwa na nafasi katika harakati za mageuzi za wengine. Endapo ufisadi, dhambi na upotovu vitaenea katika jamii, ni dhahir shahir kwamba, athari zake mbaya zitawakumba watu wote katika jamii husika. Imam Ali bin Abi Talib AS anaelezea umuhimu wa kuamrisha mema na kukataza maovu pale anaposema:
Amali zote njema na jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu mbali na kuamrisha mema na kukataza mabaya ni kama vile kutia tone la maji katika bahari pana na yenye mawimbi."
Kuamrisha mema na kukataza mabaya ni bima na dhamana ya maisha ya saada ya wanaadamu sambamba na kudhamini uhuru wao.
Tukiirejea Qur'ani Tukufu tunmapata kuwa, sira ya kivitendo ya watu wakubwa katika dini pamoja na maneno yao yana nukta muhimu na zenye thamani kubwa ambazo zinaweza kuchaguliwa na kufanywa kuwa dira na mwenendo sahihi kwa ajili ya kusaidia kuamrishana mema na kukatazana maovu. Aya ya 159 ya Surat al-Imran inabainisha mwenendo mwema na tabia njema ya Bwana Mtume SAW katika kuwalingania watu dini tukufu ya Kiislamu. Aya hiyo inasema:
Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu.
Aya hii inabainisha kwamba, kuwalingania watu mambo mema na kuwakataza madhambi ni jambo ambalo linapaswa kufanyika kwa njia bora kabisa ya kiakhlaqi ikiambatana na huruma na huba
Jambo muhimu katika kuamrishana mema na kukatazana maovu ni kuwa, mtu anayewalingania watu na kuwaita katika mambo mema yeye mwenye anapaswa kuwa ni mwenye kulifanya jambo hilo jema na kinyume chake pia.
Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kisa kifuatacho.
Inanukuliwa kwamba, siku moja mwanamke mmoja alimleta mwanawe kwa Bwana Mtume SAW ili amkataze mtoto huyo kula sasa tende. Mtume SAW akamwambia mama yule aje kesho. Siku iliyofuata Mtume SAW alimgeukia mtoto yule na kumwambia " usile tende". Mwanamke yule alishangaa sana na kumuuliza Mtume kama ni hivyo tu, basi kwa nini maneno hayo hayo hukuyasema jana. Mbora huyo wa viumbe akajibu kwa kusema: Hiyo jana mimi mwenyewe nilikuwa nimekula tende na hivyo sikutaka kumkataza kitu mtoto ilihali mimi mwenyewe nimekifanya.
Na kwa kisa hicho ndio tunafikia tamati ya kipindi chetu kwa leo. Tukutane tena wiki ijayo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh..