Sayansi na Teknolojia Mpya (1)
Karibuni katika mujmuiko huu mpya wa vipindi ambavyo vinaangazia maendeleo mapya katika sekta za sayansi, teknolojia na tiba. Karibuni kujiunga nasi hadi mwisho ambapo leo tutaangazia mafanikio ya Iran katika kuzalisha dawa ambayo Marekani tu ndiyo iliyokuwa na teknoljia hiyo duniani.
Katika ulimwengu wa leo, ustawi na maendeleo ya nchi hupimwa kwa msingi wa kiwango cha uwezo wa kielimu na kiteknolojia katika nchi husika.
Utafiti na uzalishaji sayansi na teknolojia ni kati ya nukta muhimu zaidi za ustawi na maendeleo ya kiuchumi, kijamii, kiutamaduni, kiviwanda na kisiasa katika nchi.
Hadi sasa duniani hatujaona nchi ambayo imeweza kustawi kiuchumi na kiviwanda pasina kuwa na ustawi wa pande zote katika sayansi.
Kwa msingi huo, ni lazima kila nchi ilipe kipaumbele suala la utafiti na teknolojia kwani hiyo ni nukta muhimu katika uhai na harakati ya maendeleo endelevu na kufikia maisha bora na uhuru wa kweli katika kila jamii.
Tokea zama za kale, Iran imekuwa kitovu cha sayansi na elimu. Katika uchunguzi wa historia ya mwanadamu, tunaona kuwa nchi hii iliwahi kuongoza dunia katika nyuga za sayansi asilia, hisabati, tiba, falaki, kemia n.k. Aidha, baadhi ya wasomi bingwa ambao waliweka msingi katika sayansi mbali mbali walikuwa ni Wairani.
Katika zama za leo pia Iran, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, imeshuhudia mafanikio makubwa ya wasomi wake katika nyuga mbali mbali za sayansi. Ustawi huu ni wa juu kiasi kwamba kiwango cha uzalishaji sayansi nchini Iran katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita unaonyesha kuwa katika mwaka 2015 Iran iliweza kuzalisha asilimia 1.53 ya sayansi duniani.

Makundi yanayoongoza katika uzalishaji sayansi Iran kwa taratibu ni kundi la ufundi na uhandisi, sayansi ya tiba na afya na kisha sekta ya kilimo.
Ni kwa msingi huu ndio tumeamua kuwaandalia vipindi hivi ambayo vitakuwa vikiangazia ustawi wa kisayansi nchini Iran.
Katika makala yetu ya leo tutaanza na tukio la Oktoba 25 mwaka 2016, siku ambayo Iran ilitangaza kuanza kutegeneza dawa inayotumika sana na ambayo teknolojia inayotumika kuitengeneza imekuwa ikimilikiwa na Marekani pekee. Dawa yenyewe inajulikana kama "CinnoRA" ambayo ni kati ya dawa ambazo zinahitaji teknolojia ya kisasa kuzitengeneza.
Dawa hii sasa nchini Iran inategenezwa katika shirika la CinnaGen katika mkoa wa Alborz magharibi mwa Tehran na uzinduzi wake ulihudhuriwa na Waziri wa Afya wa Iran Daktari Seyyed Hassan Ghazizadeh Hashemi.
Dawa ya CinnoRA ni katika familia ya dawa za Monoclonal Antibodies ambazo hutumika kutibu magonjwa yajulikanayo kwa Kiingereza kama autoimmune diseases. Maradhi haya yanatokana na mfumo wa chembehai (seli-cells) zinazopambana na bakteria, virusi na vitu vingine vinavyoleta madhara katika mwili kufanya kazi zaidi kuliko kiwango kinachotakiwa, hivyo huanza kuharibu seli zinginezo mwilini. Mifano ya maradhi hayo ni kisukari, ugonjwa wa viungo/maumivu na uvimbe (athritis), maradhi ya coeliac ambayo huchochea ugonjwa wa utumbo mdogo unaosababishwa na kutovumilia gluten kutoka ngano na magonjwa mengine sugu.

Pamoja na hayo magonjwa ya autoimmune yanaweza kudhibitiwa. Karibu asilimia 80 ya magonjwa haya yana alama zinazofanana na hivyo huwa vigumu kubaini ugonjwa hasa unaomsibu mtu.
Aidha yamkini katika wakati mmoja kukaibika magonjwa kadhaa. Kwa kawaida magonjwa ya autoimmune huanza bila alama au kwa alama chache na kisha kuibuka alama kubwa. Magonjwa ya autoimmumne hupatikana katika aghalabu ya familia ambapo asilimia 75 ya wanaougua huwa ni wanawake. Hali kadhalika utafiti uliofanywa Marekani umebaini kuwa Wamarekani wenye asili ya Afrika na Wamarekani asili yaani Red Indians huwa na hatari zaidi ya kuambukizwa magonjwa hayo.
Aghalabu ya magonjwa ya autoimmune bado hayajajulikana na sababu za kuibuka kwake zimetajwa kuwa ni bakteria au virusi, dawa, kemikali na mazingira anamoishi mgonjwa. Wakati mtu anapougua ugonjwa wa autoimmune yamkini wengine katika familia pia wakaupata ugonjwa huo.
Nukta nyingine katika magonjwa ya autoimmune ni kuwa alama za kuibuka ugonjwa hutofautiana lakini alama za pamoja ni kama vile kuhisi uchovu, homa na udhaifu jumla mwilini.

Magonjwa ya autoimmune huathiri sehemu nyingi za mwili kama vile ngozi, maungo ya mifupa, seli za damu, misuli, mishipa ya damu, tishu unganishi na mfumo wa homoni (kwa Kiingereza endocrine system).
Kama tulivyotangulia kusema dawa ya CinnoRA ni katika familia ya monoclonal antibodies ambazo hutumika kutibu magonjwa ya autoimmune hasa ya ngozi, maungo ya mifupa na utumbo mdogo.
Kwa mujibu wa Daktari Hashemi, Waziri wa Afya wa Iran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi ya pili duniani kupata uwezo na kujitegemea katika uzalishaji wa dawa hiyo ya CinnoRA.
Kiwanda cha kuzalisha madawa hayo kimezinduliwa hapa Iran ili kuiwezesha nchi hii kujitegemea na pia kuwakinga wale wanaolazimika kutumia dawa na madhara au matatizo wakati viwanda vya nje ya nchi vinapokataa kuiuzia Iran dawa hiyo.
Iran kama zilivyo nchi zingine za duniani, haijitengenezei madawa yote inayoyahitajia bali imekuwa ikiyaagiza kutoka nje. Pamoja na hayo, katika miaka ya hivi karibuni Iran imepiga hatua kubwa sana katika kujitengenezea dawa muhimu na hivyo kuelekea katika mkondo wa kujitegemea. Hivi sasa kutokana na uwezo wa Iran kujitengenezea dawa ya CinnoRA, wagonjwa wanaoihitajia nchini wataweza kuipata dawa hiyo kwa bei nafuuu.
Kama anavyosema Mkuu wa Shirika la Chakula na Dawa nchini, hivi sasa kuna mkakati wa Iran kuzisiaidia nchi za Malaysia na Uturuki nazo zimiliki teknolojia hii.

Hali kadhalika katika uzinduzi wa dawa hiyo ya CinnoRA, Waziri wa Afya wa Iran alisema shirika la Cinnagen linaloitengeneza linapanga kuiuza katika soko la kimataifa katika siku za usoni.