Oct 22, 2016 10:49 UTC
  • Familia Salama (10)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nasi katika mfululizo huu wa makala kuhusu Familia salama.

Makala hizi huangazia masuala mbali mbali ya afya ya familia kama vile lishe, mazoezi, madhara ya matumizi ya mihadarati, umuhimu wa mahaba katika familia n.k. Katika makala ya leo tutaangazia kuhusu umuhimu wa afa ya kiakili au kisaikolojia. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho.
Mtu mwenye afya bora ni yule ambaye mbali na afya ya kimwili, pia huwa na afya na utulivu wa kiakili au kisaiklojia. Familia ni muhimu kwa ajili ya hadhi ya kijamii ya mtoto kwani na hilo hubainika katika miaka 20 ya kwanza ya maisha katika familia. Watoto huritihi sifa za wazazi au walezi wao katika familia. Kwa msingi huo, familia inapaswa kuandaa mazingira mazuri ya kulea na kustawisha vipaji vya mtoto.
Familia inabeba jukumu la kukidhi mahitaji ya kifedha na kiroho ya mtoto ili kwa njia hiyo kudhamini mahitajio ya afya ya kimwili na kiakili ya mtoto. Kwa hakika watoto ambao wananyimwa mahaba na ukarimu wa familia wanaweza kuwa na matatizo makubwa katika mustakabali. Afya ya kiroho na kiakili huanza kuchukua muundo wake hata kabla ya kuzaliwa. Mazingira ya kiroho ndani ya nyumba, na masaibu ya kiakili wakati wa kubeba mimba pamoja na uhusiano wa mume na mke katika kipindi chote cha miezi tisa ya mimba ni mambo ambayo huwa na nafasi kubwa katika afya ya kiakili ya mtoto akisha zaliwa. Baada ya mtoto kuzaliwa, huwa anahitaji mahaba na ukarimu wa wazazi sambamba na kuhisi usalama katika familia. Kadiri uhusiano wa wazazi na mtoto wao unavyokuwa wenye ukarimu na uliojaa mahaba, ndivyo ambavyo wazazi watakuwa na nafasi kubwa katika kuainisha hatima ya mtoto wao.

Image Caption

 

Wazazi wenye mtoto zaidi ya mmoja wanapaswa kujiepusha na ubaguzi baina ya watoto na kufadhilisha moja kuliko mwingine. Aidha watoto hawapaswi kubaguliwa kwa msingi wa jinsia au umri. Kumfadhilisha mtoto mmoja kuliko mwingine ni jambo ambalo huwa na taathira mbali mbali katika msingi wa tabia katika siku za usoni.

Zama za kubalegehe ni kati ya zama muhimu zaidi katika maisha ya mwanadamu. Katika kipindi hiki, hujiri mabadiliko makubwa ya kimwili, kiakili, kiroho na kisaikolojia. Iwapo wazazi au walezi hawajui au wanapuuza yanayojiri katika kipindi hiki, yamkini jambo hilo likapelekea kuibuka matatizo na hitilafu za kifamilia na kijamii na kuwa chanzo cha kuporomoka maadili ya barobaro.

Zama za barobaro na ujana huwa zama ambazo hujiri matukio muhimu kama vile kuanza masomo ya juu, kuamua au kuchagua kazi ya kufanya maishani na kuanza kufanya kazi. Kimsingi hiki ni kipindi ambacho huainisha utambulisho wa kijamii na mustakabali wa mtu binafsi.
Hatua muhimu ya maisha ya mwanadamu yaani kuchagua mwanandoa pia aghalabu hujiri katika kipindi hiki. Kama ambavyo kuna umuhimu wa afya ya kiakili na kisaikolojia katika familia na kijana katika chaguo bora na la kimantiki la mwanandoa, pia katika kipindi hiki ndio huibuka uporomokaji wa maadili na thamani na ndoa zilizo hatari. Iwapo kutajiri kosa wakati wa kuchagua mwanandoa, yamkini familia ikakumbwa na msukosuko na hata kusambaratika ikiwa ingali changa.

