Sep 21, 2016 07:05 UTC
  • Familia Salama (7)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Afya ya Familia. Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k.

Katika makala yetu iliyopita katika mfululizo huu, tuliangazia suala la ndoa katika maisha ya mwandamu. Tulisema kufunga ndoa ni hitajio la kimaumbile na la kimsingi katika jamii ya mwanadamu. Jamii mbali mbali duniani huwa zinafuatilia malengo maalumu katika suala la ndoa na kuunda familia. Katika mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu, malengo na sababu za ndoa zimebainishwa kama dharura zenye taathira muhimu katika nguzo zote za maisha. Tulisema dini ya Uislamu imetoa umuhimu mkubwa kwa familia kuliko taasisi nyingine yoyote na ndio maana ikaitambua ndoa, uhusiano wa ndani ya familia na kubakia kwake kuwa mambo yenye umuhimu mkubwa. Kuasisi familia pia ni suna ya Mtume Mtukufu SAW, hii ni kwa sababu familia ina nafasi ya juu katika kukidhi mahitaji ya mwanadamu. Makala hii itaangazia baadhi ya nukta za kuzingatiwa ili kulinda familia ili isisambaratike. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.
Leo katika jamii nyingi, misingi ya familia inakabiliwa na tishio kubwa huku takwimu za talaka zikizidi kuongezeka. Wataalamu wa masuala ya familia wanasema, mbali na matatizo ya kiuchumi na kijamii ambayo yanahatarisha mustakabali wa familia, matatizo ya kimaadili ndani ya familia pia yamekuwa changamoto kubwa.
Katika baadhi ya familia tunashuhudia kupungua mahaba na ukuruba wa wanandoa na la kusikitisha ni kuwa baadhi sasa wamegeuka na kuwa mahasimu ndani ya nyumba.
Moja ya sababu ambazo zinahatarisha usalama wa uhusiano wa mume na mke ni kuondoka ile hali ya kuheshimiana baina yao. Baada ya mwanaume na mwanamke kufunga ndoa, wao huwa wamejenga ukuruba wa karibu zaidi kwa mitazamo ya kiroho na kihisia. Kwa hivyo ukarimu baina yao unapaswa kuwa mkubwa zaidi baina yao ikilinganishwa na wakati wanapoamiliana na watu wengine. Lakini la kusikitisha ni kuwa, katika zama hizi baadhi ya wanandoa vijana huwa wanadhalilishana na kuvunjiana heshima hata katika miezi ya awali ya maisha yao ya pamoja. Hali kama hii hupelekea machungu kuanza kuibuka nyoyoni na hivyo kuwa mwanzo wa kuzorota maisha ya ndoa.
Iwapo wanandoa watazungumziana kwa heshima basi mahaba na mapenzi baina yao huongezeka na maisha huwa yaliyojaa furaha. Njia ambayo wanandoa wanaweza kukirimiana ni kwa kuzungumziana kwa kauli nzuri na zilizojaa mahaba. Hivyo wanandoa wanapaswa kutumia maeneno mazuri na wajiepushe na tabia ya kutafuta nukta dhaifu kila wakati na pasina kuwepo udharura.
Wanandoa wanapaswa kubadilishana mawazo na fikra na waweze kuliwazana na watumie maneno bora zaidi wakati wanapozungumza kuhusu maudhui mbali mbali baina yao.
Leo tunaona namna ambavyo tabia ya kukosana au kupingana mara kwa mara baina ya wanandoa hudhuru uhusiano mzuri walionao. Katika ndoa, mwanandoa si mfanyakazi au mtumwa wa mwenzake bali wanapaswa kuwa ni wenye kusaidiana na kushirikiana.

 

Katika familia kuna umuhimu kwa wanandoa kutotilia maanani makosa madogo madogo na katika upande wa pili ni muhimu kupeana sifa nzuri na kuzingatia hisia za kila mmoja. Aidha kuna haja ya kulinda heshima ya mwanadoa mwenezako mbele ya jamii, jamaa , familia na marafiki.
Hali kadhalika wanandoa hawapaswi kulaumiana mara kwa mara. Pia ni muhimu kwa mwanandoa kujiepusha kumsengenya au kumkosoa mwenzake mbele ya watu wengine. Kutangaza udhaifu wa mume au mke ni kati ya makosa makubwa yanayofanywa na wanandoa na iwapo suala hili litaendelea basia mapenzi hupungua na kusababisha madhara.
Hakuna shaka kuwa kila mwanadamu ana udhaifu wake lakini kuutangaza na kukuza udhaifu au aibu za mwingine huibua chuki na uhasama katika familia.
Itakuwa ni jambo bora na la busara iwapo wanandoa watahimizana na kushajiishana katika mema. Aidha kila mmoja anapaswa kuyaheshimu na kuyapa umuhimu maneneo ya mwenzake. Hali kadhalika wanandoa wanashauriwa kushikiriana na kupongezana kutokana na kutekeleza majukumu na kazi mbali mbali ndani au nje ya nyumba. Mwanandoa anapaswa kuwa na mazoea mazuri ya kumshukuru mwenzake kutokana na mahaba na ushirikiano aliouonyesha. Kushukuru, kuwa mtiifu na mwaminifu katika ndoa hupelekea kuongezeka ukarimu, mahaba na kulainishwa nyoyo baina ya wanandoa.
Katika ndoa pia, mume na mke wanapaswa kufahamiana vizuri kitabia, kiroho, kifikra na hata kidini ili maisha yao yawe ya kawaida na yaliyojengeka katika msingi wa maelewano. Hali kama hii ikiwepo kila mmoja atafahamu ni wakati gani au ni kitendo kipi kinaweza kuumiza hisia za mwingine na kuibua hali ya kutofahamiana.
Maelewano kama hayo yakiwepo baina ya wanandoa, iwapo kutaibuka changamoto na hitilafu basi wao huweza kupata suluhu haraka kwa njia ya mazungumzo na kuheshimian pande mbili.
Wapenzi wasikilizaji, tunafikia tamati ya makala yetu ya leo kwa kunukulu kauli ya Bwana Mtume Muhammad SAW aliposema: "Yule aliyemchagua mwanandoa anapaswa kumheshimu."

 

 

Tags