Jumapili, 13 Novemba, 2016
Leo ni Jumapili tarehe 13 Swafar mwaka 1438 Hijria, sawa na tarehe 13 Novemba, 2016 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1135 iliyopita, alifariki dunia Abu Abdir-Rahman Ahmad Bin Shuaib Nasai, maarufu kwa jina la Sheikhul-Islami, mtaalamu mashuhuri wa hadithi. Abu Abdir-Rahman Ahmad Bin Shuaib Nasai alizaliwa mwaka 220 Hijiria katika moja ya vijiji vya Khorasan, kaskazini mashariki mwa Iran ambapo akiwa kijana alifanya safari nchini Misri na kufanya makazi yake huko. Akiwa nchini Misri alisoma elimu ya sharia za Kiislamu (fiqhi) kutoka kwa walimu wakubwa wa zama hizo na kufikia daraja la ukufunzi. Akiwa katika safari yake mjini Damascus, Syria Nasai alizungumzia sana fadhila za Ahlu Bayti wa Mtume (as) suala ambalo liliwaudhi wapinzani wa kizazi cha Mtume Muhammad na kufikia hatua ya kumpiga alimu huyo. Baada ya hapo alielekea mjini Makka na kufanya makazi mjini hapo. Kati ya vitabu vyake maarufu ni pamoja na kile alichokiita 'Khaswaisw Amiril-Mu'minina Ali' na 'Sunan Nasai.'
Siku kama ya leo miaka 1068 iliyopita, alifariki dunia mjini Herat, magharibi mwa Afghanistan Muhammad Azhari Harawi, mtaalamu wa lugha, elimu ya fiqhi na mfasiri wa Qur'ani Tukufu. Alizaliwa mwaka 282 Hijiria mjini Herat na kuanza kusomea elimu za zama hizo. Akiwa na umri wa miaka 30 na akiwa katika safari ya Hijja, alitekwa nyara na makabila ya vijijini, ambapo katika kipindi hicho cha kuwa mateka aliweza kujifunza lugha fasaha ya makabila hayo. Baadaye alielekea mjini Baghdad, Iraq na kupata kusoma elimu ya dini kutoka kwa maulama wakubwa wa zama hizo na kisha akarudi tena mjini Herat. Moja ya athari za Muhammad Azhari Harawi ni pamoja na kitabu chake cha 'Tahdhibul-Lughah' kitabu ambacho kinazungumzia masuala ya lugha na chenye juzu 15. Aidha msomi huyo ameacha vitabu vingi vikiwemo vya Tafsiri ya Qur'an Tukufu.
Siku kama ya leo miaka 392 iliyopita, aliaga dunia nchini Uholanzi Warren Earp maarufu kwa jina la Arpnus, mwasisi wa Harakati ya Utambuzi wa Ulimwengu wa Mashariki. Arpnus alizaliwa mwaka 1584 Miladia na baada ya kuhitimu masomo yake ya sekondari alijiunga na Chuo Kikuu cha Leiden nchini humo ambapo mbali na kusomea taaluma ya theolojia na kutokana na kuvutiwa sana na masuala ya ulimwengu wa Mashariki, aliamua kusomea lugha ya Kiarabu. Baadaye alifanya safari nchini Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia na kufanya utafiti wa vitabu vya hati za Mashariki huku akiibuka na kipawa cha kuzungumza lugha fasihi ya Kiarabu, Kifarsi na Kiturki. Baada ya hapo aliamua kuandika kitabu cha kanuni nyepesi za lugha ya Kiarabu kwa ajili ya kusomea lugha hiyo. Kadhalika aliweza kujifundisha itikadi za Waislamu na umuhimu wa Qur'ani Tukufu na suna za Bwana Mtume Muhammad (saw) katika dini. Mwaka 1613 Miladia Arpnus aliteuliwa kuwa mhadhiri wa lugha ya Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Leiden nchini Uholanzi na kuandika kitabu cha nahaw katika lugha hiyo.
Siku kama ya leo miaka 166 iliyopita, alizaliwa huko Scotland Robert Stevenson, malenga wa Uingereza. Stevenson alipata umashuhuri baada ya kusambaza kitabu chake alichokipa jina la 'Kisiwa cha Hazina' na kupata mafanikio makubwa. Aidha aliandika visa mbalimbali vya kuvutia ambavyo vilimzidishia umashuhuri katika enzi hizo. Ameandika vitabu kadhaa vya mashairi ya Kingereza. Alifariki dunia mwaka 1894 Miladia akiwa na umri wa miaka 44.
Siku kama ya leo miaka 126 iliyopita, nchi ndogo ya Luxembourg ilijipatia uhuru wake kutoka mikononi mwa Uholanzi. Luxembourg ina upana wa kilomitamraba 1586 huko magharibi mwa Ulaya huku ikipakana na nchi za Ujerumani, Ufaransa na Ubelgiji. Mwishoni mwa karne ya 18 Miladia nchi hiyo iliingia mikononi mwa Ufaransa kufuatia ushindi wa harakati ya wanamapinduzi wa nchi hiyo. Mwaka 1830 Luxembourg iliingia katika udhibiti wa Uholanzi na kisha Ubelgiji na hatimaye kupata uhuru wake katika siku kama ya leo.
Na siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, aliingia madarakani nchini Syria Hafez al-Assad, rais wa zamani wa nchi hiyo baada ya mapinduzi ya kijeshi. Baada ya kumalizika vita vya Waarabu na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967 na kukaliwa na askari wa utawala huo milima ya Golan, kuliibuka tofauti ndani ya chama cha Baath baina ya mirengo miwili ya rais wa wakati huo na Hafez al-Assad aliyekuwa waziri wa ulinzi na kamanda wa jeshi la anga. Tarehe 12 Novemba mwaka 1970 kongresi ya chama cha Baath ilipiga kura ya kumuuzulu Assad wadhifa wa waziri wa ulinzi. Hata hivyo Hafez al-Assad aliongoza mapinduzi siku moja baadaye yaani tarehe 13 Novemba mwaka huo huo na kutwaa madaraka ya taifa hilo. Mwezi Machi mwaka 1971 aliitisha uchaguzi na kuchaguliwa na wananchi na hivyo kutwaa madaraka kikamilifu hadi mwishoni mwa umri wake uliofikia tamati mwaka 2000.