Dec 31, 2016 05:58 UTC

Sura ya Al-Qas’as’, aya ya 1-4 (Darsa ya 682)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu. Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 682, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 28 ya Al-Qas’as’.Tunaianza darsa yetu hii kwa aya ya kwanza hadi ya tatu ya sura hiyo ambazo zinasema:

طسم

T'A SIN MIM, (T'.S.M.)

تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْمُبِينِ

Hizi ni Aya za Kitabu kinacho bainisha.

نَتْلُوا عَلَيْكَ مِن نَّبَإِ مُوسَى وَفِرْعَوْنَ بِالْحَقِّ لِقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ

Tunakusomea khabari za Musa na Firauni kwa Haki kwa ajili ya watu wanao amini.

Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 27 ya An-Naml, katika darsa yetu hii ya 682 tutaanza kutoa tarjumi na maelezo ya sura ya 28 ya Al-Qas’as’. Sura hii ina aya 88, na iliteremshwa Makka kabla ya hijra ya Bwana Mtume Muhammad SAW kuelekea Madina. Karibu aya 40 za sura hii, ambazo takriban ni nusu ya aya zake zote zinazungumzia habari za maisha ya Nabii Musa (AS), kuanzia kuzaliwa kwake, utotoni mwake, kipindi chake cha ujana hadi kuoa kwake na hatimaye kubaathiwa na kupewa Utume. Suratul Qas’as’, kama zilivyo sura nyengine 28 za Qur’ani, nayo pia imeanza kwa herufi za mkato; na mara baada ya hapo imeashiria aya za Kitabu hicho cha mbinguni. Kama tulivyowahi kueleza huko nyuma, huenda aya hizo za mkato zinaashiria ukweli huu, kwamba Mwenyezi Mungu SW ameteremsha aya za Kitabu hiki cha mbinguni ambacho ni muujiza wa milele, kwa kutumia herufi hizi hizi za alfabeti zinazotumiwa na watu wote; kwa hivyo kama na nyinyi pia mnao uwezo tumieni herufi hizo kuleta kitabu kilicho mfano wa Qur’ani. Kitabu ambacho aya zake zote zitakuwa wazi na wadhiha kabisa, za kutaalamisha, zenye kupambanua kwa uwazi haki na batili na baina ya njia iliyonyooka na ile ya upotofu iliyopinda. Kisha aya zinaendelea kwa kuashiria habari za Nabii Musa katika zama za utawala wa Firauni na kueleza kwamba: Sisi tunabainisha mambo ndani ya Qur’ani hii kulingana na ukweli na hakika ya mambo bila ya kuchanganya na kitu chochote kisicho na ukweli na uhalisia kuhusu habari za Mitume na kaumu zilizopita. Tunafanya hivi ili waumini wajue kwamba watu wema na waumini katika zama za kabla yao walifikwa na masaibu na misukosuko mikubwa; hivyo wao pia wawe thabiti na wasimame imara kuyakabili matatizo na tabu watakazopata katika zama zao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba kwa kuwa kaida na utaratibu aliouweka Allah katika historia ni wa kufuata kanuni thabiti; kuzielewa kaida za Allah kuhusiana na kaumu zilizopita kunaweza kuwa somo, ibra na mazingatio kwetu sisi na watakaokuja baada yetu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa kupambana na mataghuti na madhalimu ilikuwa ni mbinu iliyotumiwa na Mitume wa Allah; na waumini wanapaswa kuifanya njia ya Mitume kuwa dira na muongozo wao wa kufuata. Kadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba visa vyote vya Qur’ani vinatokana na matukio halisi na ya kweli; si ngano, dhana na mambo ya kubuni yasiyo na uhalisia.

Tunaihatimisha darsa yetu hii kwa aya ya nne ambayo inasema:

إِنَّ فِرْعَوْنَ عَلا فِي الأَرْضِ وَجَعَلَ أَهْلَهَا شِيَعًا يَسْتَضْعِفُ طَائِفَةً مِّنْهُمْ يُذَبِّحُ أَبْنَاءَهُمْ وَيَسْتَحْيِي نِسَاءهُمْ إِنَّهُ كَانَ مِنَ الْمُفْسِدِينَ

Hakika Firauni alitakabari katika nchi, na akawagawa wananchi makundi mbali mbali. Akalidhoofisha taifa moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na akiwaacha watoto wao wanawake. Hakika yeye alikuwa katika mafisadi.

Aya hii inaashiria mambo maalumu aliyokuwa akiyafanya Firauni katika utawala-amri wake na kueleza kwamba: Firauni alikuwa akitumia njia na mbinu tofauti kwa lengo la kuwaweka katika hali ya unyonge na udhaifu Bani Israil na kuwatawala. Kwa kuzusha mifarakano baina ya watu aliwafanya washindwe kuungana dhidi yake na kukabiliana na utawala wake wa kidhalimu. Leo hii siasa zijulikanazo kwa kimombo kama “Divide and Rule” yaani ‘wagawe watu uwatawale’ ni siasa inayotumiwa na madola makubwa kwa madhumuni ya kuziweka chini ya amri na mamlaka yao nchi na mataifa mbalimbali.

Firauni aliwapatia Waqibti ambao walikuwa ndio wakaazi wazawa wa Misri kila aina ya suhula za huduma nzuri za maisha pamoja na kuwakabidhi nafasi na nyadhifa zote za utawala. Lakini mkabala na hayo aliwafanya Bani Israil, ambao walikuwa ni wahajiri waliohamia Misri, kuwa ni watumwa, watwana na wajakazi wa kuwatumikia Waqibti, huku akiwahilikisha kwa kazi ngumu na za sulubu, bila ya kufaidika na suhula za maisha ya kawaida. Wakati taghuti Firauni alipohisi Bani Israil watakuwa ni hatari kwake aliamuru kuwa mtoto yeyote atakayezaliwa miongoni mwa watu hao, kama atakuwa ni wa kike basi abakishwe ili kuongeza idadi ya wajakazi na watumishi wao; na kama atakuwa ni mtoto wa kiume basi achinjwe. Kwa kutumia mbinu hiyo, Firauni alitaka kuzuia ongezeko la kizazi cha vijana na wanaume wa Bani Israil ili wasiweze kuanzisha uasi na mapambano dhidi ya utawala wake wa kitaghuti. Ilikuwa ni katika kipindi hicho alipozaliwa Nabii Musa; na ili kunusuru maisha ya mwanawe, mama yake akalazimika kukitia kitoto hicho kichanga kwenye kisanduku na kukitumbukiza kwenye maji ya Mto Nile. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba ikiwa watu watakuwa na umoja na mshikamano, tawala dhalimu hazitoweza kuwatawala na kuwanyongesha. Na ni kwa sababu hiyo ndio maana madola dhalimu na ya Kiistikbari kila mara hutaka kuchochea na kuzusha mifarakano baina ya watu wa mataifa duniani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kuua moyo wa kishujaa katika nyoyo za wanaume na kuwatumia wasichana na wanawake kwa kutumia kaulimbiu nzuri na ya kuvutia ya uhuru wa wanawake, ni siasa inayotumiwa siku hizi kwa sura tofauti katika dunia inayoitwa ya kisasa. Wapenzi wasikilizaji darsa yetu ya leo imefikia tamati. Tunamwomba Allah aziuangnishe safu za Waislamu, azithibitishe imani zao na awape nguvu za kuweza kukabiliana na madhalimu na mataghuti wa zama hizi. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/