Kipindi kingine katika maisha ambacho huwa muhimu katika afya ya kiakili na kisaikolojia ni kipindi cha uzeeni.
Katika kipindi hiki mwanadamu huwa anaanza kupoteza uwezo wa kimwili na wengine hukumbwa na maradhi mbali mbali na hivyo iwapo tahadhari haitachukuliwa, wazee hukumbwa na matatizo ya kiroho na kisaikolojia.
Kutozingatia utulivu wa kiroho wa wazee katika familia ni jambo ambalo yamkini likapelekea kuibuka madhara yasiyoweza kufidiwa kama vile mfadhaiko wa kiakili, tatizo la kusahau mara kwa mara na hata kupelekea kuibuka ugonjwa wa Alzheimer. Ugonjwa wa Alzheimer's ni miongoni mwa magonjwa ya kudhoofika ubongo yanayoathiri zaidi wazee au watu wa umri wa makamo.
Kwa msingi huo kuna umuhimu wa kudumisha uhusiano wa mara kwa mara baina ya watoto, wajukuu na wazee. Wajukuu wanapaswa kuwatembelea babu na nyanya au mabibi zao wakiwa wameandamana na wazazi wao na kuwaonyesha heshima na mahaba. Jambo hilo huwafanya wazee kupata furaha na kujihisi kuwa wenye faida na wanaohitajika katika jamii. Katika hali kama hii wazee huwa na uwezo wa kustahamili magonjwa, udhaifu na masaibu yanayotokana na uzee.
Nukta nyingine muhimu uzeeni ni kuzingatia mfumo sahihi wa chakula kinachojumuisha lishe sahihi na hivyo kudhamini afya yao na pia kuzia kuibuka matatizo ya ubongo.


Nukta ya mwisho ambayo tutaangazia katika makala hii, ni wanasaikolojia kusisitiza kuhusu taathira chanya ya dini au kufuata dini katika afya ya kiroho na kisaikolojia katika familia.
Katika vipindi vyote vya maisha, tokea wakati mama akiwa na mimba hadi mwisho wa maisha katika zama za uzeeni, kumkumbuka Mwenyezi Mungu au Dhikri na kuzingatia masuala ya uchaji Mungu huwa na taathira nzuri sana katika kuleta utulivu wa kiroho na kisaikolojia katika mwanadamu.
Uchunguzi umebaini kuwa, familia ambazo zinazingatia mafundisho ya kidini husalimika kwa kiwango kikubwa na matatizo na masaibu yanayotokana na utovu wa maadili.
Hali kadhalika kuzingatia ibada na mafundisho ya kidini huwa chanzo cha kupata ushindi mbele ya masaibu ya kiroho na kisaikolojia.
Katika idiolojia na itikadi zake, dini ya Uislamu inamfunza mwanadamu kwamba, kwa upande mmoja uwepo wake unafungamana kikamilifu na Mwenyezi Mungu, na kwa upande mwingine maisha yake hayaishii katika maisha ya dunia bali kuna maisha ya baada ya kufa ya Akhera. Hivyo, mwanadamu anawajibika kulinda uhusiano wa dunia na maisha ya milele ya Akhera. Katika mtazamo wa Uislamu maisha ya dunia ni utangulizi na daraja la kufika kwenye saada na ufanisi wa milele huko Akhera na mwanadamu anapaswa kuyatumia vizuri maisha yake ya dunia.
Wapenzi wasikiliaji makala yetu inafikia tamati hapa kwa leo na ni matumaini yangu kuwe mmeweza kunufaika na tuliyokuandilieni. Katika makala yetu ijayo tutaangazia suala la tatizo la mihadarati au dawa za kulevya katika jamii. Ni matumaini yangu utajiunga nasi wakati huo panapo majaaliwa yake Mola. Hadi wakati huo, Kwaherini.