Sep 05, 2016 08:50 UTC
  • Maafa ya Mina (3)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika mfululizo wa makala hizi maalumu ambazo zinaangazia maafa ya kusikitisha yaliyojiri katika eneo la Mina mwaka jana wakati wa Ibada ya Hija. Hii ni sehemu ya tatu ya mfululizo huu.

Katika makala iliyopita, tuliashiria matukio ya kusikitisha ambayo yalipelekea maelfu ya Mahujaji wa Nyumba ya Allah SWT kupoteza maisha kutokana na uzembe wa utawala wa Saudia.

Leo tutaanza kuangazia matukio ya kusikitisha katika Ibada ya Hija mwaka jana ambapo tukio la kwanza lilikuwa ni kuanguka winchi au kreni kubwa katika eneo la ndani ya msikiti mtakatifu ambao ni maarufu kama Masjid al-Ḥaram mjini Makka katika eneo ilimo Kaaba Tukufu.

Winchi hiyo iliyoanguka ilikuwa kubwa zaidi kati ya makumi ya zingine ndogo ndogo ambazo zilikuwa zikitekeleza mradi wa ujenzi ambao watawala wa Saudia wanadai ni kwa ajili ya kupanua Haram Takatifu.

Pamoja na kuwa watawala wa Saudia walifahamu kuwa msimu wa Hijja umewadia na kwamba kungekuwa na idadi kubwa ya Mahujaji katika Masjid al Haram, lakini hawakuondoa winchi hizo kubwa katika eneo hilo lenye msongamano mkubwa. Kwa msingi huo, tarehe 11 Septemba mwaka 2015, sawia na 27 Dhul Hijja mwaka 1436 Hijria Qamaria kulijiri tukio la kusikitisha la kuanguka winchi kubwa katika Masjid al Haram katika Kaaba Tukufu ambapo Mahujaji 107 waliuawa shahidi katika eneo hilo takatifu na wengine 238 kujeruhiwa.

Lakini baada ya siku chache baadaye Mahujaji walikumbwa na maafa makubwa zaidi.

Asubuhi katika siku ya siku kuu ya Idul Adha, yaani tarehe 24 Septemba 2015, idadi kubwa ya Mahujaji, kama ilivyo ada, walikuwa wanaondoka jangwa la Mashaar kuelekea Mina ili wakiwa hapo waweze kutekeleza amali ya kumpiga mawe shetani.

Lakini vikosi vya usalama vya Saudia vilifunga njia asili ambayo hutumiwa na Mahujaji na badala yake walielekezwa katika njia ndogo ya pembeni. Aidha njia za kuondoka katika njia hizo za pembeni nazo pia zilifungwa. Hatua kwa hatua idadi ya Mahujaji ilizidi kuongozeka katika eneo hilo. Mahujaji takribani elfu saba waliokuwa katika eneo hilo huku jua likiwa kali walijipata katika mbano mkubwa sana na wakaanza kukanyagana na wengi kupoteza maisha.

Maafisa wa usalama wa Saudia ambao walikuwa chanzo cha maafa hayo si tu kuwa hawakutoa msaada wowote wa maana kwa Mahujaji bali hata walichelewa sana kutoa msaada wa awali na jambo hilo kupelekea idadi

kubwa ya Mahujaji kupoteza maisha.

Kwa msingi huo, Maafa ya Mina katika Siku Kuu ya Idul Adha mwaka 1436 Hijria, yalikuwa maafa makubwa zaidi ya kibinadamu katika historia ya Hija.

Maafa ya Mina katika Hija ya mwaka 1436 Hijria

 

Serikali ya Saudia ilijaribu sana kuficha ukweli kuhusu ukubwa wa maafa ya kuogofya ya Mina. Lakini maafa hayo yalikuwa makubwa sana na watawala wa Saudia hawangeweza kuficha ukweli wa tukio hilo.

Punde baada ya kujiri maafa ya Mina, picha  na habari za tukio hilo zilienea katika mitandao ya kijamii na hivyo wakuu wa Saudia hawakuwa na budi ila kukiri ukweli. Katika hila yao ya pili, watawala wa Saudia walijaribu kuonyesha kuwa waliopoteza maisha walikuwa ni watu wachache tu na ni kwa msingi huo ndio wakatoa takwimu mbali mbali za waliofariki kutoka 700 hadi 4000. Jambo hilo pekee linaonyesha taarifa walizokuwa wakitoa hazikuwa za kweli.

