Jumatano, Septemba 14, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 12 Dhulhija 1437 Hijria sawa na Septemba 14, 2016.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, hati ya Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ilitiwa saini na nchi za Iran, Saudia, Iraq, Kuwait na Venezuela. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na makampuni makubwa ya mafuta ya Magharibi ambayo yalikuwa yakisimamia uvumbuzi, uchimbaji na uuzaji wa bidhaa hiyo kimataifa na kuainisha bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa maslahi yao binafsi na kwa madhara ya nchi zalishaji. Licha ya kwamba awali jumuiya hiyo haikuwa na nguvu wala ushawishi wowote, lakini ilikuja kupata nguvu zaidi baada ya nchi kadhaa zikiwemo, Algeria, Libya, Nigeria, Qatar, Imarat, Gabon, Indonesia na Ecuador ambazo ni wazalisha wa mafuta kujiunga nayo.
Tarehe 14 Septemba miaka 204 iliyopita, moto mkubwa na wa kihistoria duniani ambao uliwashwa kwa makusudi ulitokea katika mji mkuu wa Russia, Moscow. Tukio hilo lilitokea siku moja tu baada ya mji huo kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Napoleone Bonaparte. Mtawala wa mji wa Moscow alitoa amri mji huo uchomwe moto kwa lengo la kuyafanya majeshi ya Ufaransa yashindwe kupata chakula na suhula nyingine za kuyawezeaha kubakia mjini humo. Moto huo mkubwa uliteketeza na kuharibu kabisa robo tatu ya mji mzima wa Moscow.
Miaka 497 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 12 Dhul-Hijja mwaka 940 Hijria, aliaga dunia Ali bin Hussein Karaki al Amili mmoja wa mafakihi wakubwa wa Kiislamu. Alisoma elimu ya msingi katika eneo alikozaliwa la Jabal Amil nchini Lebanon na baadaye alifanya safari katika nchi nyingine za Kiislamu akiwa na lengo la kujiendeleza kielimu. Mhakiki Karaki kama anavyojulikana zaidi, ameandika vitabu vyenye thamani kubwa. Jamiul Maqaasid, Sharhu Sharaai' na Risatul Adalah ni baadhi ya vitabu vyake mashuhuri.
Na siku kama ya leo miaka 626 iliyopita, utawala wa Othmania uliidhibiti na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Serbia. Tukio hilo lilijiri wakati wa operesheni za utawala huo za kuzitia katika milki yake ardhi za Ulaya. Ushindi huo ulipatikana katika kipindi cha utawala wa Sultan Murad I, Mfalme III wa utawala wa Othmania. Licha ya kuweko uasi wa wananchi wa Serbia, lakini ardhi yao iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Ufalme huo kwa karibu karne tano.
Na siku kama hii ya leo miaka 17 iliyopita sawa na tarehe 24 mwezi Shahrivar mwaka 1378 Hijria shamsiya, alifariki dunia kwa maradhi ya moyo Dakta Abdulhussein Zarinkub mwanahistoria na mtafiti mashuhuri wa Kiirani. Dakta Abdulhussein alizaliwa mwaka 1301 Hijria Shamsiya katika mji wa Burujerd magharibi mwa Iran. Mwaka 1327 Hijria Shamsiya Dakta Zarinkub alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya historia na baadae akaendelea na masomo yake katika taaluma hiyo na kutunikiwa shahada ya udaktari. Mbali na historia msomi huyo wa Kiirani alipenda sana masomo ya fasihi ya lugha ya Kifarsi na irfani ya Kiislamu. Aidha aliandika vitabu na makala nyingi na moja kati ya vitabu vyake ni kile alichokiita "Alfajiri ya Uislamu."