Alhamisi, Septemba 8, 2016
Leo ni Alkhamisi tarehe 6 Dhilhija 1437 Hijria sawa na tarehe 8 Septemba 2016.
Tarehe 6 Dhilhaji mwaka 1407 Hijria yaani siku kama ya leo miaka 30 iliyopita mamia ya mahujaji wa Kiirani na mahujaji kadhaa wa nchi nyinginezo wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa serikali ya Saudi Arabia, walipokuwa wakitekeleza faradhi ya kujibari na kujiweka mbali na washirikina. Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu hutekeleza ibada hiyo kila mwaka wakati wa Hija, kutokana na mafunzo ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo sambamba na kutoa wito wa umoja na mshikamano baina ya Waislamu, hutoa tangazo la kujiweka mbali na maadui wa Uislamu hasa Marekani na utawala ghasibu wa Israel. Kwa kutilia maanani umuhimu wa suala hiyo mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayati Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) daima alikuwa akisisitiza katika ujumbe wake kwa wahujaji juu ya kufanya shughuli hiyo ya kujitenga na washirikina na mabeberu, na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei pia amekuwa akisisitiza sana juu ya umuhimu wa kufanyika kwake na kwamba inawaamsha Waislamu na kudhihirisha uwezo na nguvu zao.
Miaka 47 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia Jalal Aal Ahmad, mwandishi na mkosoaji wa Kiirani. Aal Ahmad alizaliwa mwaka 1302 Hijria Shamsiya jijini Tehran. Mwaka 1325, Jalal al Ahmad alitunukiwa shahada ya fasihi ya Chuo Kikuu cha Tehran. Aliingia katika uwanja wa siasa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia na akaanza kuandika magazeti. Alijishughulisha na kuandika makala na ukosoaji na hadithi fupifupi. Jalal Aal Ahmad alikuwa hodari katika kuandika visa na hekaya fupifupi.
Miaka 62 iliyopita katika siku kama ya leo, mkataba wa SEATO wa makubaliano ya kiulinzi ya Asia ya Kusini-Mashariki ulisainiwa katika mji mkuu wa Ufilipino, Manila. Serikali za Marekani, Uingereza, Australia, Pakistan, Thailand, Ufaransa, New Zealand na Ufilipino ndizo zilizosaini mkataba huo. Nchi hizo zilikubaliana kusaidiana iwapo zingeshambuliwa na nchi nyingine au kukabiliwa na uasi wa ndani.
Tarehe 8 Septemba ilitangazwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ujinga. Kujua kusoma na kuandika ni miongoni mwa vielelezo cha ustawi katika jamii ya mwanadamu na ujinga husababisha umaskini na kubakia nyuma kimaendeleo. Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa mkakati wa kupambana na kutojua kusoma na kuandika haukuwa wa kuridhisha katika baadhi ya nchi na hadi sasa idadi kubwa ya watu hawajapata neema hiyo.
Nchini Iran baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu kulifanyika jitihada kubwa za kupambana na ujinga wa kutojua kusoma na kuandika kwa kadiri kwamba Disemba mwaka 1979 Imam Ruhullah Khomeini alitoa amri ya kuasisiwa Harakati ya Kupamgana na Ujinga. Taasisi hiyo imechukua hatua kubwa hapa nchini.
Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, majeshi ya Wanazi wa Ujerumani yaliuzingira mji wa Leningrad miezi mitatu baada ya kuishambulia ardhi ya Umoja wa Sovieti. Hata hivyo na licha ya utabiri wa Hitler na makamanda wake, nji huo haukusalimu amri na wananchi wa mji wa Leningrad ambao kwa sasa unajulikana kwa jina la Saint Petersburg, waliendeleza mapambano na wakafanikiwa kuvunja mzingiro huo kufikia januari mwaka 1944. Karibu raia milioni moja wa mji wa Leningrad walipoteza maisha katika mzingiro wa majeshi ya Ujerumani ya Kinazi kutokana na kukosa suhula muhimu kama chakula na kadhalika.