Sep 07, 2016 05:56 UTC
  • Familia Salama (6)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Afya ya Familia. Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k.

Katika makala yetu ya sita katika mfululizo huu, tutaangazia suala la ndoa katika masiha ya mwandamu. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.

Kufunga ndoa ni hitajio la kimaumbile na la kimsingi katika jamii ya mwanadamu. Jamii mbali mbali duniani huwa zinafuatilia malengo maalumu katika suala la ndoa na kuunda familia. Katika mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu, malengo na sababu za ndoa zimebainishwa kama dharura zenye taathira muhimu katika nguzo zote za maisha.
Sababu ya kwanza na muhimu zaidi katika kufunga ndoa kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu ni kuunda nguzo ambayo itamfanya mwanaume na mwanamke wapate utulivu.
Mwenyezi Mungu SWT anasema katika Qur'ani Tukufu aya ya 21 ya Sura Rum:
"Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri."
Moja ya sababu kuu za kuongezeka msongo wa mawazo na mfadhaiko wa nafsi miongoni mwa vijana katika dunia ya leo ni kukosa kufunga ndoa katika wakati unaofaa. Vijana wa kike na kiume hukumbwa na pandashuka katika maisha na hivyo huhitaji usalama na mahaba baina yao. Anayeweza kuleta mahaba na usalama sambamba na kuwa rafiki wa kudumu ni mwanandoa mwenza. Wakati kijana wa kike na kiume wanapofunga ndoa na hivyo kuishi pamoja kwa njia halali, wao huweza kuwa chanzo cha kuwepo utulivu, usalama na mahaba baina yao.
Ndoa ni kati ya njia muhimu na zenye taathira katika kubainisha ukuruba, mahaba na mahusiano ya kibinadamu. Wanasaikolojia wanasema moja ya hitajio la kimsingi na muhimu la mwanadamu ni 'hitajio la mahaba'.
Mwanadamu anahitajia mahaba katika kila kipindi cha umri wa maisha yake. Ni dhati ya mwanadamu kuona wengine wakimpenda huku naye pia akibainisha mahaba yake. Athari ya mahaba ni kubadilika kwake kuwa mapenzi na ukuruba wa kina na wa kudumu yaani kuungana mwanamke na mwanaume katika ndoa. Iwapo wanandoa watakuwa na mapenzi imara, basi mazingira ya kifamilia huwa mazuri, yenye ukuruba na utulivu. Kupata mahaba kutoka kwa wengine na kuwapa wengine mahaba, huleta hali maridhawa na mlingano wa kisaikolojia.
Moja ya sababu muhimu zenye kutoa msukumo kwa mwanadamu kufunga ndoa ni kupata usalama wa kimwili na wa kisaikolojia. Hii ni kwa sababu ndoa hupelekea wanandoa kukidhi mahitaji yao ya kimwili na kisaikolojia.
Mwanadamu anahitaji kupata yakini kuhusu usalama na maingiliano ya kijamii. Aidha mwanadamu huhitaji mtu mwenye kumliwaza na anayeweza kutafakari pamoja naye. Iwapo mahitajio hayo hayatakidhiwa kwa wakati unaofaa katika mazingira ya kifamilia, basi jambo hilo linaweza kumsababishia mtu matatizo mengi katika maisha binafsi na ya kijamii. Kwa msingi huo ndoa ina nafasi muhimu katika kukidhi mahitaji hayo. Mwanadamu akiweza kukidhi mahitaji hayo basi hupata utulivu na maisha yenye mlingano sahihi.

 

Kufunga ndoa na kuunda familia kuna maana ya kuleta maadili mema katika jamii, kuleta usalama na afya ya kisaikolojia, utulivu, mahaba na kuhurumiana. Familia ina nafasi ya kipekee katika jamii kama chimbuko muhimu zaidi la kukidhi mahitaji hayo tuliyotangulia kuyataja.
Kati ya faida muhimu za kufunga ndoa, ni kusaidia katika kustawi na kukamilika mwanaume na mwanamke. Hii ni kwa sababu mazingira yenye ukarimu ya familia huwa yamejaa mapenzi na mahaba na hivyo kuandaa fursa ya wanadoa kutafakari pamoja kuhusu masuala mbali mbali. Jambo hilo hupelekea kustawi kijamii, kiutamaduni na kimaadili mume na mke na wanafamilia wengine.
Familia inaweza kutazamwa kama taasisi ambapo walio katika taasisi hiyo huweza kustawi kielimu na kuimarisha vipaji vyao. Katika mazingira hayo yaliyojaa vipawa, mwanaume na mwanamke huweza kujiimarisha kwani huwa wanapata hisia ya uwajibikaji na katika hali hiyo jamii nzima huweza kustawi.
Hisia ya kutaka kupata watoto na kuendeleza kizazi daima ni moja na vivutio na lengo muhimu la kufunga ndoa katika vipindi mbali mbali vya historia ya mwanadamu. Mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu wa zama hizi Shahidi Murtadha Mutahhari ameandika kuhusu matamanio ya kimwili na ghariza ya kujamiiana kwa mtazamo wa Kiislamu akisema kwamba: "Katika mtazamo wa Kiislamu matamanio ya kimwili si tu kwamba hayakinzani na masuala ya kiroho na kimaanawi bali pia ni sehemu ya tabia za Mitume. Kwa mujibu wa hadithi nyingi zilizopokewa na maulamaa wa Kiislamu, Mtume Mtukufu SAW ameeleza waziwazi mapenzi na uungaji mkono wake kamili kwa ndoa, na kinyume chake kukemea mno njia ya watu wanaokhitari maisha ya utawa."
Kufunga ndoa na kuunda familia huwa na nafasi muhimu katika kuunda jamii iliyo takasika na yenye kuzingatia maadili mema. Kwa hakika ndoa huimarisha jamii na kupelekea kuwepo maadili mema na saada pamoja na ufanisi katika umma.
Kwa hivyo Familia ni taasisi ya awali na yenye umuhimu zaidi katika jamii. Mafanikio na matatizo yanayoikumba kila jamii katika awamu ya kwanza huwa na mfungamano na familia. Dini ya Uislamu imetoa umuhimu mkubwa kwa familia kuliko taasisi nyingine yoyote na ndio maana ikaitambua ndoa, uhusiano wa ndani ya familia na kubakia kwake kuwa mambo yenye umuhimu mkubwa. Kuasisi familia pia ni suna ya Mtume Mtukufu SAW, hii ni kwa sababu familia ina nafasi ya juu katika kukidhi mahitaji ya mwanadamu.
Wapenzi wasikilizaji tunakamilisha makala hii fupi kuhusu umuhimu wa ndoa kwa kunukulu Hadithi ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad SAW alipozungumza kuhusu ndoa kama chanzo cha kuwepo maadili mema katika mwanadamu kwa kusema: "Wanaume na Wanawake wasio katika ndoa waoane kwani Mwenyezi Mungu atayafanya maadili yao yawe mema."

 

Tags