Ni vigumu kupata picha kamili ya maafa ya kuogofya ya Mina mwaka jana. Ili kuweza kufahamu kilichowasibu wageni wa Nyumba ya Allah SWT katika kipindi hicho, tunategemea kauli za Mahujaji walioshuhudia kwa karibu yaliyojiri.

Mohammad, Haji kutoka Iran ambaye alipata taufiki ya kuhiji mwaka jana na pia alikuwepo katika eneo palipojiri maafa ya Mina anasema hivi:

"Baada ya kusubiri muda mrefu, kwa hamu kuu na shauku nilielekea katika Ardhi Takatifu. Kutokana na kimya ndani ya ndege, nilipata fursa nzuri ya kutafakari kuhusu safari hii ya kimaanawi na masuala mbali mbali. Nchini Iran tulikuwa na vikao mbali mbali na wasimamizi wa msafara wetu wa Hija na kujifunza kuhusu amali za Hija. Lakini tulikuwa na madukuduku kutokana na usimamizi mbovu wa wakuu wa Saudia katika Hija jambo ambalo hupelekea kuibuka maafa kwa wageni wa Nyumba ya Allah SWT. Aidha tulifahamu kuwa, Mawahabi walikuwa na muamala mbaya na Mahujaji ambao hawakubaliani na itikadi zao hasa Mashia. Pamoja na hayo, tulimtegemea Mwenyezi Mungu na kujitahidi kuwa na mtazamo chanya kwa kutafakari kuhusu ibada hii na mandhari yenye mvuto mkubwa ya adhama ya Kaaba Tukufu na kuba maridadi ya Msikiti wa Mtume SAW."

Mohammad anaendelea kusema, "ndege yetu ilitua salama katika Uwanja wa Ndege wa Madina. Tukiwa hapo tulichelelweshwa kutokana na urasimu katika uwanja wa ndege. Maafisa wa uwanja wa ndege walikuwa wakali sana katika kuchunguza pasi za kusafiria za abiria Wairani pamoja na kuwa walifahamu zilikuwa na itibari. Waliwakera Mahujaji Wairani na kuwabugudhu kwa kukagua kupita kiasi mizigo yao. Ni kana kwamba walikuwa wakifuatilia kitu maalumu. Wakati alipokuwa akipekua begi langu, afisa Msaudi alichukua nakala ndogo ya Qur'ani niliyokuwa nayo na kuirusha pembeni kwa njia ya kuivunjia heshima. Kitendo hicho kilinikasirisha mno lakini nilijizuia kubainisha hasira zangu wazi wazi kwani nilifahamu fika kuwa, kubaini hasira zangu  kungepelekea nipate matatizo makubwa. Pamoja na hayo nilipata ujasiri wa kuuliza ni kwa nini amenipokonya nakala yangu ya Qur'ani. Afisa huyo Msaudi ambaye alionekana kutoheshimu Qur'ani ambayo ni tukufu kwa Waislamu wote, alitoa jibu lisilo la kimantiki na kusema: "Kuna nakala za kutosha za Qur'ani Masjid al Haram na Masjid an Nabii." Begi langu lilichukuliwa na nilipolipokea hotelini, nilifahamu kuwa maafisa wa Saudia walikuwa wamechukua Misahafu yangu yote na vitabu kuhusu Ibada ya Hija," anasema Mohammad ambaye alishiriki katika Ibada ya Hija mwaka jana na kushuhudua maafa ya Mina.

Maafa ya Mina katika Hija ya mwaka 1436 Hijria

 

Wapenzi wasikilizaji, tunafikia tamati hapa kwa leo, katika makala yetu Ijayo ya Maafa ya Mina, panapo majaliwa yake Mola tutaendelea kusimulia kisa cha Mohammad na aliyoshuhudia katika Ibada ya Hija mwaka jana. Kwaherini.

Kwa maelezo zaidi kuhusu Maafa ya Mina: http://kiswahili.irib.ir/habari/mina

Kwa maelezo zaidi kuhusu makala za Hija: http://kiswahili.irib.ir/uislamu/hija

Tags