Oct 21, 2016 06:06 UTC
  • Ijumaa, 21 Oktoba, 2016

Leo ni Ijumaa tarehe 19 Muharram 1438 Hijria sawa na 21 Oktoba 2016.

Tarehe 19 Muharram mwaka 61 Hijria msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na familia ya mjukuu wa Mtume, Imam Hussein (as) na mashahidi wengine waliouawa na utawala wa Yazid bin Muawiya katika medani ya Karbala uliondoka Kufa nchini Iraq ukielekea Damascus, makao makuu ya serikali ya Bani Umayyah.

Mateka hao hususan Imam Zainul Abidin na Bibi Zainab binti Ali bin Abi Twalib (as) walifichua na kuanika maovu ya Yazid bin Muawiyyah na kuwafanya watu wa Kufa wajute sana kwa kumuacha peke yake mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein katika mapambano ya Karbala. Watu wa mji wa Kufa walisikitika sana kutokana na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume na wasiwasi ulizuka juu ya uwezekano wa kuanza harakati ya wananchi dhidi ya utawala wa Yazid mjini humo. Kwa msingi huo mtawala wa Kufa, Ubaidullah bin Ziyad, alikhitari kutuma wajukuu hao wa Mtume wetu Muhammad (saw) huko Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiya wakitanguliwa na kichwa kilichotenganushwa na mwili cha Bwana wa Vijana wa Peponi, Imam Hussein (as).

Msafara wa mateka wa Karbala

Siku kama ya leo miaka 226 iliyopita, alizaliwa malenga wa Kifaransa Alphonse de Lamartine.  De Lamartine alitambulika kuwa msanii na mwanafikra mkubwa nchini Ufaransa. Aliwahi pia kusafiri Mashariki na kuishi katika mji mkuu waBairut,Lebanon. Aidha miongoni mwa athari za malenga huyu, ni pamoja na "Safari ya Mashariki" na "Kimya cha Malaika".  Alphonse de Lamartine alifariki dunia mwaka 1869.

Alphonse de Lamartine

Miaka 183 iliyopita katika siku kama hii ya leo, alizaliwa Alfred Nobel mkemia wa Sweden na mvumbuzi wa dynamite. Nobel alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza sayansi ya kemia na baadaye akafanya utafiti mkubwa katika uwanja huo na kufanikiwa kuvumbua mada za mlipuko yaani (dynamite). Kinyume na alivyotarajia, majeshi ya nchi mbalimbali yalianza kutumia dynamite vitani na hivyo kusababisha mauaji ya raia wengi. Mkemia Nobel ambaye alikuwa na utajiri mkubwa na hakufikiri kuwa dynamite ingeweza kutumiwa vibaya, aliamua kutoa utajiri wake kama tuzo na zawadi. Alfred Nobel alifanya hivyo kwa lengo kwamba, tuzo hiyo itolewe kila mwaka kwa shakhsiya aliyefanya kazi kubwa ya thamani duniani katika masuala ya sayansi, fasihi na amani. Hata hivyo kinyume na matakwa yake, leo hii tuzo ya amani ya Nobel imechukua sura ya kisiasa na inatumiwa kama wenzo wa kutangaza na kueneza siasa za nchi za Magharibi duniani.

Alfred Nobel

Tarehe 30 Mehr miaka 64 iliyopita, Dakta Hussein Fatimi, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Muswadiq, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Iran wakati huo alitangaza hbari ya kukatwa uhusiano wa kisiasa kati ya Iran na Uingereza. Uamuzi huo ulikabidhiwa kwa balozi mdogo wa Uingereza mjini Tehran, baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri. Dakta Fatimi alisema Tehran imeamua kukata uhusiano na Uingereza kutokana na upuuzaji wa serikali ya London kwa matakwa ya wananchi wa Iran ya kujipatia haki zao, hususan katika uwanja wa kutaifisha sekta ya mafuta. Dakta Fatimi aliwataka viongozi wa London wabadili siasa zao kuhusiana na Iran.

Dakta Hussein Fatimi

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita Brigedia Jenerali Mundhir Abu Ghazala, kamanda Jeshi la Majini la Palestina aliuawa na maajenti wa shirika la ujasusi la utawala ghasibu wa Kizayuni Mossad. Wazayuni walimuuwa kigaidi kamanda huyo wa jeshi la majini la Palestina kwa kutega bomu ndani ya gari lake huko Athens mji mkuu wa Ugiriki. Brigedia Jenerali Abu Ghazala ni miongoni mwa wahanga wa ugaidi wa kiserikali wa utawala wa kibaguzi wa Kizayuni unaoungwa mkono kwa hali na mali na Marekani.

Mundhir Abu Ghazala