Jan 04, 2017 03:54 UTC
  • Jumatano 4 Januari, 2017

Leo ni Jumatano tarehe 5 Rabiuthani 1438 Hijria sawa na Januari 4, 2017.

Siku kama ya leo miaka 444 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1573, Papa Gregory VII, kiongozi wa Wakristo katika karne ya 16, aliitisha mkutano maarufu kwa jina la mkutano wa 'upokonyaji'. Mkutano huo uliohudhuriwa na wawakilishi wa kidini kutoka nchi za Kikristo, ulichukua uamuzi wa kuwapokonya wafalme wa nchi hizo mamlaka ya kuchagua viongozi wa kidini wa Kikristo. Uamuzi huo uliwakasirisha watawala hao na kusababisha vita vya umwagikaji damu vilivyodumu kwa miaka kadhaa, kati ya Mapapa na Wafalme wa Ulaya.

Papa Gregory VII

Miaka 171 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarahe 5 Rabiul Thani mwaka 1267 Hijiria, gazeti la kwanza la lugha ya Kifarsi lililoitwa 'Waqai'e Ittifaqiyeh' lilianza kuchapishwa mjini Tehran. Gazeti hilo lilianza kuchapishwa wakati wa kutimia mwaka wa tatu wa ufalme wa Nasiruddin Shah Kajjar, kwa amri ya Kansela Mirza Taqi Khan Amir Kabiri. Gazeti hilo lilikuwa likiandika habari za utawala wa wakati huo wa Iran, dunia na makala za kisayansi zilizokuwa zikitafsiriwa kutoka kwenye magazeti ya Ulaya. Gazeti la 'Waqai'e Itifaqiyeh' lilichapishwa hadi toleo nambari 472 na baada ya hapo likaendelea kuchapishwa kwa majina tofauti.

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita inayosadifiana na tarehe 4 Januari 1961, ulifanyika mkutano wa kisiasa huko Casablanca nchini Morocco kwa shabaha ya kubuni msimamo mmoja wa kisiasa wa Kiafrika. Mkutano huo ulihudhuriwa na nchi za Algeria, Ghana, Guinea, Mali, Misri na Morocco. Lengo la mkutano huo lilikuwa kuanzisha kundi moja la kijeshi na soko la pamoja la nchi za Afrika.

Picha ya mji wa Casablanca

Tarehe 15 Dei miaka 38 iliyopita wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran waligoma kwenda madarasani na kufunga masomo wakionesha upinzani wao dhidi ya safari ya rais wa wakati huo wa Marekani, Jimmy Carter hapa nchini na uungaji mkono wake kwa utawala wa Shah. Wakati huo Carter alikuwa akidai kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu na mpinzani wa suala la kuziuzia silaha tawala za kidikteta. Hata hivyo serikali ya Washington ilichukua uamuzi wa kufunga mikataba ya kuuzia silaha nzito utawala wa kidikteta wa Shah na kupuuza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliokuwa ukifanywa nchini Iran. Jimmy Cater alifikia kiwango cha kumwita Shah kuwa ni kiongozi anayependwa na wananchi na kwamba Iran ni kisiwa cha amani. Hata hivyo muda mfupi baadaye wananchi walianza harakati za kudai uhuru na kujitawala na miezi 13 baada ya safari ya Carter mjini Tehran Shah aliondolewa madarakani na ikaanzishwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Jimmy Cater katika safari yake mjini Tehran

Tarehe 4 Januari miaka 6 iliyopita alifariki dunia Mohamed Bouazizi, kijana muuza mboga wa Tunisia, siku 18 baada ya kujichoma kwa moto katika mji wa Buzid akilalamika ukandamizaji na dhulma ya serikali ya nchi hiyo.

Kujichoma moto kijana huyo muuza mboga kuliibua harakati ya wananchi wa Tunisia dhidi ya utawala wa kiufisadi wa nchi hiyo na kuwa sababu ya kupinduliwa dikteta Zainul Abidin bin Ali. Kitendo hicho cha Bouazizi pia kilikuwa cheche ya harakati ya mapinduzi ya wananchi katika nchi nyingine za Kiarabu kama Misri, Libya, Yemen na Bahrain dhidi ya watawala dhalimu na vibaraka wa Magharibi.

Mohamed Bouazizi